Jumanne, 24 Septemba 2024

MAHAKAMA KUU KANDA GEITA WATUMIA FEDHA ZA SHAJARA KUTOA MOTISHA

Na CHARLES NGUSA -Mahakama Kuu, Geita

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Jaji Kevin David Mhina amesema kuwa kutokana na kutotumia karatasi katika shughuli za ofisi wameweza kuokoa fedha zilizokuwa zinatumika kununua shajara, ambazo sasa zitumika kuwapa motisha watumishi. 

 

Hayo yalisema jana tarehe 23 Septemba, 2024 na Mhe. Jaji Mhina wakati  akizungumza na watumishi tisa kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, ambao waliwasili mkoani Geita kwa ziara ya siku moja,wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda hiyo  Mhe.Dkt Deo John Nangela kwa lengo  la  kujifunza matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli za uendeshaji wa mashauri na ofisi kwa ujumla na namna TEHAMA inavyoweza kuokoa fedha za uendeshaji wa ofisi.

 

Awali akiwakaribisha watumishi hao baada ya kuwasili katika ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Geita Mhe. Jaji Mhina alisema Geita kwa sasa hatutumii karatasi katika shughuli zetu za uendeshaji wa mashauri na shughuli zingine za kiofisi kama vile shughuli za kiutawala ambazo zote zinafanyika kwa kupitia mfumo wa Kielektroniki wa Kusimamia Mashauri(CMS) na ofisi mtandao.

 

“Hivyo kwa kiasi kikubwa tumeweza kuepuka matumizi ya karatasi kabisa na kuokoa kiasi kikubwa cha fedha, ambacho kilikuwa kinatumika kununua shajara na badala yake fedha hizi kuelekezwa katika motisha za watumishi wetu ili kuwaongezea morali ya kufanya kazi ikiwa ni pamoja na kuwapatia chakula cha mchana kila siku,”alisema Mhe. Jaji Mhina.

 

Baada ya ukaribisho kutoka Mhe. Jaji Mfawidhi,Mhina watumishi hao, waliweza kupitishwa katika ofisi mbali mbali na kuoneshwa namna shughuli zinavyoendeshwa katika Mahakama hiyo, ikiwa ni pamoja na ofisi inayotumika kwa ajili ya “Visual court”   ambapo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe.Fredrick Lukuna  alisema  “chumba hiki ni kwa ajili ya kuendeshea mashauri kwa njia ya mtandao yaani  “Visual Court” na kwamba hakuna shughuli nyingine inayofanyika humu. Katika chumba hiki huwa tuna Tv kubwa ambayo kwa mfano labda nyie huko mnaweza kuwa na shahidi yuko huku kwetu hivyo mkiwasiliana nasi tunamwita anaingia katika chumba hiki  na anaendelea kutoa ushahidi wake bila wasiwasi.”

 

Aidha, watumishi hao baada ya kumaliza kupitia katika kila ofisi waliweza kuingia ukumbi wa Mahakama ambapo waliweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo mchakato mzima wa ufunguaji wa mashauri mpaka kufikia hatua ya mwisho.Mhe. Lukuna aliwaeleza kuwa mchakato unaanza kwa wakili au ofisi ya mashitaka  na pengine kupitia kiosiki cha Mahakama kwa wale ambao hawana barua pepe wala hawana wakili  hulazimika kuja kwenye kiosiki cha Mahakama kusaidiwa kupandisha nyaraka zao kwenye mfumo na kutumwa kwenda kwa Msajili kwa ajili ya kufanyiwa usajili. 

 

Mhe. Lukuna aliongeza kwamba baada ya shauri kutoka kwa Msajili kama ni la madai  ,huelekezwa kwenda uhasibu kwa ajili ya kutoa namba ya malipo yaani (control namba)  kwa ajili ya kulipia  kisha  kwenda kwa Mhe. Jaji Mfawidhi kwa ajili ya kupangiwa Jaji na upangaji wa mashauri hufanywa na mfumo wenyewe.

 

 Akizungumza kwa niaba ya watumishi waliokuja kujifunza , Mkuu wa msafara, Mhe. Jaji Nangela alipongeza juhudi zinazoendelea katika Kanda hiyo na kuwashukuru kwa namna ambavyo wameweza kuwa Mahakama ya mfano katika matumizi ya TEHAMA na kwamba wamejifunza mengi na wataenda kuyafanyia kazi yale yote waliyojifunza ili kuboresha huduma katika maeneo yao ya kazi.

 

“Tumejifunza mengi siyo tu matumizi ya TEHAMA katika Kanda hii bali pia namna mnavyoshirikiana kuanzia uongozi wa juu hadi watumishi wa chini kabisa, labda tu nitoe angalizo kwamba siwatishi bali nawaambia ukweli kuwa, siku si nyingi tutakuwa juu yenu katika matumizi ya TEHAMA na kwa juhudi alizonazo Mtendaji wetu jambo hili litafanyiwa kazi haraka  na kwamba faida ya mfumo huu pia unaondoa changamoto ya upotevu wa mafaili mahakamani na kupunguza gharama za uendeshaji,”alisema Jaji Nangela.

 

Baada ya hapo watumishi hawa wakiongozwa na wenyeji wao waliweza kutembelea eneo la mradi wa ujenzi wa jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Geita ambalo ni kwa ajili ya Mahakama Jumuishi na kwamba kukamilika kwa jengo hilo, kutasaidia  kuboresha huduma katika Kanda ya Geita kwani huduma zote zitakuwa zinapatikana katika jengo moja.


Watumishi wote waliofika kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, wakiwa  pamoja na baadhi ya watumishi kutoka Mahakama Kuu  ya Tanzania Kanda ya Geita, wakiwa  katika ofisi ya Jaji Mfawidhi Geita baada ya kuwasili mahakamani hapo, wakiendelea na utambulisho.(wa kwanza kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu  ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Kevin David Mhina, (wa kwanza kushoto )ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe.Dkt  Deo John Nangela).



Watumishi  hao wakipata maelezo baada ya kuwasili katika eneo ambalo huonesha kesi za siku hiyo kwa wateja(causelist).


Wahe. Majaji wafawidhi kutoka katika kanda hizo mbili(Sumbawanga na Geita) wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wengine baada ya kuwasili katika jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Geita.

Wahe.Majaji wafawidhi pamoja na watumishi walipotembelea ujenzi wa jengo la Mahakama Jumuishi katika Kanda ya Geita.

 

(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo- Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni