- Jaji Mkuu apokea Majaji kutoka Mahakama ya Korea
- Wameonesha kuvutiwa na maboresho yanayoendele kufanyika
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji wa Mahakama ya Upeo nchini Korea, Mhe. Oh Kyeong-Mi leo terehe 6 Septemba, 2024 amekutana na Uongozi wa Juu wa Mahakama ya Tanzania, chini ya Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali ya kiutendaji katika muktadha mzima wa utoaji haki kwa wananchi.
Viongozi wengine aliokutana nao ni Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Winfrida Korosso, Mhe. Barke Saleh na Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha
Vile vile, walikuwepo Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Victor Kategere, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert na wengine.
Akizungumza baada ya kukutana na Viongozi hao, Mhe. Kyeong-Mi, ambaye aliongozana na Msaidizi wake anayeshughulikia masuala ya utafiti katika Mahakama ya Upeo, Mhe. Yun Hwa-Rang ameeleza kufurahishwa na juhudi zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Nimefurahi kufahamu namna Serikali na Mahakama mnavyofanya kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi, kusaidia katika masuala ya utoaji haki na kisheria na pia kukabili changamoto ili kufikia mafanikio haya. Hii inanitia moyo na kuniwezesha kukabili changamoto ambazo tunakumbana nazo kule Korea,” amesema kupitia Mkalimani.
Ameeleza kuwa hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alitembelea Korea na kukutana na mwenyeji wake, jambo ambalo linaendeleza mahusiano mazuri kati ya nchi mbili na Mahakama,
Mhe. Kyeong-Mi ameelezea furaha yake kwa kupata fursa ya kutembelea Tanzania, jambo ambalo hakulitarajia na kupata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali yatakayosaidia kuboresha huduma za utoaji haki kwa wananchi nchini kwake.
Akizungumza baada ya kumkaribisha mgeni wake, Jaji Mkuu wa Tanzania alimpitisha katika safari ndefu na hatua kadhaa zilizochukuliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika mchakato wa utoaji haki.
Mhe. Prof. Juma ameeleza kuwa Mahakama ya Tanzania ilitafuta Taasisi binafsi kufanya utafiti na kuwauliza wananchi wangependa nini kifanyike na kwamba utafiti huo ndiyo uliosababisha kuanzishwa kwa Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka Mitano wenye lengo la kuboresha na kusogeza huduma karibu na wananchi.
“Baada ya kuja na mpango mkakati huu, tuliiomba Serikali itutafutie fedha za kuweza kuutekeleza. Serikali ilipata mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia. Tangu mwaka 2016 tumejenga Mahakama Kuu zaidi ya 10 na zaidi ya Mahakama Kuu 12 zinajengwa na Mahakama zingine 60 za Wilaya na Mahakama za Mwanzo zinajengwa…
“Tunafanya haya kwa sababu chini ya mpango mkakati, tutahakikisha kufikia mwaka 2025 Tanzania nzima itakuwa inazungukwa na Mahakama katika ngazi mbalimbali. Huu ndio mpango mkakati tunaofanya,” Jaji Mkuu amemweleza mgeni wake.
Mhe. Prof. Juma ameeleza kuwa Mahakama ya Tanzania pia tumepitisha mpango mkakati wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambao utarahisisha mchakato wa utoaji haki kwa wananchi.
Amebainisha kuwa hilo ni eneo ambalo Mahakama ya Tanzania imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuwa na mifumo mingi, ukiwemo wa kusajili mashauri kielektroniki, mfumo wa kutafsiri na unukuzi na mingine.
Akiwasilisha neno la shukrani kwa ugeni huo, Jaji Kiongozi amesema kwa niaba ya Jaji Mkuu na uongozi kwa ujumla, wanawashukuru Majaji hao kwa kuja Tanzania na kupata fursa ya kuitembelea Mahakama ya Tanzania na Mahkama ya Zanzibar.
“Tuna mifumo tofauti ya kimahakama hapa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Ninaamini majadiliano mliyofanya Zanzibar na hapa kwetu yamejenga msingi wa majadiliano zaidi kati ya Taasisi zetu mbili,” Mhe. Siyani amesema.
Amebainisha kuwa Mahakama ya Korea imepiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA kama nyenzo muhimu katika utoaji haki, hivyo hilo ni eneo ambalo wanaweza kuwa na majadiliano zaidi ili kubadilishana uzoefu na ujuzi ili kuboresha huduma za utoaji haki kwa wananchi.
Wakati wa majadiliano na Viongozi, Majaji hao kutoka Korea walipitishwa katika maeneo na mada mbalimbali, ikiwemo masuala ya sheria za kazi na maboresho ya sheria nchini iliyowasilishwa na Mhe. Korosso na mada kuhusu Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania na masuala ya unyanyasaji wa kijinsia kwa ujumla iliyowasilishwa na Mhe. Berke.
Mhe. Dkt. Kikwelo aliwapitisha Majaji hao kwenye mada inayohusu sheria ya haki za binadamu na taratibu za namna ya kuzifikia na pia namna Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kama kiungo muhimu kwa watumishi wa Mahakama kwenye mafunzo.
Naye Mhe. Mwanabaraka aliwapitisha Majaji hao kwenye suala zima la utoaji haki kuhusu familia na ndoa, huku Mhe, Dkt. Rumisha akiwapitisha wageni hao katika safari ya maboresho ndani ya Mahakama ya Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TEHAMA, Bw. Enock Kalege aliwapitsha Majaji hao kwenye mfumo wa teknolojia mahakamani, huku Hakimu Mkazi, Mhe. Felister Masawe akiwapitisha Majaji hao kwenye uendeshaji wa Mahakama Inayotembea na faida zake kwa wananchi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na mgeni wake (hayupo kwenye picha).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni