Jumatatu, 30 Septemba 2024

MAHAKAMA YA TANZANIA YATAJWA KWENYE KONGAMANO LA KIMATAIFA AMERIKA KUSINI

Na MWANDISHI WETU-Mahakama ya Tanzania, Willemstad Curacoa

Kongamano la kimataifa la kupambana na makosa ya miliki bunifu (Itellectual Property Crimes) limefanyika katika Mji wa Willemstad uliopo katika Visiwa vya Curacoa, Amerika ya Kusini.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Shirika la Polisi la Kimataifa (INTERPOL) kwa kushirikiana na UL Standard and Engagement na Serikali ya Curaçao liliwakutanisha jumla ya Maafisa Waandamizi wa Serikali 375 na sekta binafsi kutoka zaidi ya Nchi 65 duniani kwa siku tatu kuanzia tarehe 23 hadi 25 Septemba, 2024. 

Nchi ya Tanzania ilishiriki katika kongamano hilo na iliwakilishwa na wajumbe watatu kutoka Mahakama, Polisi na Tume ya Ushindani.  Mahakama ya Tanzania iliwakilishwa na   Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, ambaye pia ni mratibu wa masuala ya Miliki Bunifu wa Mahakama, Mhe. Upendo Ngitiri, Jeshi la Polisi iliwakilishwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Suleman Nyakulinga na Tume ya Ushindani iliwakilishwa na   Afisa Mwandamizi Mfuatiliaji wa Alama za Bidhaa Bandia, Bi. Grasiana Gallet.

Akiongea na mwandishi wetu, Mhe. Ngitiri ameeleza kuwa mkutano huo umetoa fursakwa watekelezaji wa sheria za miliki bunifu na sekta binafsi kubadilishana uzoefu na kujadili kwa pamoja namna bora  ya kupambana na  kudhibiti  vifaa bandia. 

Mhe.  Ngitiri alisema kuwa, kupitia mkutano huo wameona jinsi bidhaa bandia, mfano vyakula, vipodozi, dawa, vifaa vya magari, vifaa vya umeme na vingine vilivyo tishiokubwa duniani kote. 

Aidha, alibainisha kuwa, madhara ya matumizi ya vifaa hivyo ni makubwa kuliko watu wanavyofikiri hivyo ni muhimu  kuendelea  kutoa elimu kwa wananchi   juu ya madhara ya vifaa bandia na kutekeleza sheria za miliki bunifu.

Mhe.  Ngitiri alisema kuwa, baadhi ya mambo yaliyosititizwa katika kongamano hilo  ni pamoja na kuimarisha ushirikiano katika kupambana na makosa ya miliki bunifu, kubadilishana taarifa ya makosa ya miliki bunifu, kuwa na  sheria madhubuti zinazotoa adhabu kali kwa wahalifu wanaojihusisha na vifaa bandia, kuimarisha  ukaguzi wa vifaa vinavyoingia nchini ili kudhibiti  uingizaji wa vifaa bandia, kuweka utaratibu utakowezesha kutambua vifaa bandia katika  maeneo huru  ya biashara kwa kuwa wahalifu hutumia pia eneo hilo kupenyeza vifaa  bandia na kutoa elimu  kuhusu sheria za miliki bunifu kwa watekelezaji wa sheria hizo. 

Aidha, ilisisitizwa pia kuwa, katika nyakati hizi ambazo teknolojia imekuwa kwa kasi, wahalifu nao hutumia teknolojia ili kufanikisha uhalifu, hivyo ni vyema vyombo vinavyotekeleza sheria za miliki bunifu kwenda sambamba na maendeleo yateknolojia.  

Wakati wa ufunguzi wa Kongamo hilo, Waziri Mkuu wa Serikali ya Curacoa, Mhe.   Gilmar Pisas alisisitiza kuwa, katika ulimwengu wa leo uliounganishwa, ushirikiano ni wa muhimu katika mapambano dhidi ya makosa ya miliki bunifu. 

Waziri Mkuu alisema kuwa utandawazi umefunga hatima zetu pamoja na kufanya ushirikiano wa kimataifa uwe wa lazima. Aliongeza kuwa, Uhalifu wa Miliki Bunifu unatishia usalama wa nchi zetu, ustawi wa watu wetu na uchumi wetu. 

Naye Katibu Mkuu wa INTERPOL, Bw.  Jürgen Stock alisema kuwa, Uhalifu wa miliki bunifu ni tatizo linalokua duniani kote. Vikundi vya uhalifu vilivyopangwa vinajihusisha na biashara ya kupitisha mipaka bidhaa bandia. Mara nyingi kuna uhusiano kati ya biashara hii na aina nyingine za uhalifu, kama ufisadi, na utakatishaji wa fedha. 

Kila eneo duniani na sekta zote za viwanda zinaathiriwa na uhalifu wa uvunjifu wa miliki bunifu, hivyo   jitihada za pamoja zinahitajika.  Alieleza   kuwa, mkutano huo umetoa msukumo mpya na juhudi za pamoja za kukabiliana na tishio la vifaa bandia, ambavyo si tu vinadhuru afya ya umma, bali pia vinaharibu uchumi na kudhoofisha jamii.

Moja ya mada iliyojadiliwa katika kongamano hilo ni uhusishwaji wa Mahakama  katika  utafutaji wa matokeo chanya  dhidi ya mapambano ya  makosa ya miliki bunifu.  Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Marekani, Mhe.  Bernice Donald alieleza kuwa, jukumu kubwa la Mahakama katika suala hilo ni kuhakisha kuwa, mashauri yanayotokana na uvunjifu wa sheria za miliki bunifu  yanashughulikiwa  vema na   kwa weledi na adhabu kali inatolewa kwa wahalifu wanojihusisha na vifaa bandia. 

Alisema kuwa, kwa Marekani Majaji hupata mafunzo kutoka kwa wataalamu wa miliki bunifu na vilevile “The National Judicial College” imekuwa ikitoa mafunzo ya miliki bunifu kwa Majaji. 

Jaji Donald alisisitiza kuwa, ni muhimu Majaji wawe na uelewa mzuri wa   sheria za miliki bunifu ili kuwasaidia kuamua vyema mashauri ya miliki bunifu. Aliongeza kuwa, Jaji hajiandikii maamuzi mwenyewe bali anawaandikia wadaawa walioleta kesi mbele yake, walaji na jamii nzima na maamuzi yake huwa kanuni hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa anashughulikia kila hoja kwa usahihi na maamuzi yake yanakuwa kwa mujibu wa sheria na kununi za miliki bunifu zilizopo.

Jaji Donald alipongeza kuwa moja ya hatua kubwa iliyochukuliwa Africa ni kuandaliwa kwa “Africa Regional Intellectual Property (IP) Bench Book” ambayo Mahakama ya Tanzania inashiriki katika maandalizi ya nyenzo hiyo muhimu. 

Alisema ni jambo la kujivunia kuona jitihada za kuandaa “Africa Regional IP Benchbook” kwa ajili ya kutoa muongozo kwa Majaji ya namna bora ya kushughulikia mashauri ya miliki bunifu. 

Wakati wa kongamano hilo, Jaji Donald alimsimamisha Mhe. Upendo Ngitiri  na kumtaja kama mmoja wa viongozi wanao shiriki kuandaa Africa Regional IP Bench book akiwakilisha Mahakama ya Tanzania.

Mhe. Jaji Donald alishiriki pia kwa karibu katika maandalizi ya nyenzo hiyo muhimu ambayo iliandaliwa kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani na kamati maalum ambayo inaundwa na Majaji 14   wa Afrika na Naibu Msajili mmoja chini ya uratibu wa Bi. Tanya Hill, aliyekuwa Mshauri wa Serikali ya Marekani wa masuala ya Miliki Bunifu na Udukuzi wa Komputa.  Muongozo huo hivi sasa upo kwenye hatua za mwisho na ulishakabidhiwa WIPO kwa ajili ya mapitio na maboresho. 

 

Kutoka kushoto ni Mkuu wa Chuo cha Kimataifa cha INTERPOL cha Wachunguzi wa Uhalifu wa Makosa ya Miliki Bunifu, Bw. Jorge Fainstein Gastrell’s na kulia ni Mhe. Upendo Ngitiri, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu na Mratibu wa Masuala ya Milki Bunifu wa Mahakama.

Waziri Mkuu wa Curacao, Mhe. Gilmar Pisas (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri (wa pili kutoka kulia), Kamishina Msaidizi Mwadamizi wa Polisi, SACP Suleman Nyakulinga (wa kwanza kushoto) na mshiriki mwingine wa Kongamano hilo.

Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Marekani, Mhe. Bernice Donald (wa pili kutoka kushoto) akiwa na wawezeshaji wengine waliofanya mawasilisho kuhusu uhusishwaji wa Mahakama  katika  utafutaji wa matokeo chanja  dhidi ya  makosa ya miliki bunifu.

Washiriki kutoka Nchi mbalimbali duniani walioshiriki Mkutano huo katika hoteli ya Curacoa Mariot Hotel.

 Mhe. Upendo Ngitiri, Naibu Msajili wa  Mahakama ya Tanzania.

Kutoka kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama ya Tanzania, Mhe Upendo Ngitiri na  Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Marekani, Mhe. Bernice Donald.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

 













Hakuna maoni:

Chapisha Maoni