Jumatatu, 9 Septemba 2024

MKUTANO WA KIMATAIFA KUHUSU HAKI MAZINGIRA WAANZA NCHINI RWANDA

Rais Kagame ataka Mahakama huru, imara inayotekeleza sheria kulinda mazingira

Mahakama ya Tanzania yapongezwa kwa kutuma wawakilishi wengi.

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Kigali

Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame leo tarehe 9 Septemba, 2024 amefungua Mkutano wa Kimataifa unaofanyika jijini hapa kuwaleta pamoja Majaji na Mahakimu kutoka Jumuiya ya Madola kuzungumzia haki mazingira. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Kagame amesema kuwa utungaji wa sheria na sera za mazingira ni muhimu katika kujenga mustakabali safi na endelevu zaidi.

“Muhimu zaidi ni kuwa na Mahakama imara na huru inayotekeleza sheria na kutanguliza maslahi ya wananchi,” amesema.

Mhe. Kagame amedokeza kuwa duniani kote, halijoto inaongezeka kwa viwango visivyo na kifani, huku ubora wa hewa ukizidi kupungua, jambo linalomweka mwanadamu hatarini.

“Kuna mengi yanayoweza kufanywa kulinda mazingira na kutoa haki pale inapostahili kama kutakuwepo na ushirikiano wa karibu na watekelezaji wa pamoja wa sheria na Majaji huru na wazoefu,” amesema.

Aliwataka Mahakimu na Majaji kutumia jukwaa hilo kujadili changamoto ya rushwa na mlundikano wa mashauri, huku akibainisha kuwa uhalali wa mfumo wowote wa haki utatokana na imani waliyonayo wananchi ndani yake.

Awali akiwasilisha neno la ukaribisho katika Mkutano huo, Jaji Mkuu wa Rwanda, Mhe. Dkt. Faustin Ntizilyayo ameeleza kuwa maafisa wa Mahakama wanabeba jukumu la kipekee la kudumisha na kuendeleza haki katika masuala ya mazingira. 

“Mkutano huo unalenga kuimarisha uelewa wa pamoja wa uhuru wa Mahakama na kuchunguza jinsi mamlaka mbalimbali ndani ya Jumuiya ya Madola yanaweza kushughulikia changamoto zinazopatikana kwa pamoja,” amesema.

Kabla ya ufunguzi rasmi, Mahakama ya Tanzania ilitangazwa kufanya vizuri kwa kuleta wawakilishi wengi kwenye Mkutano huo wapatao 32, ikizidiwa kwa idadi ndogo na Mahakama ya Kenya iliyoshika nafasi ya kwanza, huku Mahakama ya Malawi ikishika nafasi ya tatu.

Katika Mkutano huo, Jaji Mkuu ameongozana na Majaji wawili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Barke Sehel, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) na Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.

Wengine ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani na Majaji wengine wa Mahakama Kuu, Mhe. John Kahyoza, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), Mhe. Ilvin Mugeta, Mhe. Butamo Philip, Mhe. Yohana Massara na Mhe. Dkt. Adam Mambi.

Viongozi wengine ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert, Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi, Katibu wa Jaji Kiongozi, Mhe. Aidan Mwilapwa na Katibu wa Msajili Mkuu, Mhe. Dkt. Jovin Bishanga.

Wapo pia Viongozi wa JMAT, Mhe. Shaibu Mzandah, ambaye ni Makamu wa Rais, Mhe. Lazaro Magai, ambaye ni Katibu Mkuu, Mhe. Mary Kallomo, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu na Mkuu wa Secretariat, Mhe. Nemes Mombury, ambaye ni Katibu Mwenezi na Mhe. Devota Ksebele, ambaye ni Mweka Hazina na Mahakimu wengine, Mhe. Adeline Kashura na Mhe. Hassan Chuka, ambaye pia ni Katibu wa Msajili wa Mahakama ya Rufani.

Mkutano huo wenye kauli mbiu ya “Haki Mazingira” umeandaliwa na Jumuiya ya Madola kwa kushirikiana na Mahakama ya Rwanda.

Baada ya ufunguzi wa Mkutano huo, Majaji na Mahakimu wameaza kujadili vipengele mbalimbali vya kisheria na kitaasisi ili kuimarisha usimamizi na upatikanaji wa haki kuhusiana na mazingira na jukumu kuu la Mahakama katika kudumisha haki mazingira. 

Kupitia mada na mijadala mbalimbali, wajumbe wa Mkutano huo watakuwa na fursa za kubadilishana uzoefu kati yao na kuunda uhusiano wa kudumu miongoni mwao.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifuatilia mambo mbalimbali yaliyokuwa yanajiri wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Chama cha Majaji na Mahakimu kutoka Jumuiya ya Madola. Picha chini akiwa na Majaji Wakuu wengine (mstari wa mbele) wakati wa hafla hiyo.




Sehemu ya Majaji kutoka Tanzania (juu na mbili chini) wakijadiliana mambo mbalimbali.





Viongozi wa Mahakama (juu na chini) wakifuatilia matukio mbalimbali.



Viongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania wakiwa kwenye Mkutano huo.


Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame akizungumza wakati anafungua Mkutano huo.


Jaji Mkuu wa Rwanda, Mhe. Dkt. Faustin Ntizilyayo akizungumza wakati anatoa ukaribisho kwenye Mkutano huo.

Washiriki wa Mkutano kutoka Tanzania.

 
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji kutoka Tanzania.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wote wa Mkutano kutoka Tanzania.


Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji Wakuu wa Mahakama kutoka Jumuiya ya Madola, akiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ( wan nne kutoka kushoto) 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni