Alhamisi, 19 Septemba 2024

RAIS SAMIA AMUAPISHA JAJI MPYA WA MAHAKAMA KUU

  • Apongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri
  • Jaji Mkuu amkaribisha Jaji mpya mahakamani, amwahidi ushirikiano 

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 19 September 2024 amemuapisha Bi. Nenelwa Mwihambi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Uapisho huo umefanyika katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Bunge na Mahakama, akiwepo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Akson, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka.

Katika hafla hiyo, kulikuwepo pia na uapisho wa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Baraka Ildephonce Leonard ambaye anachukua nafasi ya Bi. Mwihambi baada ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

Akizungumza baada ya uapisho wa Viongozi hao aliowateua tarehe 16 Septemba, 2024, Rais Samia ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kazi nzuri inayofanya ya kusikiliza mashauri kwa haraka na kutoa uamuzi kwa wakati.

Ameeleza kuwa hivi karibuni alikutana na wafanyabiashara ambao wanaonesha kufurahishwa jinsi usikilizaji wa mashauri unavyokwenda, ikiwemo kutoa hukumu kwa wakati na mashauri kutokaa mahakamani kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais amewapongeza Viongozi wote walioapishwa na kuwataka kutekeleza majukumu yao kwa haki kulingana na dhamana waliyopewa na kwa kuzingatia viapo walivyoapa.

Naye Spika wa Bunge aliungana na Viongozi wengine wa kitaifa kwa kuwapongeza wateule hao na kuwatakia kila heri katika majukumu yao mapya.

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mkuu amemshukuru Rais Samia kwa kuteua Jaji mmoja wa Mahakama Kuu, hatua ambayo imesaidia kupunguza mzigo wa mashauri kwa kila Jaji aliyepo hivi sasa.

Mhe. Prof. Juma ameeleza kuwa kabla ya uteuzi huo, Jaji mmoja wa Mahakama Kuu alikuwa na mzigo wa mashauri 238 ambayo anatakiwa kuyamaliza kwa mwaka na kwamba baada ya uteuzi huo mzigo umepungua hadi mashauri 236.

Amemkaribisha Mhe. Nenelwa mahakamani na kumhakikishia kuwa atapata kila aina ya msaada ili aweze kutekeleza majukumu yake mapya kikamilifu.

Hata hivyo, amemkumbusha kuwa majalada atakayopangiwa yanabeba maisha na mali za watu, hivyo hukumu atakazitoa zitapimwa na kupandishwa kwenye tovuti ya Mahakama na wakati mwingine kukosolewa kwa kukatiwa rufaa katika Mahakama ya Rufani.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimwapisha Bi. Nenelwa Mwihambi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Mhe. Nenelwa Mwihambi akila kiapo.

Mhe. Nenelwa Mwihambi (katikati) akila kiapo cha maadili pamoja na Viongozi wengine walioteuliwa na Rais Samia hivi karibuni kushika nyadhifa mbalimbali.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Nenelwa Mwihambi akiwa na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Baraka Ildephonce Leonard baada ya kuapishwa na Rais Samia kushika nyadhifa hizo. 

(Picha na Ikulu)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni