Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Mhe. Mizengo Peter Pinda amemtunuku Shahada ya Uzamivu ya Sheria (PhD in Law) Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea, Mhe.Dkt. Emmanuel Kawishe.
Mhe. Kawishe alitunukiwa Shahada hiyo katika sherehe ya Mahafali ya 43 ya Chuo hicho zilizofanyika tarehe 05 Desemba, 2024 katika viwanja vya Kawawa Ujiji mkoani Kigoma.
Mgeni Rasmi katika sherehe za Mahafali ya Chuo Kikuu Huria Tanzania alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ambapo katika hotuba yake, alisema kuwa, jamii ya Watanzania inayo matarajio makubwa kwa wahitimu hao wa ngazi mbalimbali kwakuwa ndio chachu katika maendeleo ya nchi.
Aidha, Mhe. Majaliwa aliwapongeza Wahadhiri na Wahitimu wa ngazi zote kwa jitihada zao za kupambana katika kuhakikisha ndoto zao zinakamilishwa kwa kutunukiwa elimu ya ngazi walizofikia huku wakiwa wameiva kitaaluma.
Waziri Mkuu aliwapa pia pongezi Wahitimu hao kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais, Dkt. Isdor Philip Mpango ambao wote kwa pamoja wamewapongeza wahitimu wote wa Chuo Kikuu Huria ambapo matunda yake yameonekana katika mahafali hiyo.
Akiendelea kuzungumza katika sherehe za Mahafali hayo ambayo yalikuwa na jumla ya Wahitimu 4,307 wa kozi na ngazi mbalimbali za elimu, Mhe. Majaliwa alisema, "Nakipongeza Chuo chetu Kikuu Huria Tanzania kwa kuamua kufanya mahafali haya ya 43 hapa mkoani Kigoma."
Akizungumza katika Mahafali hayo, Makamu Mkuu wa Chuo, Mhe. Prof. Elifas Bisanda aliweka bayana fursa zinazopatikana mkoani Kigoma, alisema kufanyika kwa mahafali hayo mkoani humo huwawezesha kupata wageni wengi ambapo huduma mbalimbali hutolewa, na kuwaeleza wenyeji wa Mkoa huo kuwa, wajipange kwa kuwa Mahafali hayo yanaweza kurudi kufanyika tena mkoani Kigoma.
“Tunaamini yapo wageni wamejifunza na wenyeji pia hivyo nimevutiwa na utaratibu huu wa Chuo maana unavutia wananchi wengi kusoma Chuo hiki kutokana na upatikanaji wa huduma upo karibu nao kwa kozi mbalimbali ambazo wakulima, wafanyabiashara, wavuvi, wafugaji, wafanyakazi wataweza kusoma vizuri na kuhitimu vizuri kwa ngazi yoyote na kutunukiwa elimu inayofanana inayotolewa na Chuo chochote hapa nchini,” alisema Prof. Bisanda.
Aliongeza kuwa, katika mahafali hiyo wapo wahitimu 4,307, ambapo kati ya hao 2,070 sawa na asilimia 48.1 ni jinsia ya kike na wapo wahitimu 55 watunukiwa wa Shahada za Uzamivu (PhD) na kati ya hao 20 ni akina mama, hata hivyo katika Shahada za Uzamili (Masters) jumla ya wahitimu ni 430 na kati ya hao wanawake ni 156, na Shahada ya kwanza wahitimu ni 1,396, kati ya hao wanawake ni 611.
Kwa upande wa ngazi ya Stashaha wahitimu walikuwa 702 na kati ya hao wanawake ni 353, Astashahada 1,619 na kati hao 896.
Mkuu wa Chuo hicho aliweka bayana kuwa, hadi kufikia tarehe 05 Desemba, 2024 jumla ya Wahitimu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania ni 62,217.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea, Mhe. Dkt. Emmanuel Kawishe akifuatilia kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi wa sherehe za Mahafali ya 43 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania, ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (hayupo katika picha) katika sherehe za Mahafali zilizofanyika tarehe 05 Desemba, 2024 katika viwanja vya Kawawa Ujiji mkoani Kigoma. Mhe. Dkt. Kawishe amehitimu Shahada ya Uzamivu ya Sheria (PhD in Law).
Waziri Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Pinda, akimvalisha kofia ikiwa ni alama ya kumtunuku Shahada ya Uzamivu ya Sheria (PhD in Law) Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea, Mhe. Dkt. Emmanuel Kawishe katika Mahafali ya 43 yaliyofanyika tarehe 05 Desemba, 2024 katika Viwanja vya Kawawa Ujiji-Kigoma.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea, Mhe. Dkt. Emmanuel Kawishe (kulia) akiwa na Msimamizi wake wakijongea mbele ya meza kuu ili kutunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Sheria (PhD in Law) katika sherehe za Mahafali ya 43 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) iliyofanyika tarehe 05 Desemba, 2024 katika Viwanja vya Kawawa Ujiji mkoani Kigoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassimu Majaliwa Majaliwa (aliyevaa joho kushoto) na Waziri Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Mhe. Mizengo Peter Pinda (kulia) wakiwa katika maandamano ya kitaaluma kuashiria kuanza kwa sherehe za mahafali ya Chuo hicho zilizofanyika tarehe 05 Desemba, 2024 katika viwanja vya Kawawa Ujiji mkoani Kigoma.
Picha ya pamoja, wa nne kulia ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Msatafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Mhe. Mizengo Peter Pinda,(wa tano kulia) pamoja na wageni mbambali wa meza kuu wakati wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza kwa sherehe za Mahafali ya 43 ya Chuo hicho yaliyofanyika tarehe 05 Desemba, 2024 katika viwanja vya Kawawa Ujiji mkoani Kigoma.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Arusha)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni