- Amtaka kuzingatia weledi, uwajibikaji
Na FAUSTINE
KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani jana tarehe 12 Desemba, 2024
alimwapisha Mhe. John Chacha kuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Hafla hiyo fupi ya uapisho
ilifanyika katika Ofisi ya Jaji Kiongozi iliyopo kwenye jengo la Mahakama Kuu “Mwembeni”
jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Viongozi kadhaa wa Mahakama, wakiwemo
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Salma Maghimbi na Mhe. Dkt. Angelo
Rumisha.
Akizungumza baada ya uapisho
huo, Jaji Kiongozi alimweleza Naibu Msajili mpya kuwa nafasi aliyoipata siyo
upendeleao bali inatokana na kufanya kazi vizuri kwenye maeneo aliyokuwa anayahudumia.
Alimtaka kuzingatia weledi,
uadilifu na uwajibika anapotekeleza majukumu yake mapya kama salamu ya Mahakama
ya Tanzania inavyoeleza na kwamba hatakiwi kubweteka.
“Nafasi uliyoipata siyo
upendeleao, bali inatokana na kazi nzuri unayoifanya. Usibweteke, endelea
kufanya kazi. Ishi kiapo chako na kumbuka yanayoelezwa kwenye salamu ya
Mahakama, yaani weledi, uadilifu na uwajibikaji, haya yatakusaidia katika kazi zako,”
Mhe. Dkt. Siyani alisema.
Naye Jaji Kiongozi mstaafu
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Fakih Jundu, akizungumza katika hafla hiyo,
alimkumbusha Naibu Msajili mpya kuwa kazi aliyopewa ni muhimu ndani ya Mahakama
kwani Naibu Msajili ndiyo kiungo kati ya Mahakama na Wananchi.
“Kwa hiyo, unatakiwa kusimama
imara kuiunguanisha Mahakama na Wananchi. Wewe ni kiungo muhimu kwenye maeneo
mengi, kuhakikisha mashauri hayakwami na kuwa na mipango mizuri itakayosaidia
mashauri kusikilizwa kwa haraka,” Mhe. Jundu alisema.
Alimhimiza Naibu Msajili
mpya kutokuwa na upendeleo kwa mtu yoyote na kujiepusha na vishawishi ambavyo
vinaweza kusababisha kuharibu kazi na kuifanya Mahakama kuwa na sifa mbaya.
“Zingatia sana maadili ya
kazi yako ili usipate matatizo yatakayokupeleka sehemu mbaya. Usifanye watu
wasikufikie na tumia lugha ya kiungwana. Matatizo na malalamiko ya watu
yafanyie kazi na kupatia ufumbusi kwa haraka,” alisema.
Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu, Mhe. Sundi Fimbo na wengine.
Naibu Msajili, Mhe. John Chacha (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi kutoka Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania. Picha mbili chini akiwa na Viongozi wengine waandamizi wa Mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni