Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Butamo Phillip amefanya ukaguzi wa robo mwaka katika Gereza la Mahabusu Mkuza na kuwataka wafungwa waliopo katika gereza hilo kujifunza miradi mbalimbali inayofanywa gerezani hapo kupitia miradi hiyo maana lengo halisi la kuwa mahali hapo ni kujifunza na kutoka na ujuzi mbalimbali.
Pamoja na ukaguzi huo aliofanya tarehe 03 Desemba, 2024, Mhe. Philip ametembelea miradi ya Gereza hilo na kubaini miradi mbalimbali inayofanywa gerezani hapo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba za maafisa, karakana ya kuchomelea na ya uselemala, mradi ya kutengeneza matofali, kilimo cha mbogamboga pamoja na duka la vinywaji.
Mhe. Philip aliwapongeza Viongozi wa Gereza la Mkuza kwa ubunifu huo na kuwataka wafungwa waliopo katika Gereza hilo kujifunza kupitia miradi hiyo ambapo amesema, “lengo la kuwa hapa ni kuwafanya muwe bora mjitahidi kujifunza maana maeneo ya kujifunzia ufundi yapo na hata mkitoka hapa mnakuwa bora zaidi.”
Akizungumza na mahabusu, wafungwa pamoja na wadau wa haki jinai alioambatana nao, Jaji Phillip aliwaomba Mahakimu na Mawakili wa Serikali pindi wanapoahirisha mashauri watoe sababu za kuahirisha shauri hilo ili washtakiwa waelewe na vilevile kuepuka sitofahamu kwa mahabusu.
Akizungumzia suala la kuchelewa kwa upatikanaji wa nakala za hukumu, Mhe. Phillip alisema kwa sasa zinatolewa kwa wakati ambapo alieleza kuwa, na hilo lilithibitishwa na Kiongozi Mkuu wa wafungwa na mahabusu (Nyapala) gerezani kwa kusema utaratibu uliowekwa na Mahakama kwa sasa ni mzuri hakuna tena kusubiri nakala ya hukumu kwa muda mrefu.
Pamoja na ziara hiyo, Jaji Phillip alitembelea pia Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo Mailimoja.
Mhe. Phillip alizipongeza Mahakama ya Mwanzo Mailimoja, Mahakama ya Wilaya Kibaha na Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani kwa kufanya kazi kwa uzalendo japo zipo changamoto ambazo zinatatulika.
Alipongeza pia kazi nzuri inayofanywa na Mahakama ya Mwanzo Mailimoja ambapo alisema pamoja na uchache wa watumishi wa Mahakama lakini kazi bado zinafanyika hazijasimama kwa namna yoyote ile.
Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Aziza Mbadjo aliwakumbusha Wasaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Mwanzo Mailimoja kujaza rejesta kwa usahihi ili ukaguzi unapofanyika kusiwe na haja ya kuitisha jalada la shauri husika kwa kuwa taarifa zote zinakuwepo tayari kwenye rejesta.
Katika ukaguzi huo, Mhe. Phillip aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama, Mhe. Aziza Mbadjo, Afisa Tawala wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Lucy Kilukaizile, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha ambaye pia ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani pamoja na wadau wa haki jinai.
Ukaguzi huo hufanyika kila baada ya miezi mitatu na lengo hili ni kuona kama changamoto za kipindi cha ukaguzi wa mwisho zimefanyiwa kazi na kuona kama kuna changamoto mpya zilizoibuka kwa kipindi cha miezi mitatu.
Afisa Tawala wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Lucy Tilukaizile akitoa ufafanuzi baada ya kuulizwa swali na mtumishi.
Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha wakimsikiliza, Mhe. Butamo Phillip alipokuwa akizungumza na watumishi baada ya ukaguzi Mahakama hiyo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Butamo Phillip, Mhe. Butamo Phillip (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Aziza Mbadjo (wa pili kulia), Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Cecilia Gomesi ( wa kwanza kulia), Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai na Afisa Tawala wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Lucy Tulukaizile pamoja na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha Pwani.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni