Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile amekutana na watumishi wapya katika kikao cha kumpokea Naibu Msajili mpya wa Kanda hiyo, Mhe. Fadhili Mbelwa.
Akizungumza na watumishi hao tarehe 11 Desemba, 2024 ofisini kwake, Mhe. Rwizile alimkaribisha Mhe. Mbelwa katika Kituo chake kipya cha kazi na kumueleza kuwa, Mahakama Kigoma wana ari kubwa ya kufanya kazi kwa ushirikiano na kwa bidii ili kuhakikisha Mpango Mkakati wa Mahakama unafikiwa kwa kiwango kikubwa.
Aidha, Jaji Mfawidhi huyo aliwakaribisha pia watumishi wapya pamoja na waliohamia katika Kanda hiyo na kuwataka kufanya kazi zao kwa kuzingatia weledi na kuhakikisha wanaishi katika maadili ya utumishi wa umma pamoja na kupenda kujifunza kazi zaidi ya moja.
Aliwataka pia kujiendeleza katika elimu ambazo zitawafanya kutokuwa nyuma ya wakati katika matumizi ya teknolojia inayokuja kuboresha na kupunguzia na kurahisisha baadhi ya majukumu.
“Teknolojia inapozidi kukua kwa kasi inapunguza majukumu hivyo ni vyema tukakutwa tuna uwezo wa kufanya jukumu lingine ili uendelee kuwa wa thamani kwa mwajiri wako,” alisema Mhe. Rwizile.
Hata hivyo alisema kuwa, Mahakama inao Mkataba wa Huduma kwa Mteja unaomtaka kila mmoja katika nafasi yake kuhakikisha mteja anapofika mbele yake apate huduma nzuri mpaka anaifikia hukumu ya shauri lake na mlolongo anaoupitia wa huduma unakuwa mzuri unaomjengea imani kwa Mahakama.
Aliwakumbusha pia kuzingatia muda wa kufika kazini na kutoka kazini ambapo alisema, “nitafurahishwa na mtumishi ambaye atafika mapema kazini na kufanya majukumu yake kwa mpangilio na kufikia saa 9:30 Alasiri awe amehitimisha majukumu yake kwakuwa tunao wajibu pia wa kijamii ni vema kutumia muda wa baada ya kazi za ofisi kujiimarisha katika mazoezi na mambo mengine tunayopaswa kuyafanya katika jamii yetu.”
Kwa upande wake Naibu Msajili mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa alisema amefurahishwa na mapokezi yake na ameahidi kushirikiana na kila mtumishi katika Kanda hiyo kuhakikisha shughuli za Mahakama zinakwenda kama zilivyopangwa.
Mhe. Mbelwa alisema kuwa, anajivunia timu ya Majaji waliopo Kanda ya Kigoma na timu ya watumishi waliopo kwani wana ari kubwa ya kufanya kazi.
Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo alimshukuru Jaji Mfawidhi kwa niaba ya Jaji Mkuu kwa kuendelea kuongeza nguvu kazi ya watumishi wa kada mbalimbali wanaokuja kuongeza nguvu ya utendaji katika Kanda hiyo. Aidha, alimshukuru Jaji Mfawidhi huyo kwa maelekezo na nasaha mbalimbali alizotoa kwa watumishi wapya 11 wa kada tofauti tofauti.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akisisitiza jambo wakati wa kikao cha watumishi wapya kilichofanyika ofisini kwake terehe 11 Desemba, 2024.
Naibu Msajili mpya wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa, akisaini kitabu cha wageni alipowasili kuripoti katika Kituo chake kipya cha kazi Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.
Naibu Msajili mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akisalimiana na Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Festo Sanga (kulia) mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Mahakama Kuu Kigoma.
Naibu Msajili mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma. Kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay na kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo.
Watumishi wapya wakiwa katika kikao na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (hayupo katika picha) pamoja na Viongozi wa Kanda hiyo akiwemo Naibu Msajili mpya wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa (wa kwanza kulia) aliyepokelewa siku hiyo katika Mahakama hiyo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni