- Jaji Mkuu aipongeza Serikali kwa uwezeshaji kuboresha mfumo utoaji haki
Na FAUSTINE
KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kukubali
kuchukua mkopo Benki ya Dunia wa Dola za Kimarekani milioni 91 ili kuboresha
mfumo wa utoaji haki, ikiwemo Vituo Jumuishi wa Utoaji Haki tisa vipya
vinavyojengwa katika Mikoa mbalimbali nchini.
Mhe. Prof. Juma ametoa pongezi
hizo leo tarehe 10 Desemba, 2024 kama Mgeni Rasmi katika sherehe ye maadhimisho
ya miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia
Temeke ambayo imefanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini
Dar es Salaam.
“Benki ya Dunia na
Serikali ya Tanzania ziliridhia Awamu ya Pili ya Mpango wa Maboresho Baada ya
Majengo Jumuishi sita kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 6 Oktoba, 2021 na kuonyesha mafanikio
makubwa katika utoaji haki. Kwa sasa, Vituo Jumuishi vinajengwa Simiyu, Geita,
Katavi, Njombe, Songwe, Songea, Lindi, Singida na Pemba…
“Tunaweza kusema, mafanikio
ya Kituo Jumuishi Temeke yamechangia kujenga hoja za kujengwa vituo jumuishi
vingine tisa. Tusherehekee mafanikio ya miaka mitatu ya Kituo Jumuishi Temeke
kama chachu ya ujenzi wa Vituo Jumuishi tisa zinazoendelea kujengwa nchini,”
amesema.
Jaji Mkuu amebainisha
kuwa sherehe hizo za Kituo Jumuishi Temeke ni miaka mitatu tangu Rais Samia alipozindua
majengo sita Jumuishi ambayo ni fahari ya Tanzania yaliyojengwa Dodoma, Dar es
Salaam (Temeke na Kinondoni), Arusha, Mwanza na kukumbusha kuwa hatua hiyo ni
matunda ya ushirikiano wa karibu baina ya Serikali ya Tanzania na Benki ya
Dunia.
Mhe. Prof. Juma ameeleza
pia kuwa sherehe hizo ni kumbukumbu ya mbinu mpya iliyotumiwa na Serikali ya
Tanzania kutatua changamoto ya muda mrefu ya uchakavu mkubwa na kutokuwepo na miundombinu
ya Mahakama na kwamba Serikali ya Tanzania ilikopa kutoka Benki ya Dunia ili
Mahakama ya Tanzania itekeleze Mpango Mkakati wa Miaka Mitano kupitia Programu
ya Maboresho.
“Kwa mara ya kwanza Benki
ya Dunia ilijitokeza katika maboresho ya huduma za utoaji haki kwa kiasi
kikubwa. Tunasherehekea miaka mitatu ya Benki ya Dunia kujitokeza kufadhili
ujenzi wa miundombinu ya Mahakama kwa kutambua kuwa utoaji wa haki kwa weledi,
ufanisi na uwazi ni wezeshi kwa ukuaji wa uchumi, biashara na ustawi wa
wananchi,” amesema.
Jaji Mkuu amefafanua kuwa
kutokana na unyeti wa mashauri ya ndoa, talaka, watoto, matunzo ya watoto na mirathi,
Mahakama ya Tanzania iliamua kati ya vituo sita jumuishi zilizokuwa
zikitarajiwa kujengwa, angalau Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kimoja kitumike
kushughulikia migogoro ya kifamilia.
“Maamuzi haya ya kutenga
kituo Jumuishi Temeke yalisukumwa na tatizo la uwepo wa idadi kubwa ya mashauri
ya mirathi pamoja na mashauri ya ndoa na talaka. Mfano, kati ya mwaka 2017-2019
kulikuwepo na mashauri 7,600 ya mirathi ambapo kati yake mashauri 3,765
yalikuwa katika ngazi ya Mahakama za mwanzo. Mashauri ya ndoa na talaka
yalikuwa takribani 4,200 kati ya mwaka 2017-2019,” amesema.
Aidha, Mhe. Prof. Juma
amebainisha kuwa msukumo na uhitaji wa kuwa na Kituo Jumuishi Mahsusi kwa mashauri
ya watoto, ndoa, talaka, matunzo na mirathi ilitoka katika asasi za kiraia na
wadau wengine wa haki za binadamu kama Chama Cha Wanasheria Wanawake (TAWLA),
Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Chama Cha Majaji na Mahakimu
Wanawake (TAWJA).
“Katika nyakati tofauti
tofauti, vyama hivi viliwasilisha hoja zao kwa uongozi wa Mahakama. Hivyo basi,
leo hii tunasherehekea pia za miaka mitatu ya Mahakama ya Tanzania kuwasikiliza
wadau walioomba kuanzishwa kwa Mahakama ya Masuala ya Familia Temeke Dar es
Salaam,” amesema.
Jaji Mkuu ameeleza pia kuwa
kupitia Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Programu ya Maboresho, Mahakama ya
Tanzania ilijenga hoja kwa Serikali ya Tanzania, na Serikali ya Tanzania
ilikubali kuwa, Mahakama ya Tanzania ni mtekelezaji muhimu wa Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025.
“Mahakama ikisogeza
huduma zake sehemu zote Tanzania na ikitekeleza majukumu yake ya utoaji haki
kwa ufanisi, weledi na uwazi itaichangia Tanzania kuyafikia Malengo Makuu
Matano yaliyotajwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025,” amesema.
Mhe. Prof. Juma ameyataja
baadhi ya malengo hayo yanayotekelezwa na Mahakama ni pamoja na kuwepo kwa
mazingira ya amani, usalama na umoja; kujenga utawala bora; na kujenga uchumi
imara unaoweza kukabiliana na ushindani na nchi nyingine duniani.
Akizungumza kabla ya
kumkaribisha Jaji Mkuu kuzungumza na wananchi, Jaji Mfawidhi wa Kituo cha
Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwake, Kituo kimefanikiwa kuhudumia
idadi kubwa ya wananchi ambao wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku kwa ajili ya
kupata huduma mbalimbali zinazotolewa.
Amesema kuwa kitakwimu, ndani ya mwaka wa kwanza wa kutoa huduma, mwaka
2021 hadi 2022, Kituo kilipokea wastani wa wateja 700 kwa siku, mwaka wa 2022
hadi 2023, Kituo kilikuwa kinapokea wastani wa wateja 971 na kwa mwaka 2023
hadi 2024, Kituo kimekuwa kinapokea wastani wa wateja 890 kwa siku. Hivyo wanajivunia
kwa idadi hiyo ambayo ni ishara kwamba wananchi wanaridhika na huduma
zinazotolewa Kituoni.
“Kitakwimu, tangu kuanzishwa kwa Kituo hadi kufikia tarehe 26 Agosti, 2024,
Kituo kimehudumia wateja wapatao 580,610; kati ya hao wanaume wakiwa 265,985,
sawa na asilimia 45.8, wanawake 311,183, sawa na asilimia 53.6 na watoto
waliohudumiwa ni 3,442, sawa na asilimia 0.6,” Mhe. Mawanabaraka amesema.
Kwa upande wa mashauri, amebainisha pia kuwa kipindi cha mitatu kuanzia
tarehe 27 Agosti 2021 mpaka tarehe 26 Agosti 2024, Kituo kimesajili jumla ya
mashauri 22,929, kati ya hayo yaliyoamuliwa ni 20,077, ambayo ni sawa na
asilimia 88 ya mashauri yote yaliyofunguliwa na yale ambayo hayakusikilizwa ni 2,852,
sawa na asilimia 12.
Viongozi mbalimbali wa Mahakama na wadau mbalimbali wamehudhuria sherehe
hizo, wakiwemo Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Makamishna wa Tume ya
Utumishi wa Mahakama, Majaji Wastaafu wa Mahakama Kuu, Wasajili na Watendaji wa
Mahakama, Mawakili wa Kujitegemea, Viongozi wa Dini, Wanafunzi wa Shule ya
Sheria kwa Vitendo na Watumishi wa Kituo Jumuishi Temeke.
Wakati wa maadhimisho hayo, Jaji Mkuu wa Tanzania alizindua taarifa maalum ambayo imeandaliwa na Kituo hicho kuonesha kazi mbalimbali ambazo zimefanyika katika kipindi cha miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni