Alhamisi, 5 Desemba 2024

MAHAKAMA YA TANZANIA YANG’ARA BONANZA LA MICHEZO EAMJA

Yafanikiwa kushika namba moja katika michezo ya kabumbu, netiboli, kuvuta Kamba

Majaji, Mahakimu Afrika Mashariki waweka majoho pembeni, washiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali

Na MARY GWERA, Mahakama-Arusha

Mahakama ya Tanzania imeibuka mshindi wa kwanza katika shindano la michezo ya mpira wa miguu (kabumbu), netiboli, kuvuta kamba  iliyochezwa kwenye Bonanza la Michezo la Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA).

Bonanza hilo lililosheheni michezo mbalimbali limefanyika leo tarehe 05 Desemba, 2024 kuanzia majira ya saa 9 alasiri katika Viwanja vya Agakhan jijini Arusha ikiwa ni sehemu ya ratiba ya matukio ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA) unaofanyika jijini Arusha.

Michezo mbalimbali ikiwemo kabumbu, netiboli, bao, karata na mingine ilianza kuchezwa na Timu/washiriki kutoka Tanzania, Zanzibar, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na Sudani ya Kusini majira ya saa 10 jioni huku ikiwa na mashabiki lukuki waliojawa na bashasha.

Takribani dakika 15 tangu kuanza kwa Mchezo wa mpira wa Miguu, Timu ya Mahakama ya Tanzania ambayo ilikuwa imejumuisha na washiriki kutoka Zanzibar ilifanikiwa kuinyuka bao la kwanza timu ya wenzao Kenya na Uganda.

Haikuishia hapo, Timu hiyo iliendelea kuichapa Timu ya Kenya na Uganda kwa mabao mengine matatu zaidi na kufanya idadi ya magoli kufikia manne hadi kufikia mwisho wa mchezo huo ambao ulichukua dakika 70.

Mbali na mpira wa miguu, Timu ya Netiboli ya Mahakama ya Tanzania iliyojumuisha pia washiriki wa Zanzibar na Rwanda nayo iliwashangaza mashabiki kwa kuitandika jumla ya mabao saba (7) dhidi ya tatu.

Kadhalika, katika mchezo wa kuvuta kamba, Timu ya wanawake Tanzania na Zanzibar wamefanikiwa kuchukua kinyang’anyiro huku Timu ya kuvuta kamba ya wanaume kutoka Kenya na Uganda nayo ikafanikiwa kuchukua ushindi.

Aidha, katika michezo mingine mfano ya vijiti, kutembea na mayai na kadhalika kumekuwa na washindi mchanganyiko wakiwemo Watanzania, Wakenya, Waganda na washiriki wengine.

Bonanza la michezo lilihitimishwa majira ya saa 1:30 usiku kwa kutoa medali kwa washindi wa michezo tajwa pamoja na makundi mbalimbali yaliyoshiriki kufanikisha kufanyika kwa michezo hiyo.

Kesho tarehe 06 Desemba, 2024 ikiwa ni siku ya mwisho ya Mkutano wa 21 wa EAMJA, washiriki takribani 400 wa Mkutano huo watapata pia nafasi ya kufanya utalii katika Hifadhi ya Ngorongoro.


Timu za Mpira wa Miguu za upande wa Tanzania, Zanzibar (wenye sare za dark bluu) wakiwa katika picha na Timu ya Kenya na Uganda leo tarehe 05 Desemba, 2024 baada ya kumaliza kulisakata kabumbu katika viwanja vya Agakhan jijini Arusha.
Mchezo wa karata ukiendelea kuchezwa.


Mtanange ukiendelea katika Viwanja vya Agakhani jijini Arusha.

Mashabiki nao hawakuwa nyuma katika kuwatia joto wachezaji. Wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Anorld Kirekiano na aliyeshikilia vuvuzela ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya pamoja na sehemu ya watumishi wengine kutoka Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Zanzibar.

Mashabiki wakifuatilia mchezo wa kabumbu leo tarehe 05 Desemba, 2024 katika viwanja vya Agakhan jijini Arusha. 

Mchezo wa karata.

Timu ya Netiboli kutoka Mahakama ya Tanzania ikishangilia baada ya ushindi ya bao saba kwa tatu.


Picha mbalimbali za Bonanza la Michezo ya Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA).

(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Arusha)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni