Alhamisi, 5 Desemba 2024

TANZIA; MTUMISHI WA MAHAKAMA AFARIKI DUNIA

 TANZIA


Marehemu Farida Ally Semba enzi za uhai wake.

Mahakama ya Tanzania inasikitika kutangaza kifo cha mtumishi wake, Bi. Farida Ally Semba aliyekuwa akihudumu katika Ofisi ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania jijini Dar es Salaam, kwa nafasi ya Msaidizi wa Ofisi akiwa kama Msaidizi wa Ofisi Mkuu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, marehemu Farida alikutwa na umauti mnamo alfajiri ya saa 11 ya tarehe 4 Desemba, 2024 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa amelazwa kipatiwa matibabu tangu Ijumaa ya tarehe 29 Novemba, 2024 mkoani Dar es Salaam baada ya kuugua kwa vipindi tofauti na kulazwa.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, msiba huo upo nyumbani kwa marehemu eneo la Kibaha Picha ya Ndege manispaa ya Ubungo na kwamba mazishi yatafanyika Ijumaa tarehe 6 Disemba, 2024 wilayani Lushoto, Mkoa wa Tanga.

Marehemu Farida Ally Semba aliajiriwa na Mahakama ya Tanzania mwaka 1991 kama Msaidizi wa Ofisi Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na kuhudumu mpaka mwaka 1994. Aidha, mwaka 1994 alihamishiwa Mahakama ya Mwanzo Ilala jijini Dar es Salaam na baadaye marehemu alihamishiwa Ofisi za Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, marehemu alihudumu katika Ofisi ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania mpaka mauti yalipomfika.

Mahakama ya Tanzania inaungana na ndugu, jamaa na marafiki kuomboleza msiba huu wa kuondokewa na mpendwa wetu.

BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA JINA LA BWANA LIHIMIDIWE.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni