· Yaweka Historia Kuwa na Jengo lake tangu kuanzishwa kwake
Na Lydia Churi- Tume ya
Utumishi wa Mahakama, Dodoma
Tume
ya Utumishi wa Mahakama imekabidhiwa jengo lake na
Mkandarasi wa ujenzi, Kampuni ya CRJE (East Africa) LTD baada ya kazi ya ujenzi
kukamilika jijini Dodoma.
Hafla ya kukabidhiwa kwa jengo hilo imefanyika jana tarehe 30 Novemba, 2024 kwenye kiwanja namba 3 Block D katika eneo la NCC, pembeni ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Akizungumza
mara baada ya kukabidhiwa jengo hilo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa
Tume ya Utumishi wa Mahakama Bw. Rickneville Mwanri aliishukuru Kampuni ya CRJE
(East Africa) Ltd kwa kufanikisha kazi ya ujenzi wa jengo hilo la Tume ambalo
amesema litabadili mazingira ya kazi na kuwa bora zaidi kwa watumishi wa Tume.
“Tume
haijawahi kuwa na jengo lake tangu kuanzishwa kwake hivyo kujengwa na
kukamilika kwa jengo hili ni hatua kubwa, naipongeza sana Serikali kwa
kuwezesha ujenzi huu. Jengo hili sasa litakuwa ni chachu kwa watumishi kuongeza
kasi ya utendaji kazi”, alisema Mkurugenzi huyo.
Alisema
kuwa kiwanja kilichotumika kujenga jengo la Tume kina ukubwa wa mita za mraba
9,590, na kina hati yenye namba DOM008194 iliyotolewa tarehe 22 Julai, 2022.
Aliongeza kuwa jengo hilo limegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 14.3
(14,300,000,000).
Awali
akikabidhi jengo hilo, Meneja wa Mradi wa Kampuni ya CRJE (East Africa) Ltd Bw.
Xie Xiang aliishukuru Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa
kuiamini Kampuni yake na kuipa kazi kubwa ya ujenzi wa jengo hilo la Ofisi.
Naye Mshauri Mradi huo, Architect Queen Mduma
aliishukuru Tume kwa kuwaamini kusimamia Mradi wa ujenzi wa Jenggo lake
ambapo amesema kazi imefanyika kitaalamu na kwa kuzingatia taratibu zote za
ujenzi wa majengo makubwa.
Kujengwa kwa jengo la Ofisi za Tume ya Utumishi wa
Mahakama jijini Dodoma kunaweka historia kwa Taasisi hiyo kumiliki jengo lake
la ofisi tangu kuanzishwa kwake.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba
kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Tume
hii imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika
Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa
Mahakama Sura ya 237.
Jengo la Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama lililomalizika kujengwa jijini Dodoma.
Sehemu ya Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mahakama ya Tanzania pamoja na wafanyakazi wa Kampuni ya CRJE (East Africa) Ltd wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya hafla ya kukabidhiana jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama lililomazika kujengwa jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni