Na NAOMI KITONKA-Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, Temeke
Kuelekea
Wiki na Siku ya Sheria nchini, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis
Juma leo tarehe 14 January 2025 ametangaza Kauli Mbiu itakayojadiliwa kwenye
maadhimisho hayo katika mkutano wa Waandishi wa Habari uliofanyika katika
ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke.
Kauli
hiyo iliyotolewa na Jaji Mkuu ambayo inalenga kuelezea nafasi ya Taasisi mbalimbali
katika utoaji haki inasema, “Tanzania 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia
Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”
Akizungumza
katika mkutano huo, Jaji Mkuu alisema, “Kauli mbiu hii inatusaidia kutumia
mkakati na ufanyaji wa maboresho ya Mahakama hasa tunapoiendea dira mpya ya
matumaini ya mafanikio 2050 ya uchumi wa kiwango cha kati ngazi ya juu. Kama Mahakama tumejipanga kufanikisha mpango
huo na tutakuwa na mjadala mpana wa kujiangalia kama Taasisi kwa sababu
tumekuwa ni mmoja wa watekelezaji wakubwa wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya
mwaka 2025…
“…kila
Taasisi ya umma inapaswa kujua dhana ya haki ya madai sio tu suala la mahakamani
ila kuanzia kwao na kila mahali,hatuwezi kukwepa wajibu wetu wa mageuzi makubwa
ya kitaasisi na pia kujua umuhimu wa kutafuta wataalamu wa mabadiliko na
maboresho katika Taasisi kuendea kasi ya maendeleo ya dira yetu,” aliongeza
Jaji Mkuu.
Kauli
mbiu hiyo pia ina lengo la kuzitahadhari Taasisi zinazosimamia haki-madai
kuhusu umuhimu wa kufanya matayarisho ya hayo mabadiliko makubwa ili yawezeshe
na kuepuka kuwa vikwazo kwa Tanzania kuwa Taifa lenye maendeleo yanayolingana
na Nchi zenye uchumi wa kipato cha kati ngazi ya juu.
Katika mkutano huo Jaji Mkuu aliongozana na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Sharmillah Sarwatt na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Naibu Msajili, Mhe. Evodia Kyaruzi, Mtendaji wa Mahakama ya Kituo Jumuishi Temeke, Bwana Samson Mashalla,Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Watoto, Mhe. Mwamini Kazema, Mahakimu kutoka Mahakama ya Mwanzo na Mahakama ya Wilaya pamoja na watumishi wa kada mbalimbali kituoni hapo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni