Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Jumla ya Wanafunzi 168 wa Kidato cha tatu kutoka Shule ya Sekondari Mikamba iliyopo kata ya Kidahwe mkoani Kigoma wamefanya ziara Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma yenye lengo la kujifunza kuhusu mamlaka ya Mahakama na muundo wake na huduma zinazotolewa na Mhimili huo.
Akizungumza na wanafunzi hao tarehe 20 Oktoba, 2025 Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo alisema kuwa, “Ninyi ndio Taifa la kesho ambalo mtakuja kuwa Viongozi mbalimbali wakiwemo Mahakimu na Majaji ambao mnapaswa kuwa na uadilifu, weledi, na uwajibikaji kama tufanyavyo sisi kwa sasa, hivyo ongezeni juhudi katika masomo yenu na mkumbuke kumtanguliza Mungu katika yote, ili awatangulie mfaulu vizuri masomo yenu, mje kuwa Viongozi bora katika jamii na Taifa letu.”
Aidha, Mhe. Tarimo alitoa rai kwa wanafunzi hao kuwa, elimu waliyoipata wasikae nayo bali waisambaze katika jamii zao wanazotoka kwani Mahakama ni wazi kwa kila mtu na ndio Mhimili pekee wenye mamlaka kamili ya kutoa haki katika jamii.
Naye Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola akishirikiana na Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Kanda hiyo, Mhe. Hassan Galiatano walitoa elimu kwa wanafunzi hao ili kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.
“Mahakama ni kati ya Mihimili mitatu ya Dola kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatimiza wajibu wake kisheria na ni Chombo pekee chenye mamlaka ya utoaji haki nchini, hivyo ina wajibu wa kutoa haki bila kuacha shaka,” alisema Mhe. Msola.
Aliwaeleza wanafunzi hao kuwa, Mahakama inatoa haki kwa mujibu wa Katiba na Sheria mbalimbali na kwamba hujikita katika usahihi wa shauri na ushahidi uliopo mbele ya Mahakama husika ili kuhakikisha haki inatolewa mapema ipasavyo bila upendeleo wa aina yoyote.
Kwa upande wake, Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama hiyo, Mhe. Hassan Galiatano aliwataka wanafunzi hao kuendelea kuipenda Mahakama na kuitembelea mara kwa mara maana imejipambanua katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utendaji wake, ambapo aliwajulisha kuwa Mahakama inafanya shughuli zake za usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya Mfumo wa Kielektroniki ya Uratibu na Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) unaomuwezesha mwananchi yoyote kupata fursa ya kutumia simu janja kupata taarifa zake za kimahakama.
Kwa upande wake Kiongozi wa Wanafunzi hao, Bi. Jenia Josephat aliushukuru Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kwa kuridhia wao kufanya ziara yao katika Mahakama hiyo pamoja na mafundisho waliyoyapata kutoka kwa viongozi hao, kwamba ni chachu kwao katika kukua na kuongeza juhudi katika masomo yao.
Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola (katikati), Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe.
Hassan Galiatano (kushoto) na Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Sekondari Mikamba (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mikamba.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni