Jumatatu, 13 Aprili 2026

CHAMA CHA MAJAJI NA MAHAKIMU MUSOMA CHAFANYA MKUTANO

Na FRANCISCA SWAI – Mahakama, Musoma.

Chama cha Majaji na Mahakimu (TMJA) Kanda ya Musoma, kilifanya mkutano wake tarehe 10 Aprili, 2026 kujadiliana masuala ya kiutendaji na kuweka mikakati mbalimbali kuhakikisha suala la utoaji wa haki linatekelezwa kama inavyokusudiwa bila mkwamo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya, alisistiza umuhimu wa Mahakimu kuhudhuria mikutano, kwani ndio sehemu pekee wanapopata nafasi ya kukutana kwa wingi na kujadiliana mambo mbalimbali.

“Kanda inavyo vikao mbalimbali ikiwemo cha menejimenti, kusukuma mashauri, vikao vya Mawakili na Madalali na vingine vingi, ila huko kote Mahakimu hawaingii kwa pamoja, isipokuwa katika mkutano wa TMJA ambao ndio jukwaa pekee linalowawezesha Mahakimu kwa umoja wao kukukutana na kujadili masuala yanayowahusu,” alisema Mhe. Mtulya.

Pamoja na kuwasisitiza umuhimu wa mkutano huo, Jaji Mfawidhi aliwahimiza kuzingatia na kutekeleza maelekezo ya Viongozi mbalimbali, ikiwemo kusimamia utekelezaji wa malengo yanapangwa na Menejimenti ya Kanda, kwani yanasaidia kuboresha utendaji wa kazi na kuwezesha Kanda ya Musoma kushika nafasi ya pili kitaifa kwa kasi nzuri ya usikilizaji wa mashauri.

Aidha, katika mkutano huo mada mbalimbali zilizijadiliwa ikiwa ni pamoja na ushughulikiwaji wa mashauri ya mirathi. Wajumbe wa mkutano huo walikumbushana maelekezo mbalimbali ya Viongozi kuhusu utekelezaji wa masuala ya mirathi, changamoto wanazokutana nazo katika kushughulikia masuala hayo pamoja na namna bora ya kuyashughulikia.

Vilevile, wajumbe wa mkutano huo kwa pamoja walishiriki mafunzo yaliyotolewa kwa njia ya mtandao kuhusu matumizi ya Sheria ya Kiislam katika Mahakama za Mwanzo. Mafunzo hayo yaliyotolewa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania.

Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu (TMJA), Kanda ya Musoma, Mhe. Hadija Masala (aliyesimama) akitoa neno la utangulizi wakati wa mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu (TMJA) Kanda ya Musoma.

Wajumbe wa mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu (TMJA) Kanda ya Musoma wakiwa wamesimama kwa ajili ya kutoa heshima zao na kuwakumbuka watumishi wa Kanda ya Musoma waliofariki katika kipindi cha mwaka 2025/2026, akiwemo aliyekuwa Hakimu Mahakama ya Mwanzo Bunda Mjini, Mhe. Patrick Masenge na aliyekuwa Dereva Mahakama ya Wilaya Bunda, Bw. Abriel Lazaro.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (aliyesimama) akitoa neno la ufunguzi wakati wa mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu (TMJA) Kanda ya Musoma.

Mjumbe wa mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu (TMJA) Kanda ya Musom,a Mhe. Oscar Lyimo (aliyesimama) akiwasilisha mada kuhusu ushughulikiwaji wa mashauri ya mirathi wakati wa mkutano huo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Monica Ndyekobora (wa pili kushoto), akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo.

Wajumbe wa mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu (TMJA) Kanda ya Musoma, ambao pia ni Majaji wa Mahakama Kuu Musoma, wakifurahia jambo wakati wa mkutano huo, wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya, katikati ni Jaji wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Marline Komba na wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Kamazima Kafanabo.

Wajumbe wa mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu (TMJA) Kanda ya Musoma wakifuatilia kwa makini mafunzo yaliyotolewa kwa njia ya mtandao kuhusu matumizi ya Sheria ya Kiislam katika Mahakama za Mwanzo.

Sehemu ya wajumbe wa mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu (TMJA) Kanda ya Musoma wakiwa katika picha ya pamoja.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni