Jumanne, 5 Mei 2026

TMJA MOROGORO YAADHIMISHA SIKU YA WAFANYAKAZI DUNIANI KWA MAFUNZO

  • Yafanya pia uchaguzi wa Viongozi

Na ASHA JUMA-Mahakama Morogoro

Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Mkoa wa Morogoro hivi karibuni kiliungana na Wafanyakazi wengine duniani kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani inayofanyika kila mwaka tarehe 1 Mei, kwa kufanya mkutano maalum uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Kongamoyo mkoani Morogoro.

Maadhimisho hayo yalilenga kuwakutanisha pamoja Majaji na Mahakimu kwa ajili ya kusherehekea siku hiyo muhimu kwa  kubadilishana uzoefu, pamoja na kujengeana uwezo kupitia mafunzo mbalimbali ya kitaaluma yanayohusu utendaji kazi wa Mhimili wa Mahakama.

Miongoni mwa mada zilizotolewa ni Muhtasari wa Utamaduni wa Mahakama (Judicial Culture) nchini Tanzania, ambapo washiriki walipata fursa ya kujifunza kuhusu misingi, maadili, mila na taratibu zinazoongoza utendaji kazi wa vyombo vya utoaji haki.

Ilielezwa kuwa utamaduni wa Mahakama unajengwa juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria mbalimbali pamoja na kanuni na miongozo ya Mahakama.

Msingi huo ni muhimu katika kuhakikisha haki inatendeka kwa usawa na ufanisi. Mada hii iliwasilishwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Morogoro, Mhe. Stephen Magoiga.

Aidha, mada nyingine iliyowasilishwa ni Muhtasari wa Sifa na Tabia Muhimu za Uongozi katika Mhimili wa Mahakama (Overview on Judicial Leadership Attributes), iliyolenga kuwajengea washiriki uelewa kuhusu sifa zinazopaswa kuzingatiwa na Viongozi wa Mahakama.

Baadhi ya sifa hizo ni pamoja na uadilifu, hekima na busara katika kufanya maamuzi, uwazi na uwajibikaji, uwezo wa kusimamia haki kwa usawa, pamoja na kuwa na uongozi wenye maadili na mfano bora kwa wengine. Mada hii ilitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim.

Baada ya mafunzo hayo, wajumbe walipata nafasi ya kufanya uchaguzi wa Viongozi mbalimbali wa TMJA kwa Mkoa wa Morogoro. Katika uchaguzi huo, Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Morogoro, Mhe. Aisha Sinda, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na Mhe. Mbaraka Mchopa akachaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti. Nafasi ya Katibu ilichukuliwa na Mhe. Joseph Ngwega, Mhe. David Luvanga akachaguliwa kuwa Mwakilishi wa Taifa, na Mhe. Latifa Kassim Mohammed kuchukua nafasi ya Mhazini.

Kwa ujumla, maadhimisho hayo yamekuwa na mafanikio makubwa kwa kuimarisha mshikamano miongoni mwa wanachama wa TMJA, kuongeza uelewa wa kitaaluma na kuweka msingi imara wa uongozi bora ndani ya Mhimili wa mahakama mkoani Morogoro.

Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Morogoro, Mhe. Aisha Sinda aliye chaguliwa kuwa Mwenyekiti TMJA Morogoro.

Mhe. Mbaraka Mchopa aliye chaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.

Mhe. Joseph Ngwega  aliye chaguliwa kuwa Katibu.

Mhe. David Luvanga aliye chaguliwa kuwa Mwakilishi wa Taifa.

Mhe. Latifa Kassim Mohammed aliyechukua nafasi ya Mhazini.

Mahakimu pamoja na Majaji wakiwa katika viwanja vya Kongamoyo.

HABARI HII IMEHARIRIWA NA FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni