Ijumaa, 19 Juni 2026

WATUMISHI KUTOKA CHUO CHA UFUNDI ARUSHA WATEMBELEA MAHAKAMA KUU DIVISHENI YA BIASHARA

Na KEVIN HEZRON-Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Dar es Salaam

Watumishi kutoka Chuo cha Ufundi Arusha (Arusha Technical College), jana tarehe 18 Juni, 2026, walitembelea Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika usimamizi na utunzaji wa kumbukumbu.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu – Divisheni ya Biashara, Mhe. Kevin Mhina, aliwashauri wageni hao kufanya juhudi za kuhamia katika mfumo wa utendaji usiotegemea karatasi.

Alieleza kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali hurahisisha utekelezaji wa shughuli za Taasisi, huongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wakati.

Katika ziara hiyo,  Afisa TEHAMA Mwandamizi wa Mahakama Kuu – Divisheni ya Biashara, Bi. Amina Said, aliwasilisha mada kuhusu Kanzidata ya Hifadhi na Usimamizi wa Nyaraka (Record Centre Database) iliyobuniwa kwa lengo la kuboresha usimamizi wa majalada yaliyofungwa.

Aliwaeleza wageni hao changamoto zilizokuwepo kabla ya kuanzishwa kwa kanzidata hiyo, ikiwemo ugumu wa kufuatilia maeneo yalipohifadhiwa majalada na ucheleweshaji wa upatikanaji wa taarifa muhimu.

Aidha, aliwasilisha namna kanzidata hiyo inavyowezesha usajili wa majalada, utambuzi wa maeneo yanapohifadhiwa, ufuatiliaji wa Watumishi wanaochukua majalada kwa matumizi ya muda pamoja na utoaji wa taarifa na ripoti mbalimbali.

Kanzidata hiyo imeleta maboresho makubwa katika kuokoa muda, kuongeza ufanisi wa kazi, kupunguza upotevu wa majalada na kuboresha utoaji wa huduma.

Baada ya kupata mawasilisho na kushuhudia onesho la matumizi ya kanzidata hiyo, wageni hao walionesha kuvutiwa na ubunifu huo na kutoa pongezi kwa Mahakama Kuu – Divisheni ya Biashara kwa kutumia TEHAMA kutatua changamoto za kiutendaji.

Kwa pamoja walieleza kuwa wamejifunza mambo mengi yatakayowasaidia katika kuboresha mifumo ya usimamizi wa kumbukumbu katika Taasisi yao.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Kevin Mhina akiwakaribisha Watumishi kutoka Chuo cha Ufundi Arusha.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Kevin Mhina akizungumza na wageni kutoka Chuo cha ufundi Arusha. Kushoto kwake, ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Susan Kihawa,  na Kulia kwake ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Bw. Anatory Kagaruki.

Bi. Amina Said, Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, akitoa wasilisho juu ya matumizi ya kanzidata ya usajili, usimamizi na utunzaji wa kumbukumbu.

Wageni kutoka Chuo cha ufundi Arusha, wakisikiliza kwa makini mawasilisho yaliyoandaliwa.

 

Picha na Iman Kasian, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni