Na CHIMPAE MSELE – Mahakama, Katavi
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Katavi, Mhe.
Godfrey Ntemi Isaya, ameipongeza Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA) ya Mahakama Kuu Katavi kwa kuandaa mfumo wa kielektroniki wa kuhifadhi kumbukumbu za mirathi unaojulikana kama e-Mirathi Archive
System (MAS).
Pongezi hizo zimetolewa tarehe 9 Oktoba, 2026 katika Ukumbi wa Mafunzo uliopo ndani ya jengo la Mahakama Kuu
Katavi, wakati wa uzinduzi wa mfumo huo. Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Isaya ameipongeza Idara ya TEHAMA kwa kufanya kazi kwa weledi na kuanzisha mfumo
unaolenga kurahisisha utunzaji na upatikanaji wa nyaraka za mirathi.
Amesema mfumo huo utasaidia kuharakisha upatikanaji wa haki mapema
ipasavyo, kupunguza usumbufu
unaojitokeza katika utafutaji wa kumbukumbu za mirathi, hususan katika Mahakama
za Mwanzo mkoani Katavi.
Aidha, Mhe. Isaya ameonesha kuridhishwa na ubunifu huo wa kuandaa mfumo e-Mirathi Archive System uliofanywa
na watumishi wa Idara ya TEHAMA kwa juhudi na
kazi kubwa waliyoifanya. Akieleza
kuwa utakuwa na mchango muhimu katika kuboresha utendaji wa shughuli za Mahakama.
Mhe. Isaya amebainisha kuwa mfumo huo utasaidia kupunguza changamoto
zinazowakabili yatima, wajane na wagane katika kufuatilia masuala ya mirathi,
kwa kuwezesha kumbukumbu kupatikana kwa haraka pale zinapohitajika. Hatua hiyo itasaidia kupunguza muda wa kusubiri nyaraka na kuondoa baadhi
ya usumbufu ambao umekuwa ukijitokeza katika usimamizi wa mashauri ya mirathi.
Katika hatua nyingine, amewataka Mahakimu kuhakikisha kuwa mashauri yote
ya mirathi yaliyofunguliwa hapo awali katika Mahakama wanazosimamia yanaingizwa kwenye mfumo huo. Amesisitiza kuwa
kufanya hivyo kutasaidia kuboresha usimamizi wa mashauri na kupunguza
ucheleweshaji wa utoaji wa haki katika masuala ya mirathi.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, mfumo wa e-Mirathi Archive System
(MAS) umeandaliwa kuhifadhi kumbukumbu mbalimbali za mashauri ya mirathi, ikiwemo
mienendo ya mashauri, nakala za hukumu, maamuzi na amri za Mahakama. Pia, mfumo huo utahifadhi vielelezo, taarifa za wasimamizi wa
mirathi, wadhamini na wanufaika wa mirathi.
Vilevile, mfumo huo una uwezo wa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (SMS)
kwa wasimamizi na wanufaika wa mirathi ili kuwakumbusha kuhusu hatua muhimu za
mashauri yao, ikiwemo muda wa kufunga shauri la mirathi unapokaribia au
unapofika.
Jaji Isaya amesema mfumo huo una manufaa makubwa kwa wanufaika wa
mirathi, wasimamizi wa mirathi na watendaji wa Mahakama, kwa kuwa utasaidia kuhifadhi taarifa sahihi, kuimarisha usalama
wa kumbukumbu na kupunguza uwezekano wa watu wasiohusika kujiingiza katika
mashauri ya mirathi kwa lengo la kujipatia manufaa yasiyostahili. Amesema matumizi ya mfumo huo yanatarajiwa kuongeza ufanisi katika
usimamizi wa mashauri ya mirathi na kuchangia utoaji wa haki kwa wakati,
ikilinganishwa na changamoto zilizokuwepo awali.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Masjala ndogo Katavi, Mhe. Godfrey Ntemi Isaya akizindua mfumo wa kielektroniki
wa e-Mirathi Archive System (e-MAS)
Hakimu Mkazi Mwandamizi Mhe. Jackson Ryoba
Irondo akitoa shukulani kwa uongozi Mahakama Katavi baada ya kupata mafuzo ya
mfumo wa kielektroniki wa e-Mirathi Arhive System (e-MAS)
Muonekano wa ndani wa Mfumo wa e-Mirathi Archieve System (e-MAS)
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania,
Masjala Ndogo ya Katavi, Mhe Godfrey Ntemi Isaya (katikati), Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Katavi Mhe. Silvia Lushasi, (kushoto)
kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Katavi Bw. Epaphras
Tenganamba wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mahakimu pamoja na wataalam wa
Idara ya TEHAMA.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha & James Busanya - Mahakama)
.jpg)
.jpg)

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni