Ijumaa, 23 Juni 2017

VIONGOZI WA MAHAKAMA KUU KANDA YA TABORA WATAKIWA KULINDA MIPAKA YA MAHAKAMA.


Na Magreth Kinabo 

Viongozi wa Mahakama za Mwanzo, Hakimu Mkazi  na  Mahakama  za Wilaya  watakiwa   kuhakikisha kwamba wanailinda  viwanja  vya Mahakama  ya Tanzania  na kuviwezesha   kupata  hati   miliki    ili  kuwezesha  upanuzi  wa  miundombinu ya  Mahakama  ikiwa ni hatua  kuendelea kusogeza huduma za Mahakama kwa wananchi.

Kauli  hiyo ilitolewa na Jaji Kiongozi  Mahakama ya Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand  Wambali alipokuwa akizungumza na  baadhi ya viongozi  wa Mahakama Kuu  Kanda ya Tabora  na  watumishi kwenye ziara ya siku tatu iliyoanza tarehe 19.06 2017 na kumalizika  tarehe 22.06.2017.

Mhe . Jaji  Kiongozi alisema  hayo, katika ziara  hiyo  yenye  lengo  la  kukagua  shughuli za utendaji kazi wa Mahakama sanjari na kuendelea kutoa elimu ya Mpango Mkakati  wa Miaka Mitano (2015/16 hadi 2020) wa Mahakama ya Tanzania, kwa  Viongozi   na watumishi  wa Mahakama,  Mkuu wa Mkoa huo, Aggrey  Mwanry Wakuu wa Wilaya, wakiwemo  wajumbe wa  Kamati  za Ulinzi na Usalama za Mkoa  huo. 

“ Hakikisheni mnaweka  uzio kwenye mipaka ya viwanja vya mahakama na kutafuta hati miliki na kuweka uzio, kwa sababu  viwanja  vina maeneo  makubwa , hivyo rasilimali  muhimu ambazo zitatumika  kupanua miundombinu ya  mahakama  bila vikwazo,” alisema Mhe. Jaji Kiongozi.

Aidha Mhe. Wambali  aliwaomba  watumishi wa Mahakama, ambao wanaofanya kazi katika miundombinu isiyoridhisha kutokata tamaa ya utendaji kazi, bali waendelee kufanya  jitihada hizo ili kuhakikisha malengo ya mpango mkakati huo  wa Mahakama  yanafanikiwa.

Pia  alimtaka kila mtumishi wa Mahakama kuendelea  kufanya kazi kwa bidii, weledi, kuzingatia kanuni za utumishi wa umma na maadili, ukiwemo ubunifu bila kujali nafasi aliyonayo.

Mpango huo, mkakati una  nguzo kuu tatu, ambazo ni Uimarishaji wa Utawala Bora, Uwajibikaji na Usimamizi wa Rasilimali,Upatikanaji wa Haki  kwa Wakati,na Ushirikishwaji wa wananchi na wadau katika shughuli za Mahakama.

Katika  ziara hiyo Mhe. Wambali   alitembelea Mahakama za Mwanzo, Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya  na Mahakama  Kuu,katika Wilaya  za  Igunga, Nzega, Sikonge , Uyui, Kaliua, Tabora na Urambo  ambapo aliridhishwa  kasi usikilizaji wa mashauri kwa sababu hakuna  kesi  za muda mrefu  kuanzia kipindi cha Januari hadi Mei,mwaka 2017.


 Jaji Kiongozi wa Mahakama  Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand  Wambali(katikati)  akiwa katika picha ya pamoja na  baadhi  ya viongozi na  watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora  baada ya kuwasili  Mahakamani  hapo.





Jaji Kiongozi wa Mahakama  Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand  Wambali  akipanda mti wa kumbukumbu huku akishuhudiwa na  baadhi  ya Viongozi  wa Kanda  ya  Mahakama Kuu Tabora na watumishi wa Mahakama. 


    



.
\                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                      

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni