Alhamisi, 22 Februari 2018

MABORESHO YA MIUNDOMBINU: UJENZI WA MAHAKAMA TATU ZA WILAYA WASHIKA KASI MKOANI LINDI



Na Nurdin Ndimbe, Lindi
Katika kutekeleza dhamira yake ya kuboresha huduma za Mahakama na kusogeza huduma hizo karibu zaidi na wananchi, Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imeanza rasmi ujenzi wa majengo matatu ya Mahakama katika mkoa wa Lindi pamoja na wilaya zake za Kilwa na Ruangwa

Ujenzi wa Mahakama hizi ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2015/16 hadi 2019/2020) wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama ambao ulianza kutekelezwa rasmi mwaka 2015. Miradi hii kwa pamoja inalenga kuboresha huduma na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Mahakama imeanza ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mkoa wa Lindi ambalo litajumuisha pia na Mahakama ya wilaya ya Lindi Majengo mengine yanayojengwa ni ya Mahakama za wilaya za Kilwa na Ruangwa. Akizungumza na mwandishi wa habari hii Mtendaji wa Mahakama Mkoani Lindi, Bw. Joseph Chota alisema kuwa miradi yote hii inajengwa na Kampuni ya Moladi Tanzania. ‘’Unajua Mkoa wetu una matatizo makuwa ya Miundombinu ya Mahakama, sehemu nyingi majengo sio ya kwetu aidha tumeazimwa au kupewa na Halmashauri husika  na majengo haya ni ya siku nyingi na chakavu sana’’ alisema Mtendaji huyo. ‘’Kwa hiyo ujio wa miradi mitatu ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kilwa, Ruangwa pamoja na jengo la Mhakama ya Hakimu Mkazi Lindi ni faraja kubwa kwetu  kwa Mahakama pamoja na Mkoa kwa ujumla’’ alisistiza.
    Kwa upande wake Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Moladi Tanzania inayosimamia ujenzi wa majengo hayo Mkoani Lindi Mhandisi Avkado amesema kuwa Mahakama zote tatu zinajengwa na Kampuni ya Moladi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ardhi.
“Kama mnavyoona Mahakama hizi zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi, kwa hapa Kilwa tayari zege la msingi tumemaliza tunasubiri kuanza sasa kusimamisha  ‘pannels’ kwa ajili ya kumwaga kuta za jengo lenyewe” Alisema Mhandisi huyo.
Kuhusu ujenzi wa jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi tuna changamoto ya udongo katika eneo la ujenzi hata hivyo changamoto inashughulikiwa ili kupata ufumbuzi wa haraka ili tuendelee na ujenzi.
“Mafanikio makubwa ya miradi hii iko kwa upande wa mradi wetu Wilayani Ruangwa kwa sasa boma kwa maana ya jengo liko tayari na sasa tumeanza kuunganisha vyuma kwa ajili kuanza kupaua jengo hilo, ukiancha changamoto ndogondogo zinazojitokeza tunajitahidi kuhakikisha kuwa miradi hii inamalizika katika muda uliopangwa,” alisistiza.                                           
 Katika mahojiano maalum na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Ruangwa, Mhe.Ramla Shehagilo yaliyofanyika ofisini kwake Mahakama ya Wilaya Ruangwa anasema kuwa ujenzi wa Mahakama hiyo unaoendelea katika Wilaya hiyo umeleta faraja na ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Wilaya hiyo kwani wamekuwa wakisumbuka kupata huduma katika jengo na mazingira yasiyo ya kuridhisha.
“Kwakweli wananchi wa Wilaya hii  na hata wateja wanaokuja katika Mahakama yetu wanaonekana kufurahia ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ambapo pindi itakapokamilika itawaondolea adha ya kupata haki katika mazingira yasiyo nadhifu, kama unavyoona jengo hili lilikuwa la Mahakama ya Mwanzo Ruangwa, ilipoanzishwa Wilaya, Mahakama ya Wilaya ikaanzishwa kwahiyo tunafanyia kazi katika mazingira magumu na  ya kubanana”  alisema Hakimu huyo wa Wilaya.

 Azma ya Mahakama ya Tanzania ni kusambaza huduma za Mahakama nchi nzima ili hata mwananchi aliyepo katika ngazi ya Kata aweze kupata huduma ya Haki.
Mbali na ujenzi pia kumekuwa na ukarabati wa majengo ya Mahakama ya mara kwa mara zote zikiwa ni jitihada za kuhakikisha kunakuwa na miundombinu ya majengo bora ya kutolea haki kama sehemu ya utekelezaji wa malengo yaliwekwa katika kutekeleza uboreshaji wa Miundombinu na Mpango Mkakati ya Miaka mitano wa Mahakama.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Ruangwa Mhe.Ramla Shehagilo akitoa maelezo ya maendeleo shughuli za Kimahakama pamoja na ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa.
Muonekano wa jengo hilo kwa upande wa mapana upande wa nyuma.
Jengo la Mahakama ya Wilaya Ruangwa likionekana kwa juu likiwa tayari kuanza kupauliwa.
Muonekano wa mbele wa jengo
Mtendaji wa Mahakama Mkoani Lindi Bw Joseph Chota akiangalia msingi kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Hakimu Kazi Lindi.Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi itakapokamilika itaghatimu milioni 642,490,000/-
Mwakilishi wa Kampuni ya Moladi Tanzania Mhandisi Avcado akitoa maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Kilwa mjini Kilwa Masoko.
Msingi uliochimbwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi.



 
 
 
 


 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni