Alhamisi, 1 Februari 2018

RAIS AIPONGEZA MAHAKAMA KWA KUTUMIA TEHAMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuanza kutumia teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika suala zima la utoaji wa haki nchini. 

Akizungumza kwenye kilele cha wiki ya Sheria na siku ya Sheria Nchini, Rais Magufuli amesema Tehama inayo nafasi kubwa katika kurahisisha  mfumo wa utendaji kazi na utoaji wa haki na kuahidi kuusadia Mhimili huo katika vifaa vya Tehama.

Mhe. Rais alisema kwa Mahakama kutumia Tehama katika kazi zake, itasaidia kuongeza kazi ya utendaji pamoja na kupunguza tatizo la rushwa ambalo limekuwa ni kubwa katika Taasisi nyingi za serikali.

Aidha, Kufuatia Tume ya Utumishi wa Mahakama kuwafukuza kazi zaidi ya watumishi  112 wa Mahakama kutokana na makosa mbalimbali ya ukosefu wa maadili na uwajibikaji, Rais amempongeza Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania na kuzitaka Taasisi nyingine kuiga mfano wake.

“ Naipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama ambayo wewe ni Mwenyekiti wake kwa kuwafukuza kazi watumishi 112 wakiwemo Mahakimu 27, asante sana na sijutii kukuteua kuwa Jaji Mkuu, alisema  Mhe. Rais.

Alisema Mahakama inafanya kazi zake vizuri lakini bado wapo watumishi wachache wanaokiuka maadili na hawa hatupaswi kuwaacha  maana wanachelewesha utoaji wa haki kwa wakati.Amevitaka vyombo husika kupanga mkakati wa kutatua tatizo hili.
Naye Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amevitaka vyombo vyote vya dola  kutoa kipaumbele katika Sheria kwa kuwa sheria ni msingi wa amani na amani ni maendeleo.  

Alisema kwa kulitambua hilo, Mahakama ya Tanzania katika wiki ya sheria  imetoa elimu ya sheria na taratibu za sheria kwa wananchi mbalimbali  na imejiwekea malengo ya kuongeza uwazi na ufanisi katika masuala utawala na uendeshaji wa mashauri na Tehama ndio jibu sahihi la karne ya 21.

Jaji Mkuu alisema Mahakama imedhamiria kuondokana na tatizo la rushwa na imeazimia na haitaki kubaki nyuma na kasi ya mabadiliko ya kunufaika na manufaa makubwa ya Tehama.

Aliongeza kuwa  Mahakama ya Tanzania imelenga kunufaika na Tehama  kwenye eneo la usimamizi wa fedha, ukusanyaji wa takwimu, ukusanyaji wa mapatona usikilizaji wa mashauri.

Siku ya Sheria nchini huadhimishwa kila mwaka  na ilianza kuadhimishwa nchini mwaka 1996.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika viwanja vya Chimala jijini Dar es salaam 
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia kwenye sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika viwanja vya Chimala jijini Dar es salaam. 
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Majaji Wastaafu kwenye sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika viwanja vya Chimala jijini Dar es salaam. 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Viongozi wa Dini. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni