Jumatano, 7 Novemba 2018

MAHAKAMA KUU MOSHI YAMUAGA KITAALUMA MHE. JAJI AISHIEL SUMARI BAADA YA KUSTAAFU RASMI


Na Paul Mushi, Mahakama Kuu-Moshi

Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi imemuaga rasmi Kitaaluma aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu katika Kanda hiyo, Mhe. Jaji Mstaafu Aishiel Sumari.

Sherehe za kumuaga kitaaluma zilizohudhuriwa na Wahe. Majaji na Watumishi wa Kanda hiyo pamoja na Wawakilishi kutoka Ofisi ya Mwanasheria wa Mkoa na Mawakili zilifanyika Novemba 06,  katika eneo la Mahakama Kuu Kanda ya Moshi ikiwa ni hitimisho la safari yake katika Utumishi wa Umma.

Katika hotuba yake Mhe. Jaji Mstaafu Sumari aliwashukuru Viongozi wa Mahakama ya Tanzania na Watumishi wote wa Mahakama kwa ujumla kwa kushirikiana nae katika kipindi chote cha utumishi wake.

“Kwa namna ya pekee napenda kuwashukuru pia watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza niliofanya nao kazi kuanzia 2006 hadi Dec 2014 na Mahakama Kuu Kanda ya Moshi January 2015 hadi Nov 2018,” alisema Mhe. Jaji Mstaafu Sumari.

Katika Utumishi wa Umma, Mhe. Jaji Mstaafu Sumari aliwahi kushika nafasi mbalimbali mfano katika Ofisi ya Mwanasheria kuanzia mwaka 1984 hadi 2003 kama Mwanasheria wa Serikali.

Mwaka 2003 alichaguliwa kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Makosa ya Jinai, Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Mwaka 2006,  Rais Mstaafu wa Serikali wa awamu wa nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alimteua Mhe. Aishiel Sumari kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Mhe. Jaji Mstaafu Sumari amelitumikia Taifa kwa muda wa miaka 34 hadi kufikia leo tarehe 06/11/2018 alipohitimisha safari ya Utumishi wa Umma.

Kwa Mujibu wa taratibu za Kimahakama Jaji anapostaafu hustaafishwa kwa kufanyika shauri maalumu ambalo ndilo hasa huitimisha zoezi zima la kustaafu kwa mujibu wa sheria.

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi, ambaye pia alikuwa Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Aishiel Sumari (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu na Mawakili walioshiriki katika hafla ya kumuaga kitaaluma iliyofanyika Novemba 06, 2018.

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi, Mhe. Aishiel Sumari (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi na Arusha, Majaji Wastaafu pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi.
 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni