Jumapili, 25 Aprili 2021

MAHAKIMU WAKAZI SINGIDA WAPIGWA MSASA

Na Mwandishi wetu, Mahakama-Singida

Mahakimu Wakazi wa Mahakama ya Mkoa wa Singida wametakiwa kutumia muda mwingi kujifunza vitu vipya ili kuongeza ujuzi katika kazi yao ya utoaji haki kwa wananchi.

Akizungumza wakati akifungua rasmi kikao kazi kilichojumuisha Mahakimu wapatao 40 wa Mkoa huo, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Jaji George Masaju alisema kuwa mafunzo na uzingatiaji wa weledi katika kufanya kazi ni vitu muhimu katika kuboresha huduma ya utoaji haki.

Mhe. Jaji Masaju ambaye alifungua Mafunzo hayo kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma aliwaambia Mahakimu hao kuwa mada za kikao kazi hicho zitumike kuboresha huduma kwa wananchi.

Katika kikao hicho Mahakimu hao walipatiwa mada mbalimbali ikiwa ni Pamoja na uendeshaji wa mashauri ya uhujumu uchumi, upokeaji, utunzaji na uondoshaji wa vielelezo, uendeshaji na usimamiaji wa mashauri ya mirathi kwa Mahakama za Mwanzo na Wilaya, Makosa yanayojirudia katika uendeshaji wa mashauri ya unyanyasaji wa kijinsia.

Mada nyingine ni uendeshaji wa mashauri ya ndoa na talaka, uendeshaji wa mashauri ya madai kwa Mahakama za Mwanzo, maadili ya Mahakimu na utekelezaji wa hukumu kwa Mahakama za Mwanzo na Wilaya.

Aidha, katika kipindi cha kikao hicho cha siku tatu kilichofanyika kuanzia Aprili 22 hadi Aprili 24, 2021, ilifanyika pia semina ya Mahakimu Wafawidhi wa Wilaya za mkoa wa Singida juu ya uongozi, ukaguzi, usimamizi na mahusiano.

Kikao kazi hiki kiliandaliwa na Ofisi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkowa Singida kwa kushirikiana na Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) tawi la Singida, ambapo pia tawi hilo lilifanya kikao chao cha robo mwaka.

Sehemu ya Mahakimu Wakazi wa Mahakama mkoani Singida wakimsikiliza mgeni rasmi (hayupo pichani) alipokuwa akifungua rasmi kikao kazi kwa ajili ya Mahakimu hao.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Jaji George Masaju akifungua kikao hicho kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Mustapher Siyani.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Elimo Massawe akizungumza jambo na washiriki (hawapo pichani) wakati wa kikao hicho.

Baadhi ya Wahe. Mahakimu waliohudhuria katika kikao hicho wakifuatilia kwa umakini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni