Ijumaa, 10 Septemba 2021

RAIS WA MAHAKAMA YA HAKI YA AFRIKA MASHARIKI AMTEMBELEA JAJI MKUU

Na Innocent Kansha – Mahakama.

Jaji Mkuu wa Tanzania ameahaidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki na kuwapongeza Wakuu wa nchi wanachama kwa kuwaamini Viongozi hao kusimamia majukumu ya Mahakama hiyo, kwani haki ni msingi wa amani pasipo haki hakuna utangamano.

Akizungumza na viongozi hao walioongozwa na Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki waliomtembelea Ofisini kwake Jijini Dar es salaam mapema leo Septemba 10,2021, Jaji Mkuu Prof. Juma alisema Mahakama ya Tanzania inaongozwa na Mpango Mkakati wake, wenye nguzo kuu tatu ambazo ni Utawala bora, uwajibikaji na Usimamizi wa Rasilimali, Upatikanaji na utoaji haki kwa wakati na Kuimarisha Imani ya wananchi na Ushirikishwaji wa wadau.

“Kwa sababu tunaamini kwamba ukiwa na utawala bora, uwajibikaji, matumizi mazuri ya rasilimali watu na fedha kwa kutumia viwango hivi utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutoa haki kwa wote na kwa wakati, kwani haki ni msingi wa amani bila haki hakuna utangamano”, alieleza Jaji Mkuu.

Prof. Juma alisema kwa upande wa nguzo zinazoijenga Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki kama vile mtangamano wa kisiasa, ushuru wa forodha, soko huru na sarafu ya pamoja kwa nchi wananchama wa Jumuiya ya Afrika Masharika bila shaka hakukosekani usuluhishi wa migogoro mara nyingi nchi hizi hazitumii vizuri chombo hiki kutatua migogoro yao.

Jaji Mkuu akaongeza kuwa changamoto ya kuhakikisha wananchi wanapata haki ya kweli bado ni kubwa ukiangalia jiografia ya nchi hii utaona kuna maeneo mengi ya vijijini mwananchi anatembea mwendo mferu kuifuata haki, wengi hawafahamu sheria na taratibu na miundo mbinu mingine sio rafiki kama umeme, barabara na miundombinu ya majengo hususani ya Mahakama kwa kushirikiana na Mahakama yenu haki inaweza kufikiwa kwa haraka zaidi.

Naye, Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mahariki Jaji Nestar Kayobela alisema anamshukuru Jaji Mkuu kwa niaba ya uongozi wa Mahakama ya Tanzania, ujumbe wake ni kuendeleza mazuri ya mtangulizi wake kwa kipindi chake cha miaka saba ijayo ya uongozi kwa kuzingatia mambo makuu matatu.

Akielezea mambo hayo makuu matatu ambayo ndiyo dira ya uongozi wake kwa kipindi cha miaka saba ni falsafa ya kufanya kazi kwa kushirikiana (team work), jambo lingine ni kuongoza kwa nia njema (good faith) pamoja na shughuli za kimahakama kuendeshwa kidiplomasia (Judicial Diplomacy).

Jaji Kayobela akaongeza kuwa wamefufua mashirikiano na kuendesha mikutano ya Majaji Wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya inayounda Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki na Majaji hao walikutana mjini Kigali mwezi mei 2021 na kuazimia mkutano mwingine utafanyika mwezi Disemba 2021 Jijini Nairobi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu ya kuwafunza Majaji na Mahakimu wa nchi wanachama wa Jumuiya kwa kuanzia Mahakama imetoa mafunzo Jijini Bujumbura kwa wadau hao wapatao 420 na hatua inayofuata mafunzo yanarajiwa kufanyika South Sudani na hatimaye kuzunguka Jumuiya nzima.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ameuhakikishia ujumbe huo kuupa ushirikiano wa asilimia mia moja na kuwaambia Mahakama imepiga hatua kubwa sana katika maboresho mbalimbali ya kuhakikisha mwananchi anapata haki kwa wakati mathalani matumizi ya TEHAMA, maboresho ya miundombinu ya majengo kwa kujenga mapya na kukarabati mengine kuanzia ngazi ya Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama Kuu.

Maboresho mengine aliyoyaeleza Mtendaji Mkuu huyo ni Matumizi ya Ofisi mtandao (E- Office), matumizi ya aplikasheni utoaji mrejesho wa huduma za Mahakama kwa mteja (Online Feedback Application), matumizi ya kusajili mashauri kwa njia ya mtandao (E- Failing), utunzaji wa amri na hukumu za Mahakama Kuu na rufani kwa njia ya mtandao (Tanzilii) na kusajili na kuhuisha masahuri kwa njia ya mtandao (JSDS II) na usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya mtandao maarufu (Video Conference).

 

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa kwenye picha ya viongozi wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki amehaidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki na kuwapongeza Wakuu wa nchi wanachama kwa kuwaamini Viongozi hao kusimamia majukumu ya Mahakama hiyo, wengine ni Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Masahariki Jaji Nestar Kayobela (wa pili kushoto), Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki Mhe. Yohane Masala (wa pili kulia), Jaji wa Divisheni ya Rufani ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki Mhe. Sauda Mjasiri (wa kwanza kushoto) na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki Mhe. Yufnalis Okubo (wa kwanza kulia)
   
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma (aliyesimama) akitoa neno la utambulisho wakati wa ziara ya vionzgozi  wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki walipomtembelea Jaji Mkuu Ofisini kwake


Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akimulekeza na kumuonyesha vitabu mbalimbali vilivyoandaliwa na Mahakama ikiwemo Mpango Mkakati mpya wa miaka mitano unaoanzia 2020/21 - 2024/25 na ulioisha muda wake,  Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki Jaji Nestar Kayobela (kulia) kabla ya kumkabidhi zawadi hizo za vitabu.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyesimama) ameuhakikishia ujumbe huo kuupa ushirikiano wa asilimia mia moja ili kutimiza adhima ya kutoa na kutenda haki kwa wanachi wa jumuiya wanachama wanahudumiwa na Mahakama hiyo.



Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa tatu kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki mara walipo mtemebelea Ofisini kwake Jijini Dar es salaam Septemba 10,2021. Wengine ni Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Masahariki Jaji Nestar Kayobela (wa tatu kushoto), Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki Mhe. Yohane Masala (wa pili kushoto), Jaji wa Divisheni ya Rufani ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki Mhe. Sauda Mjasiri (wa kwanza kushoto), Msajili Mkuu wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki Mhe. Yufnalis Okubo (wa pili kulia) na Msaidizi wa msajili masijala ndogo ya Dar es salaam Bw. Mennas Mafwere (wa kwanza kulia).

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa tatu kulia) akiwa ameshikana mikono kwenye picha ya pamoja na Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Masahariki Jaji Nestar Kayobela (wa tatu kushoto) mara walipo mtemebelea Ofisini kwake Jijini Dar es salaam Septemba 10,2021. Wengine ni Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki Mhe. Yohane Masala (wa pili kushoto), Jaji wa Divisheni ya Rufani ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki Mhe. Sauda Mjasiri (wa kwanza kushoto), Msajili Mkuu wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki Mhe. Yufnalis Okubo (wa pili kulia) na Msaidizi wa msajili masijala ndogo ya Dar es salaam Bw. Mennas Mafwere (wa kwanza kulia).

(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni