Na Faustine Kapama, Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 22 Novemba, 2021 amezindua
Vitabu vya Mkusanyiko wa Maamuzi ya Mashauri ya Kazi (Labour Court Case Digest)
ambapo amehimiza kasi ya usikilizaji wa mashauri na utatuzi wa migogoro ya kazi
inayoletwa mahakamani ili kusaidia kuchochea ukuaji wa uchumi hapa nchini.
Akizungumza
katika hafla ya uzinduzi wa Vitabu hivyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Jaji Mkuu alisema kuwa hakuna ubishi kwamba
maendeleo ya mtu mmoja mmoja na kukua kwa uchumi wa nchi kwa ujumla kunategemea upatikanaji wa haki ambayo huchagizwa na umalizaji wa haraka wa migogoro
inayowasilishwa Mahakamani.
Alibainisha
kuwa sekta ya kazi ni moja ya sekta muhimu katika ukuaji wa uchumu, hivyo
kwa upekee, umalizaji wa haraka wa mashauri ya kazi yaliyopo katika ngazi mbali
mbali za vyombo vya utatuzi wa migogoro ya kazi na utoaji haki ni moja ya nguzo
muhimu katika ukuaji wa uchumi.
“Ndio
maana mnamo mwaka 2018, tulifanya Ugatuzi wa Mamlaka na kuwapa mamlaka Majaji
waliopo katika Kanda za Mahakama Kuu kuweza pia kusikiliza mashauri ya kazi.
Hii imesaidia umalizikaji wa haraka wa mashauri ya kazi sehemu zote ambazo kuna
Kanda ya Mahakama Kuu,” Jaji Mkuu alisema.
Mhe.
Prof. Juma amesema pia kuwa ili migogoro ya kazi iweze kutatuliwa kwa haraka na
kwa wakati, ni sharti Mahakama itoe tafsiri ya sheria za kazi kupitia maamuzi
mbalimbali ili kumuwezesha mtatuzi wa migogoro kufanya maamuzi ya haki na kwa
wakati.
“Vitabu hivi vitawezesha Mahakama na vyombo
vingine vya kutoa haki katika sekta ya kazi pamoja na wadau wake kufanya
urahisi wa rejea wakati wa usikilizaji na utoaji maamuzi wa mashauri ya kazi.
Si hivyo tu lakini pia vitabu hivi vitasaidia Waajiri na Wafanyakazi kujua
zaidi mambo muhimu yaliyomo kwenye sheria za kazi kwa kuwa sheria hizo
zimetafsiriwa katika vitabu hivi,” alisema.
Jaji
Mkuu amesema kuwa Mkusanyiko wa vitabu hivyo utatasaidia kupunguza migogoro
katika sehemu za kaz na kuchochea kuongeza ufanisi katika utendaji kazi kwa
kila mmoja kujua haki na wajibu alionao itakayopelekea kukua kwa uchumi.
“Kwetu
sisi Mahakama na vyombo vya Usuluhishi na Uamuzi, vitabu hivi vitasaidia
kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri na hivyo itawezesha wananchi kupunguza
muda watakaotumia katika kudai haki kwenye vyombo hivi na badala yake kutumia
muda mwingi katika uzalishaji mali,” alisema.
Kwa
upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma
Maghimbi alisema kuwa kwa mujibu wa kanuni ya 3(1)(a) ya Kanuni za
Mahakama ya kazi, Mahakama hiyo
inajukumu la kuweka kumbukumbu za maamuzi inayokuwa imeyatoa katika kutekeleza
mamlaka yake, hivyo utekelezaji wa jukumu hilo ndilo chimbuko la kuwa na vitabu
hivyo vya ripoti ya maamuzi ya Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi.
Akifafanua
zaidi, Mhe. Maghimbi alisema kuwa “Labour Court Case Digest” ni vitabu
vinanyokusanya maamuzi mbalimbali yanayohusiana na ajira na mahusiano kazini,
yaliyoamuliwa na Majaji wa Divisheni ya kazi na mashauri hayo hukusanywa kwa
umahiri ili kujumuisha maamuzi yanayogusa masuala tofauti na yenye kutoa
tafasiri na misimamo ya Sheria za kazi, Kanuni zilizopo pamoja na Mikataba ya
Kimataifa inayohusiana na masuala ya kazi.
“Ukusanyaji
huu hufanywa na watalaamu waliobobea katika Sheria na uwezo wa kufanya
uchambuzi wa mashauri, kuyakusanya na kuyaripoti kwa namna ambayo itamnufaisha
mlengwa,” alisema. Aidha, alibainisha hhumuni la uzinduzi wa vitabu hivyo ni kuongeza
wigo wa ufahamu kwa wadau wote wa sekta ya kazi pamoja na jamii kwa ujumla, juu ya uwepo wa vitabu
hivyo ambayo ni miongozo ya sheria katika kushughulikia na kutatua masuala
mbalimbali katika sekta ya kazi ikiwemo migogoro inayotokana na mahusiano
kazini.
Hafla
ya uzinduzi wa Mkusanyiko wa Vitabu hivyo inayojumuisha maamuzi ya Mahakama
Kuu, Divisheni ya Kazi kwa mwaka 2016, 2017 na 2018 imehudhuriwa na maafisa
mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania, akiwemo Kaimu Jaji Kiongozi, Mhe. John Mgetta na Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke, maalumu kwa mashauri yanayohudu ndoa na talaka, Mhe. Ilvin Mugeta.
Wageni
wengine walikuwa Mkuu wa Shule ya Sheria, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe.
Dkt. Benhajj Masoud, Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia
Kazi (ILO-Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi), Bw. Wellington Chibebe,
Majaji mbalimbali wa Mahakama Kuu ya Tanzania na wadau mbalimbali wa Mahakama.
Uzinduzi
wa Vitabu hivyo unaweka historia nyingine ya kutoa toleo la tatu la ‘Labour
Court Case Digest’ ikijumuisha maamuzi muhimu ya Divisheni ya kazi kwa miaka ya
2016, 2017 na 2018 kwa kukusanya na kuyaweka pamoja katika vitabu vya sheria
vyenye maamuzi mbalimbali yenye kutafasiri na kuweka misimamo ya kisheria
kwenye sekta nzima ya kazi.
Hii
ni mara ya tatu machapisho kama hayo yameweza kutolewa na Mahakama Kuu
Divisheni ya Kazi kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO). Chapisho
la kwanza lilihusisha “Labour Court Case Digest” za mwaka 2011 na 2012.
Chapisho la pili lilikuwa la mwaka 2013, 2014 na 2015.
Kutokana
na hatua hiyo, Jaji Mkuu aliishukuru ILO kwa kuendelea kutoa ufadhili kwa Mahakama
ya Tanzania kuwezesha na kufanikisha matoleo yote hayo matatu ya Labour Court
Case Digest. Amesema kuwa ILO wamekuwa wadau wakubwa wa utoaji haki katika
mashauri ya kazi na wamekuwa wanasaidia Divisheni ya Kazi katika mambo
mbalimbali ikiwemo mafunzo kwa Majaji.
Kabla ya uzinduzi huo, Jaji Mkuu alipokea neno fupi
kutoka kwa wawakilishi mbalimbali, akiwemo Bw. Willington Chibebe (ILO), Naibu Wakili
Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende, Bw. Frank Mwalongo kutoka Chama cha Wanasheria
wa Tanganyika (TLS), Bi Suzzane Ndomba kutoka Chama cha Waajili (ATE), Bw. Noel Nchimbi kutoka Chama cha Wafanyakazi
(TUCTA) na Bw. Sammy Katerega ambaye anatoka Wawakilishi binafsi.
Kwa
ujumla wao, wawakilishi hao waliiipongeza Mahakama ya Tanzania, kupitia
Divisheni ya Kazi kwa kazi nzuri inayofanya ya kutatua migogoro mbambali ya
wananchi, lakini wakaomba utafutwe utaratibu utakaowezesha majaji wanaohudumu
katika mahakama hiyo kukaa muda mrefu ili kuwa na uelewa mpana wa sheria za
kazi na pia maamuzi yanayotolewa yawe kwa lugha ya Kiswahili.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akizindua Vitabu vya Mkusanyiko wa Maamuzi ya Mashauri ya Kazi leo tarehe 22 Novemba, 2021 jijini Dar es Salaam. Kushoto kwa Jaji Mkuu ni Kaimu Jaji Kiongozi, Mhe. John Mgetta na Mkuu wa Shule ya Sheria, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Benhajj Masoud na kulia kwake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Kazi (ILO-Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi), Bw. Wellington Chibebe.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Vitabu vya Mkusanyiko wa Maamuzi ya Mashauri ya Kazi leo tarehe 22 Novemba, 2021 jijini Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akifuatilia jambo katika hafla ya uzinduzi wa Vitabu vya Mkusanyiko wa Maamuzi ya Mashauri ya Kazi leo tarehe 22 Novemba, 2021 jijini Dar es Salaam. Kushoto kwa Jaji Mkuu ni Kaimu Jaji Kiongozi, Mhe. John Mgetta na Mkuu wa Shule ya Sheria, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Benhajj Masoud na kulia kwake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Kazi (ILO-Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi), Bw. Wellington Chibebe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni