Na Faustine Kapama – Mahakama, Lushoto
Mafunzo ya siku tano
yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kuwaleta pamoja
Makatibu Mahsusi 56 kutoka Mahakama mbalimbali nchini yameingia siku ya pili
leo tarehe 10 Agosti, 2022 huku washiriki hao wakitakiwa kuwa na ‘vifua’ ili waweze
kutekeleza majukumu yao kikamilifu katika mnyororo mzima wa utoaji haki kwa
wananchi.
Akiwasilisha mada kuhusu ‘Ijue
Mahakama Yako’ na “Tamaduni za Mahakama,’ Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro Mhe. Japhet Manyama amewaambia washiriki wa
mafunzo hayo kuwa wao ni nguzo muhimu ya ofisi ya Mahakama kwa vile hakuna
wasichokijua kinachofanywa na viongozi wao katika maeneo yao ya kazi.
“Nyinyi ndiyo mhimili wa
Mahakama, watumishi wengine kama afisa utumishi, karani, mtendaji au mlinzi
hawakai na viongozi wao katika ofisi moja. Mnatakiwa kutunza siri za viongozi wen
una kutunza siri za ofisi. Najua kila mtu ana mapungufu yake, msiwe wepesi wa
kuanika kila kitu kinachofanyika kwa mabosi wenu na ofisi mnazozihudumia kwa
ujumla,” amesema.
Mwezeshaji huyo amesema
kazi kubwa ya Mahakama ni kutoa haki kwa wananchi kwa wakati, hivyo kila mmoja
wao anapaswa kutekeleza majukumu yake pale alipopangiwa, ikiwemo katika ngazi
ya Ukatibu Mahsusi. “Nyinyi ni watu wakubwa sana mahakamani, ila hamjui tu. Ulishawahi
kukuta ofisi ipi ina Makatibu Muhtasi wanne? Ulishawahi kujiuliza kwa nini upo
peke yako?” alihoji.
Akawapitisha kwa ufupi kwenye
dira na dhamira ya Mahakama ya Tanzania na kusisitiza kila mmoja kufanya kazi
kwa bidii kwa kuzingatia maadili. Amewahimiza kujiepusha na vitendo vyote hasi,
ikiwemo matumizi ya lugha mbaya kwa wananchi, jambo ambalo halikubaliki hata kidogo
katika Mahakama ya sasa.
“Mahakama ya bora liende
imeshapita, lazima tubadilike kwenda sambamba na mabadiliko na uboreshaji wa miundombinu
unaoendelea kwa sasa,” amesema na kuwakumbusha pia kuwa kwa sasa Mahakama
inachagiza matumizi teknolojia ya kisasa kwenye kila huduma ya kimahakama, hivyo
wanapaswa kwenda na kasi hiyo ya mabadiliko.
Awali, akiwasilisha mada
kuhusu ‘Utunzaji wa Majalada ya Watumishi na Mawasiliano ya Siri za Serikali’, Mkufunzi
Msaidizi Masomo ya Uhazili kutoka Utumishi, Bi Juliana Mwalusamba amesema kuwa
kila mtumishi katika sehemu ya kazi ana wajibu wa kutunza siri za Serikali kwa
mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi, kwani kwa kufanya hivyo
kutaiwezesha Serikali kufanya kazi zake kwa utulivu na pia kulinda usalama wa
Taifa.
“Katibu Mahsusi ni mmoja
wa watumishi wanaoshiriki kazi nyingi zinazohusisha matumizi ya majalada ya
watumishi. Ni wajibu wako kuhakikisha kuwa taarifa za watumishi
zinashughulikiwa kwa usiri mkubwa hata kama hazijawekwa kwenye jalada la siri. Ni
marufuku kabisa kwa mtumishi kushika au kuangalia kwa namna yoyote jalada lake
binafsi au taarifa zilizo ndani ya jalada lake,” amesema.
Akawakumbusha washiriki
hao wa mafunzo kuwa wakati wa kutekeleza majukumu katika osisi za umma kila
mtumishi anapaswa kutunza siri za Serikali katika kutekeleza takwa la sharia na
kanuni mbalimbali, kulinda amani na utulivu sehemu ya kazi au jamii, kuepuka mipango
pingamizi, kulinda faragha za watu, kulinda usalama wa Taifa na kuepuka udhalilishaji.
“Watumishi wa umma na
wananchi wote tunapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi katika
kulinda siri za Serikali ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kutokana na kuvuja
kwa taarifa hizo,” amesema.
Mada nyingine iliwasilishwa
na Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji na Tathmini, Bw. Sebastian Lacha ambayo ilihusu
‘uelewa wa mpango mkakati wa Mahakama kwa ajili ya utekelezaji mzuri wa
shughuli za kila siku’ iliyowasilishwa.
Zingine ni ‘utawala, muundo
na maendeleo ya mifumo; maendeleo ya ujuzi, ukaguzi na usimamizi wa utendaji;
upatikanaji wa haki na uadilifu wa umma’ iliyowasilishwa na Naibu Msajili
kutoka Kitengo cha Uboreshaji cha Mahakama, Mhe. Sekela Mwaiseje na ‘matumizi
ya TEHAMA katika shughuli za kimahakama’ iliyowasilishwa na Afisa TEHAMA Mwandamizi,
Bw. Allan Machela.
Sehemu nyingine ya Makatibu Mahsusi 56 (picha tatu za chini) wanaoshiriki kwenye mafunzo yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro Mhe. Japhet Manyama (kulia) akiwa katika ukumbi wa mafunzo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni