·Yatangaza rasmi kushiriki mashindano SHIMIWI
·Yajichimbia kujifua kwenye michezo nane
Na
Faustine Kapama-Mahakama
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) leo tarehe 24 Septemba, 2022 imefanya Mkutano Mkuu
wa mwaka kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji, ikiwemo kushiriki kikamilifu
kwenye mashindano yajao ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali
(SHIMIWI) yanayotarajia kufanyika jijini Tanga kuanzia tarehe 1 Octoba, 2022.
Akizungumza katika
Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi namba moja katika Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Mahakama Sports, Wilson Dede amewahimiza wanamichezo
wote kujiandaa kikamilifu ili kupata ushindi wa kishindo kwenye michezo yote nane
watakayoshiriki kwenye mashindano ya SHIMIWI mwaka huu. Ameitaja michezo hiyo
kuwa ni Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata,
Tufe, Riadha Wanaume na Wanawake pamoja na Baiskeli.
“Mwaka jana kwenye
mashindano haya tulishiriki kwenye michezo kadhaa na kufanikiwa kushika nafasi
ya kwanza na kupata makombe mawili kwenye Kamba Wanaume na Kamba Wanawake.
Mwaka huu tunataka ushindi na makombe kwenye michezo yote tunayoshiriki, uwezo
wa kufanya hivyo tunao na upo mikononi mwetu,” aliwaambia wajumbe wa Mkutano
huo.
Mwenyekiti Dede aliwasihi
wanamichezo wenzake kuendeleza ushirikiano walionao na kudumisha nidhamu ya
mchezo tangu wakiwa kwenye mazoezi, kambini na kwenye uwanja wa mashindano, kwani
kwa kufanya hivyo nuru ya mafanikio itaweza kuwaangaza na hatimaye kutimiza
matarajio ya Mwajiri, yaani, Mahakama ya Tanzania.
“Mwajiri wetu ana
matarajio makubwa sana kutoka kwetu na ndiyo maana ametupa kibali cha
kushiriki. Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel
hataki tuishie kwenye mashindano ya SHIMIWI pekee, anataka twende mbali zaidi
ya hapa. Azma yake ni kushiriki kwenye Ligi Kuu kwenye michezo yote. Kwa hiyo,
ili tuweze kufikia matarajio haya hatuna budi kushikamana, kupendana na kuzingatia
nidhamu wakati wote,” alisema.
Mwenyekiti huyo aliwatakia
wanamichezo wote afya njema na maandalizi mema ya mazoezi na kuwasihi
kuzingatia programmu zinazotolewa na walimu ili waweze kujiandaa vyema kushiriki
kikamilifu kwenye mashindano hayo. Amewatangazia kuwa Timu ya Mahakama Sports itaondoka
kuelekea Tanga kushiriki mashindano ya SHIMIWI muda wowote mara baada ya taratibu
za kiutawala kukamilika.
Akizungumza kwa kifupi kwenye
Mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Mahakama Sports Theodosia Mwangoka amewashukuru
wanamichezo wenzake kwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu kwenye
Mkutano huo na kuwaomba kuzingatia maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi. Amewasihi
kutunza siri za kambi na masuala mengine nyeti ambayo hayafai kujadiliwa nje ya
Mkutano.
Mbali na Mwenyekiti na
Naibu Katibu Mkuu, viongozi wengine waliohudhuria Mkutano huo ni Wajumbe watatu
wa Kamati Tendaji Mchawi Mwanamsolo, Judith Mwakyalabwe na Rhoida Makassy, Mjumbe
Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole, Afisa Michezo kutoka Utawala Nkuruma
Katagira, Meneja wa Timu Antony Mfaume na Mhasibu Rajabu Diwa. Makamu
Mwenyekiti Fidelis Choka na Katibu Mkuu Robert Tende hawakuweza kuhudhuria
Mkutano huo kwa vile walikuwa na Mkutano mwingine uliokuwa unafanyika jijini
Dodoma.
Afisa Michezo kutoka Utawala Nkuruma Katagira akijibu baadhi ya hoja za kiutawala zilizoibuliwa kwenye Mkutano huo. Kulia ni Meneja wa Timu Antony Mfaume na kushoto ni Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole.
Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Mahakama Sports Mchawi Mwanamsolo akeleza uzoefu wake katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza wakati wakiwa kambini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni