Na Evelina Odemba-Morogoro
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani hapa limeendesha
mafunzo ya kukabiliana na majanga ya moto kwa watumishi wa Mahakama katika Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro ili kuweza kujiokoa wao wenye pamoja na mali
zingine.
Mafunzo hayo yalioandaliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe yalishirikisha wadau
wengine wa Mahakama, ikiwemo jeshi la Polisi, Magereza, Mawakili wa Kujitegeme
na Makampuni ya Usafi na Ulinzi yanayohudumu katika Kituo hicho.
Akifungua mafunzo hayo yalitofanyika hivi karibuni, Mhe
Ngwembe alisema wanataka kuhakikisha watumishi wote wa Mahakama na watendaji
wengine wanakuwa na uelewa wa kuweza kujikoa. Alisema Serikali imetumia fedha
nyingi katika ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki, hivyo ni jukumu lao
kuhakikisha wanavitunza na kuvilinda na majanga ya moto.
Naye Mkaguzi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Emmanuel
Ocheng, ambaye alimwakilisha Kamanda wa Jeshi hilo mkoani Morogoro aliupongeza
uongozi wa Mahakama kwa kuja na wazo hilo la kutoa mafunzo hayo kwa watendaji
wake.
Sanjari na hilo, Mkaguzi Ocheng alisema jengo hilo la Kituo
Jumuishi limekuwa mfano wa kuigwa kwa majengo yote ndani ya mkoa wa Morogoro
kutokana na kuwa miundombinu yote muhimu ya kupambana na moto. Alisema Jeshi
hilo litaendelea kushirikiana na Mahakama hiyo katika kutoa elimu ya uzimaji
moto kwa wananchi kutokana na nafasi watakayopatiwa.
Ameishauri jamii kupitisha michoro ya nyumba zao kwa
jeshi hilo kabla ya kuanza ujenzi ili kusaidia kuweka sahihi miundombinu ya
uzimaji moto ili kujiepusha na majanga hayo. Mkaguzi Ocheng alitumia fursa hiyo
kuwaomba watendaji wa Kituo Jumuishi kukagua mara kwa mara vifaa vyao vya
kuzimia moto katika magari yao.
Mafunzo hayo ya siku moja yametoa fursa kwa watumishi
wa Mahakama na watendaji wengine kujifunza aina za moto, vifaa vya kuzimia na
jinsi ya kuvitumia. Watendaji hao walionyesha kuridhika na kufurahia elimu hiyo
tofauti na hapo awali walivyokuwa wakielewa suala hilo.
Mtumishi wa Mahakama, Bi. Shany Kapinga akifanya kwa vitendo zoezi la uzimaji moto. Pembeni ni watumishi pamoja na wadau wakishuhudia namna moto unavyozimwa.
Mwonekano wa mbele wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni