Na Arapha Rusheke-Mahakama Kuu, Dodoma
Tume ya Kurekebisha Sheria na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali wamesaini makubaliano na Taasisi ya Habari za Kisheria Afrika, the African Legal Information Insitute (AfricanLII), kuhusu
ushirikiano kwenye masuala ya upatikanaji kwa urahisi wa nyaraka za kisheria
kwa njia ya kidijitali, ikiwemo maamuzi ya Mahakama na Sheria mbalimbali.
Katibu wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Bw. Grifin
Mwakapeje na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa ndiyo
waliotia saini makubaliano hayo kwa upande wa taasisi za Tanzania, huku Mwakilishi AfricanLii, Bw. Greg Kempe akisaini kwa niaba ya taasisi yake. Katika hafla hiyo, Mahakama
ilishiriki kama mdau na mzoefu katika eneo hilo.
Hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo ilifanyika
hivi karibuni jijini hapa siku ya kwanza ya warsha ya siku mbili kuhusu utoaji
na upatikanaji endelevu wa sheria kwa njia ya kidijitali. Warsha hiyo ilifunguliwa
na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damasi Ndumbaro.
Akizungumza wakati anafungua warsha baada tukio hilo, Mhe.
Dkt. Ndumbaro alisema utiaji saini wa makubaliano hayo utahakikisha sheria zote
za Tanzania zinazotungwa na Bunge na sheria ndogo zinapatikana kwenye mifumo ya
kidijitali.
“Mradi huu pia utasaidia wananchi na taasisi za Serikali
ambazo zinatumia Sheria mbalimbali kuweza kuzipata kiurahisi, tunatumia
mapinduzi ya teknolojia kuhakikisha tunapeleka haki kirahisi na kwa wepesi kwa
kila Mtanzania,” alisema Waziri wa Sheria na Katiba.
Warsha hiyo ya siku mbili iliandaliwa na GIZ, AfricanLii na
Laws Africa na washiriki wake ni Mahakama ya Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Seriali Tume ya Kurekebisha Sheria, Chama cha Wanasheria wa Tanganyika
(TLS), Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali na Wizara ya Katiba na Sheria.
AfricanLII na Laws Africa zimekuwa zikisaidia upatikanaji wa
maamuzi na Sheria nchini Tanzania kupitia Mfumo wa Taarifa za Maamuzi na Sheria
wa TanzLII (www.tanzlii.org)
tangu 2018.
Mfumo huo wa TanzLII umesaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji
wa maamuzi na Sheria na kuwa ni mfano wa mifumo bora ya kisheria barani Afrika
na Duniani. AfricanLII na Laws Africa wamependekeza ushirikiano wa taasisi
mbalimbali katika kutunza Sheria na maamuzi ya Mahakama katika mfumo huo kwa
pamoja.
Katibu wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Bw. Grifin
Mwakapeje (kulia) na Mwakilishi AfricanLii, Bw. Greg
Kempe wakisaini mkataba huo.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristi Longopa (kulia)
na Mwakilishi AfricanLii, Bw. Greg Kempe wakionyesha mkataba huo.
Meza Kuu ikiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe Dkt. Damasi Ndumbaro (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sekretarieti ambayo imeandaa warsha hiyo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni