Na Lydia Churi na Charles Ngusa-GEITA
Mahakama ya Tanzania imeendelea kusogeza huduma zake
karibu zaidi na wananchi ambapo hivi karibuni mkoa wa Geita utaanza kutoa
huduma za Mahakama Kuu ambayo itakuwa ni
Mahakama Kuu ya mfano katika matumizi ya mtandao.
Akizungumza na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa
Mahakama ngazi ya Mkoa na wilaya za mkoani Geita, Jaji Mkuu wa Tanzania na
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma amesema
Geita itakuwa ni Mahakama Kuu ya kwanza kuachana na matumizi ya karatasi kwa
kuwa itatumia zaidi mtandao kuendesha shughuli zake.
”Zaidi ya wananchi 2,977,608 wa Mkoa wa Geita wamekuwa wakienda
umbali mrefu kufuata huduma huduma za Mahakama Kuu mkoani Mwanza, hivyo
kuanzishwa kwa Mahakama Kuu katika mkoa huu kutasogeza karibu zaidi huduma kwa
wananchi”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema maandalizi ya kuanzishwa kwa Mahakama Kuu mkoani
Geita yanaendelea ambapo tayari jengo limefanyiwa ukarabati. Aliushukuru uongozi
wa mkoa wa Geita kwa kuipatia Mahakama ya Tanzania jengo la muda litakalotumiwa
na Mahakama ya Hakimu Mkazi ambayo majengo yake yatatumiwa na Mahakama Kuu.
Aidha, Jaji Mkuu alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe.
Martin Shigella kwa kuonesha utayari wa kuwa na huduma hiyo na pia juhudi kubwa
ya kushirikiana na Mahakama ili
kuhakikisha mkoa wa Geita unakuwa na Mahakama Kuu.
Alimtaka Mkuu huyo wa mkoa kuendeleza juhudi zake katika
kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo ni kuboresha hali ya
maisha ya watanzania na ustawi wa wananchi wa mkoa wake na kuimarisha mazingira
ya amani, usalama na umoja.
Alisema Mahakama ya Tanzania inao mchango mkubwa katika
uwepo wa mazingira ya amani, usalama na umoja kwa kuwa wananchi wanapofika
mahakamani wanaamua kutatua migogoro yao kwa amani badala ya kutumia nguvu
inayoweza kuvuruga amani na usalama wa nchi, hivyo kujenga utaifa na udugu.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna wa Tume ya
Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amewataka Viongozi na watumishi wa Mahakama mkoani Geita
kujiandaa kuanzisha Mahakama Kuu hususan kuandaa mifumo ya Masjala.
”Mkuu wa mkoa wa Geita ameonesha uhitaji na utayari wa
kuwa na huduma za Mahakama Kuu hivyo utayari wake ni lazima uendane na
maandalizi mazuri”, alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani amewataka watumishi wa Mahakama mkoani humo kutoa
ushirikiano kwa Majaji, viongozi wengine
pamoja na watumishi watakaoanzisha masjala ya Mahakama Kuu.
Alimtaka Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzannia
kuainisha mahitaji ya uanzishwaji wa Masjala hiyo pamoja na masjala nyingine za
Mahakama Kuu zinazotarajiwa kuanzishwa kwa wingi hivi karibuni.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Geita ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kasi yake katika
uboreshaji wa huduma za kimahakama nchini na kuongeza imani ya wananchi kwa
Mhimili huo.
”Kila unapoona demokrasia inashamiri, amani na utulivu
unaimarika ujue ni kwa sababu Mhimili unaosimamia haki unatimiza wajibu wake
ipasavyo”, alisema Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Mkuu huyo wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa aliwataka wakuu wa wilaya ambao ni
Wenyeviti ngazi ya wilaya kuona umuhimu wa kushirikiana na Mahakama katika
kuimarisha utendaji kazi wa shughuli za utoaji haki mkoani Geita.
Aidha, Bw. Shigella alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Geita
kutafuta kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Majaji.
Kuanzishwa kwa Mahakama Kuu mkoani Geita kutaifanya
Mahakama ya Tanzania kuwa na jumla ya kanda 18 za Mahakama Kuu nchini. Lengo la
Mahakama ni kuwa na Mahakama Kuu kwenye kila mkoa nchini. Mikoa ambayo bado
haina huduma za Mahakama Kuu ni pamoja na Singida, Simiyu, Katavi, Lindi,
Pwani, Songwe na Njombe.
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma akizungumza.
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania Makao Makuu na wale wa Mahakama mkoani Geita wakiwa kwenye Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama jana mkoani Geita.
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigella alipomtembelea ofisini kwake. Wengine ni Makamishana wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Viongozi wa Tume.
Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigella akizungumza na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama walipomtembea ofisini kwake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni