Na Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) kwa kushirikiana na washiriki mbalimbali wa
mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI)
leo tarehe 13 Octoba, 2023 wameungana na wanamichezo wengine kufanya matendo ya
huruma kwenye vituo vinne vya watu wenye mahitaji maalum.
Uongozi wa SHIMIWI Taifa
chini ya Katibu Mkuu Alex Temba uliongoza shughuli hiyo, huku Mahakama Sports
ikiwakilishwa na wajumbe 12 akiwemo Katibu Mkuu Robert Tende. Vituo
vilivyotembelewa ni Kituo cha Watoto Yatima Tosamaganga na vingine vya Ismani,
Huruma na Furaha. Zawadi zilizotolewa zinajumla ya thamani ya shillingi
13,750,000.
Shughuli ya kutembelea
vituo hivyo ilianza majira ya saa tatu na nusu hivi asubuhi kutokea katika
Viwanja vya Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha baada ya Viongozi wa SHIMIWI
kuwagawa wanamichezo katika makundi manne kutokana na umbali wa vituo
vilivyokuwa vimepangwa kutembelewa.
Mahakama Sports
waliungana na wanamichezo wengine kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Mifugo, Ras Mara na wengine kutembelea Kituo cha Tosamaganga, huku Katibu Mkuu SHIMIWI
Alex Temba na Mratibu wa Masuala ya Kijamii Itika Mwankeja wakiongoza msafara
huo.
Baada ya kuwasili katika
Kituo hicho, wanamichezo hao walipokelewa na Mkuu wa Kituo Sister Hellena Kihwele
ambaye aliwatembeza katika maeneo mbalimbali na kukutana na watoto.
Wanamichezo hao
wameonesha upendo wa ajabu kwa watoto waliowakuta kwani walikuwa wanawagombania
kuwabeba na kucheza nao michezo mbalimbali ya kitoto. Watoto walionekana kuwa
na nyuso za furaha baada ya kuwaona wanamichezo hao.
Baada ya kuonesha upendo
huo, Viongozi wa SHIMIWI na wanamichezo walikabidhi zawadi mbalimbali kwa Mkuu
wa Kituo kwa niaba ya watoto.
Akizungumza wakati wa
makabidhiano hayo, Katibu Mkuu SHIMIWI alimweleza Sister Hellena kuwa zawadi
hizo zinatokana na michango iliyotolewa na wanamichezo kutoka wizara, taasisi
na idara mbalimbali ambazo zipo mkoani Iringa kwa ajili ya mashindano.
"Tupo hapa Iringa
kwa ajili ya mashindano yanayojumuisha watumishi wa umma kutoka Wizara, Idara
na Taasisi mbalimbali za Serikali. Kabla hatujamaliza mashindano haya tumeamua
kuja kuwaona watoto wetu kwa ajili ya kuwapa zawadi kidogo. Tumejichangisha
kidogo kidogo kwenye posho zetu ili kupata zawadi hizi. Naomba uzipokee,"
amesema.
Naye mratibu wa masuala
ya kijamii SHIMIWI amemweleza Mkuu wa Kituo kuwa zawadi ambazo wameziwasilisha
zimezingatia makundi yote ya watoto, ikiwemo mchele, unga, sabuni, mafuta ya
kula, maziwa, dawa za mswaki, miswaki, juice, madaftari na vingine vingi.
Amemwomba Sister Hellena
kupokea zawadi hizo ili ziweze kusaidia ingawa kwa uchache ili watoto hao
waweze kuvitumia. Kadhalika, Dada Itika alikabidhi fedha taslimu millioni moja
kwa Mkuu huyo wa Kituo ili ziweze kusaidia katika mahitaji mbalimbali.
Akipokea zawadi hizo,
Sister Hellena amewashuku Viongozi wa SHIMIWI na wanamichezo wote kwa moyo wa
huruma waliouonesha kwa watoto hao. Amesema zawadi walizotoa kweli zimezingatia
watoto wote waliopo kwenye Kituo chake, hivyo akashukuru kwa majitoleo hayo.
" Kwa mfano hapa
tuna watoto ambao wametoka jeshini baada ya kumaliza mafunzo kwa mujibu wa
sheria. Hawa ni wahitimu wa kidato cha sita na wamekulia hapa hapa. Tunasubiri
mamlaka ziwapatie mikopo kwa ajili ya kwenda vyuoni. Kama hawatapata, basi
nitakaa nao hapa hapa maana sina pa kiwapeleka" amesema.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Aines Kedimondi amewashukuru wanamichezo wote kwa kujitoa na kuomba makundi na watumushi wengine wa umma kuiga mfano huo kwa maslahi ya watoto na wenye uhitaji maalum.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni