Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor amewapongeza wadau wote
wa Mahakama kwa mchango wao mkubwa katika kuondoa mashauri ya mlundikano.
Mhe. Mansoor alitoa
pongezi hizo wakati wa vikao vya kusukuma mashauri ya jinai na madai
vilivyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki
kilichopo mkoani hapa.
“Hili ni jambo la
kujivunia kuwa Kanda yetu ya Morogoro hakuna kesi za mlundikano, hongereni sana
kwa wadau wetu maana mngetukwamisha tusingeweza kuyafikia haya mafanikio,
juhudi zenu zinafahamika” alisema.
Mhe. Mansoor aliongeza kuwa
watumishi wa Mahakama wote kwa umoja wao wamechangia pia katika kufikia mafanikio
hayo.
Kauli hiyo ya Jaji
Mfawidhi iliungwa mkono na Jaji wa Mahakama Kuu katika Kanda hiyo, Mhe. Gabriel
Malata ambaye alisema timu hiyo ya wadau wa Mahakama ni ya ushindi ambayo
haipaswi kurudi nyuma katika zoezi zima la utoaji haki.
Naye Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Augustina Mmbando alieleza hali
ya mashauri kwa upande wa Mahakama Kuu kwa kipindi cha mwezi Julai hadi tarehe
26 Oktoba, 2023.
Alieleza kuwa mashauri ya
madai yaliyofunguliwa kwa kipindi hicho yalikuwa 218, yaliyomalizika ni 270 na
yaliyobakia na yanaendelea kusikiliza ni mashauri 254.
Kwa upande wa mashauri ya
jinai, Mhe. Mmbando alieleza kuwa kuanzia Julai hadi 27 Oktoba, 2023
yalifunguliwa 182, yaliyosikilizwa ni 191 na yaliyobakia ni 80. Alisema kwa
sasa hakuna mashauri ya mlundikano na hawategemei kuwa nayo katika kituo hicho.
Naibu Msajili alitumia
fursa hiyo kuwajulisha wadau juu ya matumizi ya mfumo mpya wa usajili wa
mashauri (e-CMs) ambao ni maboresho ya mfumo wa JSDS2 na kuongeza kuwa kwa sasa
mfumo huo upo kwenye majaribio.
Alisema kuwa hivi punde mfumo
huo mpya utaanza kutumika kikamilifu, hivyo aliwahimiza kufanya jitihada za
kujifunza na kuujua mfumo huo.
“Rai yetu wadau wetu wote
kuendelea kuzingatia matumizi ya mifumo hii, pia nitoe pongezi za dhati kwa
wadau wetu wanaokwenda sambamba na kasi yetu ya uendeshaji na usikilizaji wa mashauri”
alihitimisha Mhe. Mmbando.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kwa Kanda ya Morogoro, Msomi Baraka Lweeka aliipongeza Mahakama kwa kupiga hatua kubwa na kwa ushirikiano mzuri wanaoupata, hivyo kuchochea mashauri humalizika kwa wakati.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor akiendesha vikao vya
kusukuma mashauri vilivyofanyika hivi karibuni.
Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Gabriel Malata akifuatilia taarifa iliyokuwa
ikisomwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Augustina
Mmbando (hayupo pichani).
Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Augustina Mmbando akiwapitisha wajumbe
wa kikao kwenye taarifa ya mashauri wakati wa vikao vya kusukuma mashauri.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Livin Lyakinana akifuatilia jambo wakati
wa kikao.
Bi. Neema Haule kutoka
Ofisa ya Taifa ya Mashtaka Morogoro akichangia mada wakati wa kikao hicho.
Sehemu ya wajumbe wakati
wa kikao wakifuatilia masuala mbalimbali.
Wajumbe wa kikao ambao pia
ni Wenyeviti wa Mabalaza ya Ardhi Morogoro wakifuatilia mjadala wakati wa
kikao.
Kaimu Mtendaji wa
Mahakama Kanda ya Morogoro, Bi. Elinuru Maleko akifuatilia mijadala ndani ya
kikao cha kusukuma mashauri.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni