Jumatano, 13 Machi 2024

KAMATI YA BUNGE YAKAGUA MRADI WA UJENZI WA IJC NJOMBE

·       Kamati yaridhishwa na hatua za awali za ujenzi.

·       Yaipongeza Mahakama na Serikali kuendelea kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi.

Na Innocent Kansha – Mahakama, Njombe.

Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria leo tarehe 13 Machi, 2024 imekagua Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki IJC' kinachojengwa mkoani Njombe chenye thamani ya shilingi takribani Bilioni 7.6 mradi unaotekelezwa na Mahakama ya Tanzania.


Akizungumza wakati wa zoezi la ukaguzi wa kituo hicho Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Kizito Muhagama amesema mradi huo ni moja ya miradi mikubwa inayotekelezwa nchini kupitia Wizara ya Katiba na Sheria na Mtekelezaji wa mradi ni Mhimili wa Mahakama.


“Mradi huu ni wa kutoa huduma za sheria kwenye jengo moja ‘Integrated Justice Centre’ ambapo Mahakama za ngazi mbalimbali zinakuwa katika jengo moja ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi lakini pia wanaotoa haki waweze kutekeleza wajibu wao na majukumu yao kwa namna ambayo ni jumuishi na rahisi zaidi,” ameeleza Mhe.Dkt. Muhagama.


Mhe. Dkt. Muhagama amesema, hatua ya ujenzi inayoendelea katika Mradi huo ni asilimia 5 ni kama hatua za awali za ujenzi na kwa maelezo Kamati iliyopewa kutoka Serikalini na kwa Mkandarasi ni sawa kwa maana kwamba ujenzi upo ndani ya muda uliokusudiwa kimkataba.


“Mradi hauna changamoto za moja kwa moja unazozigusa Serikali kwenye utekelezaji wake. Kamati ilidhani kuna changamoto za upatikanaji wa vibali kwa maana ya misamaha ya kodi na Mkandarasi ametuhakikishia kwamba hicho siyo kikwazo katika utekelezaji wa mradi huo, ni imani yangu pamoja na wajumbe wa kamati hii kwamba Mradi upo vizuri na utaisha kwa muda uliopangwa,” amesisitiza Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge.


Kamati imempongeza Rais wa Jamhuri ya Mhungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuthubutu na kwa kuamua kwa dhati kabisa kusogeza huduma ya utoaji haki kwa wananchi wa Tanzania ambao wanahitaji huduma hiyo inayotekelezwa mkoani Njombe na maeneo mengine nchini, amesema Mbunge huyo kwa niaba ya Kamati.


“Lakini hii ni hatua kubwa sana ya kuboresha mifumo ya utoaji haki nchini ikizingatiwa kwamba, tunaendelea kuijenga Tanzania ambayo ina hali ya utulivu na amani ya kutosha,” amesema Mhe. Muhagama.


Aidha, Mhe. Dkt. Muhagama ameongeza kuwa, kwakuwa Mradi huo umeshuhudiwa na Wabunge wa Kamati hiyo kwa pamoja ni imani yao kuwa changamoto zozote zitakazojitokeza zitatolewa taarifa kwa ukaribu zaidi ili wakati wa kupanga bajeti zisaidie kutatuliwa kwa mwaka ujao wa fedha ambao utahusu pia uendelezaji na ujenzi wa miundombinu ya utoaji haki kwa Watanzania.


Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Pindi Chana amesema ukaguzi huo wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria unaenda sambamba na maelekezo ya Rais Samia ya kuboresha miundombinu ya utoaji haki kwa maana ya “Reforms & Rebuilding” ili Watanzania wote wapate haki kwa usawa na kwa wakati kama ilivyokusudiwa.


“Kamati hii ya Bunge inatusaidia sana mawazo mapendekezo ya namna bora ya kuboresha shughuli za utoaji haki kupitia Serikali na Mahakama. Japo kuwa tunajua jukumu la Bunge ni kupitisha bajeti, kutunga sheria na kuisimamia Serikali. Hivyo leo tupo katika jukumu mojawapo la Bunge la kusimamia Serikali ‘Oversight role’ ya kupitia Kamati ya Bunge baada ya kupitisha Bajeti hii ndiyo kazi ya Kamati,” amesema Mhe. Dkt. Chana.


Mhe. Dkt. Chana amesema, kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imedhamiria kuhakikisha utawala wa sheria unakuwa ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali.


“Tunataka kuona wawekezaji wakija wawe na imani na Utawala wa Sheria, tunataka Watanzania waishi kwa amani, kwa uhuru kusiwepo na changamoto za kijinai na pale zinapojitokeza basi tuwe na miundombinu ya kudhibiti na kukabiliana nazo,”


Mhe. Dkt. Chana ameongeza kuwa miundombinu hiyo inayojengwa inakwenda sambamba na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia Duniani hasa katika eneo la utoaji haki, ikiwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa IJC Njombe.


Naye, Mkadiriaji Majengo kutoka Mahakama ya Tanzania, Bw. Abdallah Nalicho akifanya wasilisho fupi la Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) mkoani Njombe, amesema kuwa ujenzi wa kituo hicho umezingatia mahitaji mbalimbali yanayoendana na uhalisia na matarajio ya wananchi watakaopata huduma za haki ndani ya jengo hilo. Kwa kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri, kuokoa muda na kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa watoa haki.


“Mathalani usanifu wa jengo hili umezingatia mahitaji ya watu wenye mahitaji maalum mfano; walemavu, watoto, akina mama wanaonyonyesha na wajawazito, wazee wasiojiweza na wadau mbambali katika mnyororo wa utoaji haki wanaosaidiana na Mahakama (waendesha mashtaka, mawakili wa kujitengemea, watoa ushauri wa kisheria, ustawi wa jamii, dawati la jinsia na Mahakama maalum kwa ajili ya watoto waliokinzana na Sheria,” ameongeza Bw. Nalicho.


Akielezea faida za ziada za ujenzi wa Kituo hicho, Bw. Nalicho amesema kimesaidia kutoa ajira kwa wataalum wa masuala ya ujenzi wapatao 23 na wafanyakazi wasio wataaluma wa ujenzi wenyeji wa Mkoa wa Njombe na hivyo kukuza na kuongeza kipato cha wananchi kupitia Mradi huo.  


Mwenyekiti wa Kamti ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Kizito Muhagama(wa pili kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ukaguzi wa Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) mkoani Njombe leo tarehe 13 Machi, 2024.


Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana akizungumza na Wanahabari wakati wa ukaguzi uliofanywa na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kwenye Mradi wa ujenzi wa IJC mkoani Njombe.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Pindi Chana akizungumza na wanahabari wakati wa ukaguzi wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria wakikangua ujenzi wa mradi wa IJC mkoani Njombe.


Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria wakichangia wasilisho la taarifa ya Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kinachojengwa mkoani Njombe na Mahakama ya Tanzania.

Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria wakichangia wasilisho la taarifa ya mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kinachojengwa mkoani Njombe na Mahakama ya Tanzania.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana akichangia jambo wakati wa kuwasilisha taarifa fupi ya Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha utoaji haki mkoani Njombe wakati wa ukaguzi wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria.
Mkadiriaji Majengo kutoka Mahakama ya Tanzania, Bw. Abdallah  Nalicho akifanya wasilisho fupi la Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) mkoani Njombe.

Mkadiriaji Majengo kutoka Mahakama ya Tanzania, Abdallah Chande Nalicho akifanya wasilisho fupi la Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) mkoani Njombe.

Mwenyekiti wa Kamtai ya Bunge ya Katiba na sheria Mhe. Dkt. Joseph Kizito Muhagama (katikati) akisema jambo wakati wa wasilisho la mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani Njombe wakati wa ukaguzi wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria mkoani Njombe.

Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na sheria wakifuatilia wasilisho la taarifa ya mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kinachojengwa mkoani Njombe na Mahakama ya Tanzania. Kulia ni  Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana.


Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na sheria wakifuatilia wasilisho la taarifa ya mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kinachojengwa mkoani Njombe na Mahakama ya Tanzania. Kulia ni  Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Pindi Chana.


Mwenyekiti wa Kamti ya Bunge ya Katiba na sheria Mhe. Dkt. Joseph Kizito Muhagama (katikati) akifuatilia wasilisho la Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani Njombe wakati wa ukaguzi wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria mkoani Njombe.

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Njombe, Bw. Yusuph Msawanga akitoa taarifa ya maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani Njombe wakati wa ukaguzi wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria mkoani Njombe.
    

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na sheria wakiwasili katika eneo la Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) mkoani Njombe leo tarehe 13 Machi, 2024.

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria wakiwasili katika eneo la Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) mkoani Njombe leo tarehe 13 Machi, 2024.

(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni