Na Innocent Kansha-Mahakama.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 13 Mei amekutana na
kufanya mazungumzo na wajumbe wa Bodi
ya Mahakama Saccos Ltd na kuahidi kuendea kuwapa ushirikiano ili ushirika huo
uweze kukua na kutimiza adhima ya kuwa chama cha ushirika wa
akiba na mikopo cha kuigwa na cha kisasa.
Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika
Ofisini kwake jijini Dar es Salaam Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma amesema eneo la
wanachama ambao ni watumishi wa Mahakama ni muhimu sana kwani Mahakama ina watumishi
zaidi ya 5,000 lakini wanachama wa Saccos wapo 524, hii inaonyesha bado kuna mtaji
mkubwa upo nje unaweza kusaidia kuongeza mtaji ushirika.
Jaji
Mkuu akatoa rai kwa viongozi hao kutumia fursa za uboreshaji wa miundombinu ya
Mahakama hasa majengo yanayo endelea kujengwa nchi zima kubuni miradi ya
kuwekeza katika maeneo hayo ili kukuza mtaji wa Saccos kama vile kuomba zabuni
za ndani za kutoa huduma kwa wanachama wao.
“Nimepokea
taarifa yenu imesheheni mambo mengi muhimu ya kufanyia kazi, pengine niseme tu
haitokuwa sahihi kwa baadhi ya mambo kuyatolea majibu ya papo kwa papo ni vema
nikae na viongozi wenzangu tujadiliane namna bora ya kutatua sehemu ya
changamoto mlizowasilisha,” amesema Jaji Mkuu.
Mhe.
Prof. Juma amesema Mahakama itaendelea kutoa fursa mbalimbali za kuitangaza Saccos
kwa watumishi na Taasisi zingine kupitia mikutano kama vile Baraza la
wafanyakazi, ziara za viongozi katika maeneo mbalimbali nchini Makongamano,
Maadhimisho, Sherehe, Mikutano na maonyesho mbalimbali yanayoandaliwa na Mahakama ya Tanzania ili viongozi wa Saccos wapate muda wa
kuhamasisha wanachama wajiunge na ushirika ili ukue.
“Nimependa
sana Mwenyekiti wa Bodi alivyotoa mifano ya JMAT na TAWJA walivyoweza kusaidiwa
kuimarisha umoja wao nanyi mnaomba kusaiwa kuimarisha mtaji wanu tena mnaomba
kusaidiwa kwa wamu moja tu. Ninaamini hilo pia linawezekana tukishirikiana,”
amesema Jaji Mkuu.
Jaji
Mkuu amesema ana amini sana katika nguvu ya Saccos na ni njia bora inayoweza
kuinua wanyonge. Ukipitia ripoti nyingi za utafiti wa REPOA sehemu ya changamoto
za watumishi zimeainishwa nyingi sana, ni vema kupitia Saccos ikaleta chachu ya
kutatua hizo changamoto.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi
Mwandamizi na Mwenyekiti wa Bodi ya Mahakama Saccos
Mhe. Ferdinand Philip akisoma taarifa ya Saccos hiyo amebainisha malengo na
matarajio ya uongozi wa Bodi hiyo ni kuimarisha Chama ili kukua zaidi kwa kupata wanachama wengi
zaidi kutokana na mikakati iliyopo ya kutoa elimu, hamasa na uelewa zaidi juu
ya manufaa mengi yatokanayo na kuwa mwanachama wa Mahakama Saccos Ltd.
“Dhima ya ushirika ni kuinua, kustawisha na kuboresha
hali ya kiuchumi na kijamii kwa wanachama, kwa kuwahamasisha kuweka akiba na
kuwapatia mikopo yenye manufaa na riba nafuu pamoja na huduma zingine za
kifedha kwa kutumia mfumo wa teknolojia ya kisasa,” amesisitiza Mhe. Philip.
Mhe. Philip amesema maendeleo ya Chama ni makubwa
kwani Chama kimeendelea kuboresha huduma za mikopo ili kuwawezesha wanachama
wake kiuchumi. Aidha, katika kipindi cha kuanzia Januari, mwaka 2024, chama
kimeweza kukusanya kiasi kikubwa cha fedha kama ilivyoainishwa na takwimu fedha
kama ifuatavyo; Akiba ya wanachama ni shilingi 1,166,321,000/-, Hisa za
Wanachama ni shilingi 30,750,000/-, Wadai na malipo ya mbele ni shilingi
98,472,160/- na Riba tarajiwa isiyoiva ni shilingi 102,904,692/-.
Kwa upande wa manufaa wanayopata wanachama wa Mahakama
Saccos Ltd, Mhe. Philip amesema kuwa, wanachama wa Mahakama Saccos Ltd ambao ni
watumishi wa Mahakama ya Tanzania, wameweza kupata mikopo mbalimbali yenye riba
na masharti nafuu, ambayo imeweza kutatua mahitaji yao ya kifedha na kuweza
kufanikisha mambo mbalimbali kama vile: kuanzisha miradi mbalimbali ya kibiashara,
kununua viwanja vya makazi na kujenga nyumba zao za kuishi
Mafanikio mengine ni kama kujiendeleza kielimu, kuwasomesha
watoto na wategemezi wao, kununua vyombo vya usafiri, kuwawezesha watumishi
wapya kupata fedha za kuanzia maisha na kupata mikopo ya dharula kwa ajili ya matibabu
ya ndugu na familia zao, ameongeza Mwenyekiti wa Bodi.
Mhe. Philip amesema, eneo lingine la faida kwa
wanachama ni elimu na mafunzo ya ushirika, biashara na ujasiriamali
yanayopatikana kwa kuwa mwanachama wa Mahakama Saccos Ltd. Elimu na mafunzo hayo
ni kama, matumizi bora ya
mikopo wanayokopa, uanzishwaji wa miradi mbalimbali ya kibiashara yenye tija.
Usimamizi bora wa miradi
wanayoianzisha, udhibiti wa mitaji, elimu ya ujasiriamali na elimu ya maisha
baada ya kustaafu.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa ufafanuzi wa mambo kadhaa wakati wa mazungumzo na wajumbe wa Bodi ya Mahakama Saccos Ltd waliofika ofisini kwake leo tarehe 13 Mei, 2024
Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mwenyekiti wa Bodi ya Mahakama Saccos Mhe. Ferdinand Philip akisoma taarifa ya Mahakama Saccos Ltd huku Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akiwa anamsikiliza kwa umakini mkubwa.
(Picha na Innocent Kansha-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni