Jumatano, 29 Mei 2024

UANZISHWAJI WA IJC KINONDONI WANUFAISHA WANANCHI

Na Mary Gwera, Mahakama-Dar es Salaam

Mtendaji wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni, Bw. Beatus Benedictus amesema tangu kuanzishwa kwa Kituo hicho hadi sasa kimehudumia jumla ya idadi ya wananchi wapatao 41,582.

Akizungumza hivi karibuni na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano- Mahakama ya Tanzania, Bw. Gerard Chami aliyefanya ziara katika Kituo hicho kwa ajili ya kujitambulisha, kujua mafanikio na namna Kituo kinavyofanya kazi, Mtendaji huyo alibainisha kuwa, uanzishwaji wa Kituo hicho umekuwa wa manufaa kwa wananchi na watumishi pia.

“Tunashukuru uwepo wa IJC Kinondoni umeleta matumaini na mafanikio makubwa na mazuri kwenye jamii inayotuzunguka pamoja na Watumishi kiujumla,” alisema Bw. Benedictus.

Akizungumzia kuhusu hali ya Mashauri kwa upande wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni/Kinondoni, Mtendaji huyo, alisema idadi ya mashauri yaliyofunguliwa Januari-Desemba, 2020 yalikuwa 987. Aliongeza kuwa, idadi ya mashauri yaliyofunguliwa Januari-Desemba, 2021 yalikuwa 1,971 yaliyoamuliwa ni 856 yakiwemo na mashauri ya nyuma.

Kwa upande wa Mahakama ya Wilaya Kinondoni, Bw. Benedictus alieleza kwamba, mashauri yaliyofunguliwa katika Mahakama hiyo kuanzia Januari hadi Desemba, 2020 yalikuwa 1,015 na mashauri yaliyoamuliwa ni 856 yakiwemo na mashauri ya nyuma.

Kadhalika, katika Mahakama hiyo kwa mwaka 2021, jumla ya mashauri 1,047 yalifunguliwa na kati ya mashauri hayo yaliyoamuliwa ni 1,044 yakiwemo na mashauri ya nyuma.

Kwa upande wa Mahakama ya Mwanzo Kinondoni, idadi ya mashauri yaliyoamuliwa Mahakama Januari hadi Desemba, 2020 ni 780 na Mashauri yaliyoamuliwa ni 9,88 yakiwemo na mashauri ya nyuma. Idadi ya mashauri yaliyofunguliwa Januari 2021 hadi Dec 2021 ni 1,233 yaliyoamuliwa ni 1,182 yakiwemo na mashauri ya nyuma.

Aidha, alibainisha kuwa, kabla ya kuanzishwa kwa IJC Kinondoni kulikuwa na jumla ya mashauri 188 yakiwa ni mashauri ya mrundikano na baada ya kuanzishwa kwa Kituo hicho kuna jumla ya mashauri ya mrundikano ni 48 pekee.

Akizungumzia namna Kituo hicho kinavyoshughulikia malalamiko, Mtendaji huyo alieleza kwamba, malalamiko yote hupokelewa kwenye dawati maalum la malalamiko na kwa njia ya mfumo na kisha kuingizwa kwenye mfumo maalum wa malalamiko ambapo mteja na mshughulikiaji wa malalamiko wote kwa pamoja wanapata ujumbe.

Aliongeza kuwa, ujumbe huo hutoa mrejesho wa namna lalamiko la Mlalamikaji lilivyoshughulikiwa na kama bado halijashughulikiwa limefikia hatua gani.

Kadhalika, alieleza kuwa, katika Kituo hicho kuna madawati maalum kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kijinsia na kutoa misaada ya kisheria.

“Dawati la Jinsia husaidia kumaliza migogoro midogo midogo ya kijinsia ambapo wananchi hupata kujua haki zao kwa kuelewa undani wa mambo jinsi yanavyopaswa kuwa,” alisema.

Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni-Kinondoni, Mhe. Is-haq Kuppa alielezea kuhusu faida za Kituo hicho ambapo alisema kwamba, pamoja na faida zingine wateja hupata huduma kwa haraka na kwa wakati sababu ya uwepo wa wadau wote katika jengo moja.

“Kupitia Kituo hiki wateja hupata huduma za rufaa kwa wakati sababu ya uwepo wa Mahakama zote muhimu kwenye jengo moja kupitia huduma hii imesaidia kwa kiasi fulani kurudisha imani kwa Mahakama kwa kufuatia huduma wanazopata,” alisema Mhe. Kuppa

Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni kilianza kufanya kazi mnamo tarehe 25 Oktoba, 2021, Kituo hicho kina jumla ya Mahakama tatu (3) yaani Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni/Kinondoni, Mahakama ya Wilaya Kinondoni pamoja na Mahakama ya Mwanzo Kinondoni. 

Hadi kufikia tarehe 03 Mei, 2024 Kituo hicho kilikuwa na jumla ya Watumishi 61 ikiwa ni idadi kwa Mahakama zote tatu zilizopo ndani ya Kituo hicho kati yao wanaume 20 na wanawake 41. Miongoni mwa idadi hiyo kuna jumla ya Mahakimu 13 ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi ina jumla ya Mahakimu watatu (3), Mahakama ya Wilaya Mahakimu sita (6) na Mahakama ya mwanzo Mahakimu wanne (4). 

Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni-Dar es Salaam.

Mtendaji wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni, Bw. Beatus Benedictus.
 
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni-Kinondoni, Mhe. Is-haq Kuppa (kulia) akiwa katika mahojiano maalum na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Bw. Gerard Chami alipotembelea Kituo hicho hivi karibuni.
 
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni-Kinondoni, Mhe. Is-haq Kuppa akizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Bw. Gerard Chami (hayupo katika picha).
 Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Bw. Gerard Chami akimsikiliza Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni-Kinondoni, Mhe. Is-haq Kuppa (hayupo katika picha).
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kinondoni, Mhe. Jacqueline Rugemalila (kushoto) na Afisa Tawala, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni-Kinondoni, Bi. Amina Mlanda wakifuatilia mahojiano.
 
Picha ya pamoja baada ya mahojiano: Wa pili kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni-Kinondoni, Mhe. Is-haq Kuppa, wa pili kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kinondoni, Mhe. Jacqueline Rugemalila, wa kwanza kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Bw. Gerard Chami na wa kwanza kushoto ni Afisa Tawala, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni-Kinondoni, Bi. Amina Mlanda.
 
Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Bw. Gerard Chami akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja 'Call Centre' ya Mahakama ya Tanzania waliopo ndani ya jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni. Katikati ni Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mtaalam wa Kuchakata na Kupitia mrejesho wa Wananchi (Techinical Supervisor-Call Centre) na kulia ni Msimamizi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja, Mahakama ya Tanzania, Bi. Evetha Mboya. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni