Jumanne, 4 Juni 2024

KAMATI ZA MAADILI YA MAHAKIMU SIMIYU ZAAGIZWA KUKUTANA

Emmanuel oguda, Mahakama-Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda amewaagiza Wenyeviti wa Kamati za Maadili ya Mahakimu ngazi ya Wilaya ambao ni Wakuu wa Wilaya zilizopo ndani ya Mkoa huo kuhakikisha wanafanya vikao vya Kamati hizo kwani vinapaswa kufanyika kwa mujibu wa Sheria.

Maagizo hayo yalitolewa jana tarehe 03 Juni, 2024 wakati wa mafunzo kwa Wenyeviti na Makatibu wa Kamati za Maadlili ya Mahakimu za Mkoa wa Simiyu yaliyotolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali kwenye Ofisi za Mkuu wa Mkoa huo.

Aidha, Mhe. Dkt. Nawanda amewataka Wakuu wote wa Wilaya kudumisha Mahusiano na Mhimili wa Mahakama pasipo kuingilia maamuzi ya Mhimili huo,  huku akiwasisitiza Wakuu wa Wilaya pia kuwashirikisha Mahakimu wafawidhi katika maeneo yao kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu elimu kwa wananchi. 

Mkuu huyo wa Mkoa amemshukuru Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga kuandaa mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati za Maadili Mkoa wa Simiyu na kuahidi kuzingatia mada zote zilizowasilishwa sambamba na kuwahimiza Wenyeviti kuzingatia mada zote zilizowasilishwa.

Awali akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali aliwasisitiza Wakuu hao wa Wilaya kuhakikisha wanakutana mara moja kila robo ili kukidhi matakwa ya Sheria kuhusu vikao vya maadili ya Mahakimu katika maeneo yao. 

“Niwaombe sana Wakuu wa Wilaya kukutana katika vikao hivyo kwani ni muhimu kukutana na kutoa taarifa baada ya vikao hivyo. Kamati hizo zijikite zaidi katika makosa ya kimaadili ya Mahakimu,’’ alisema Jaji Mahimbali.

Wakati huo huo, Mhe. Mahimbali alimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya Mkoa wa Simiyu Ripoti ya Utafiti kuhusu kuridhika kwa watumiaji wa huduma za Mahakama ya mwaka 2023 iliyofanywa na REPOA.

Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wajumbe hao katika kutimiza wajibu wao katika kutenda kazi zao kwa mujibu wa Sheria. Yamewahusisha Wenyeviti na Makatibu wa Kamati za Maadili Mkoa wa Simiyu ambao ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Dk Yahaya Nawanda na Wakuu wa Wilaya ambao waliambatana na Makatibu Tawala kutoka Wilaya za Bariadi, Maswa, Meatu, Itilima na Busega.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda akisisitiza jambo wakati wa mafunzo kwa Kamati za Maadili za Mahakimu Mkoa wa Simiyu yaliyofanyika jana tarehe 03 Juni, 2024.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali akiwasilisha mada wakati wa Mafunzo kwa Kamati za maadili Mkoa wa Simiyu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe Frank Mahimbali (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda, Ripoti ya Utafiti kuhusu kuridhika kwa watumiaji wa Huduma za Mahakama ya mwaka 2023.
Sehemu ya wajumbe wakifuatilia mafunzo kwa Kamati za Maadili ya Mahakimu Mkoa wa Simiyu.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni