Jumapili, 30 Juni 2024

'KUSTAAFU NI LAZIMA KWA KILA MTUMISHI KAMA MUNGU AKIKUJAALIA KUFIKA UMRI WA KUSTAAFU'

Mhe. Huruma Shaidi asema hata kama umeanza kazi jana ukumbuke kuna kustaafu

Na Eunice Lugiana, Mahakama-Dar es Salaam

Naibu Msajili wa Mahakama aliyekuwa akihudumu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam iliyopo Kisutu, Mhe. Huruma Shaidi amewakumbusha watumishi wa Mahakama kuwa, kustaafu ni lazima kwa kila mtumishi hivyo ni vema kujiandaa hata kama umeajiriwa jana yapaswa kujua ipo siku ya kustaafu. 

Mhe. Shaidi aliyasema hayo tarehe 28 Juni, 2024 katika viwanja vya Mahakama wakati wa hafla ya kumuaga yeye pamoja na Msaidizi wa Kumbukumbu aliyekuwa akihudumu katika Mahakama hiyo, Bw. Evod Kimario  kufuatia kustaafu katika utumishi wa umma. 

“Hata kama umeajiriwa jana kumbuka iko siku ya kustaafu itafika inabidi kila mmoja kujiandaa,” alisema Mhe. Shaidi.

Aidha, Mhe Shaidi amewashukuru watumishi wote wa Mahakama hiyo na kuwaomba Mahakimu wote na Naibu Wasajili kutenda haki wakati wote maana kwa kutofanya hivyo kuna sauti inayosikika usiku ukiwa peke yako ikihoji kwa kutokutenda haki.

Akizungumza kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe David Ngunyale  ameeleza kwamba, kazi aliyoifanya Mhe. Shaidi imebaki kumbukumbu kwenye mioyo  na nafsi za watu wengi kwa kusimamia haki. 

Mhe Ngunyale amewaomba watumishi wenzake  walioko kazini kuiga mfano mwema wa Mhe. Shaidi ili wastaafu salama na pia kumuombea katika maisha yake ya ustaafu ili yale aliyoyashuhudia  katika maisha yote kama shahidi ayashuhudie kwa wajukuu zake  awaambie yote mikuki na furaha ili kesho yao iwe njema.

Kadhalika, Mhe. Ngunyale alikiri kuwa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ndiyo ilimfundisha uhakimu akiwa mwaka wa nne Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alikuwa pamoja na Mhe. Shaidi, Mhe. Mutungi, Mhe. Khadai, Mhe. Tiganga na wengine. 

Aidha, Mhe. Ngunyale alimshukuru  pia Msaidizi wa Kumbukumbu, Bw. Kimario ambaye pia amestaafu.

Mhe. Ngunyale aliongeza kuwa yeye alilelewa na Mhe. Shaidi wakati akiwa Naibu Msajili Kanda ya Tabora, ambapo ujio wake katika Kanda hiyo kwa wakati huo waliufurahia. 

Hafla hiyo ilihudhuriwa na  Naibu Wasajili, Mahakimu, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka, Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam-Kisutu, Bi. Athanasia Kabuyanja wadau wote wa Mahakama kwa uwakilishi pamoja na watumishi wa Kanda zote katika Mahakama hiyo.

Katika hafla hiyo, watumishi hao waliostaafu walipokea zawadi kutoka kwa watumishi na lakini pia walikata keki walioandaliwa ikiwa ni ishara ya upendo. 

Wastaafu wakiwa pamoja na wenzi wao. Wa pili  kutoka kulia ni Naibu Msajili aliyekuwa akihudumu Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam-Kisutu, Mhe. Huruma Shaidi, kushoto kwake ni mke wake. Wa kwanza kushoto ni Msaidizi wa Kumbukumbu, Bw. Evod Kimario na kushoto kwake ni mwenzi wake wakiwa katika picha ya pamoja wakati hafla ya kuwaaga baada ya kustaafu utumishi wa umma iliyofanyika tarehe 28 Juni, 2024 katika Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam-Kisutu.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale akitoa nasaha kwa wastaafu kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi katika hafla ya kuwaaga iliyofanyika tarehe 28 Juni, 2024 katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam-Kisutu.

(Imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni