Ijumaa, 14 Juni 2024

MAHAKAMA YA RUFANI ILIYOKETI MUSOMA YAHITIMISHA KIKAO CHAKE KWA MAFANIKIO

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jumla ya mashauri 32 yaliyopangwa katika Kikao cha Mahakama ya Rufani Tanzania kilichofanyikia Mahakama Kuu Kanda ya Musoma yamesikilizwa huku mashauri 30 kati ya hayo yameamuliwa na kufanya kiwango cha usikilizwaji na umalizwaji wa mashauri hayo kuwa asilimia 97.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 14 Juni, 2024 Mahakama Kuu Musoma kupitia taarifa ya Msajili wa Mahakama ya Rufani iliyotolewa katika kikao cha Mahakama ya Rufani (post session meeting) kilichoendeshwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Gherabast Mwarija.

Akisoma taarifa hiyo kwa niaba ya Msajili wa Mahakama ya Rufani, Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Mhe. Monica Ndyekobora amesema kati ya mashauri yaliyopangwa kusikilizwa katika kikao hicho, ni shauri moja pekee lililoahirishwa na jingine moja linasubiri kutolewa uamuzi.

Mhe. Ndyekobora amesema kuwa, kati ya mashauri hayo Rufaa za Jinai zilikuwa 10 na zote zimeamuliwa, Ombi la Jinai lilikuwa moja nalo pia limeamuliwa, Rufaa za Madai nane kati ya hizo sita zimeamuliwa na Maombi ya Madai yalikuwa 13 na yote yametolewa uamuzi.

Msajili huyo amesema kuwa, shauri moja lililoahirishwa ambalo lilipangwa kusikilizwa tarehe 31 Mei, 2024 liliahirishwa kutokana na mleta rufaa kuwasilisha ombi mbele ya jopo la Majaji kuomba kuongeza Ushahidi wa nyongeza.

“Baada ya kusikiliza Waheshimiwa Majaji walikubaliana na ombi la mleta rufaa na kuelekeza ushahidi wa nyongeza ukachukuliwe Mahakama Kuu na baada ya uchukuaji wa Ushahidi huo, ndipo shauri lipangwe kwa usikilizwaji na Msajili,” ameeleza Mhe. Ndyekobora.

Ametaja baadhi ya changamoto zilizojitokeza kuwa ni pamoja na baadhi ya Mawakili kutotokea kwenye baadhi ya mashauri, baadhi ya Waadawa kutofika mahakamani bila taarifa licha ya kuwa wamepokea wito wa kuitwa shaurini na nyingine.

Lengo la kikao hicho ni kutoa tathmini ya  yaliyojiri wakati wa kikao cha Mahakama ya Rufani, changamoto pamoja na mapendekezo mbalimbali katika usikilizwaji wa mashauri.

Mapendekezo kadhaa yametokana na kikao hicho ikiwa ni pamoja na kuwataka Wadau wa Mahakama hususani Mawakili kuhakikisha wanapitia mabadiliko mapya ya Kanuni za Mahakama ya Rufani ili kusaidia wateja wao kupata haki kama inavyotakiwa.

Pendekezo lingine ni Mawakili wanaowakilisha wateja wanatakiwa kufika mahakamani hata kama wamejitoa kusikiliza shauri kwa sababu mbalimbali ni vema kufika mahakamani na kutoa sababu zao za kujitoa mbele ya Mahakama ili kutosababisha mashauri kuhairishwa pasipo sababu za msingi.

Lingine ni kuwataka Wadaaawa kutoa ushirikiano pale wanapopelekewa wito wa kufika mahakamani ili kuzuia shauri kuhairishwa pasipo sababu za msingi.

Aidha, wamependekeza pia, kuhakikisha kila panapokuwa na mashauri ya unyanyasaji wa kingono (Sexual Offenses Cases) Mahakimu wanaosikiliza mashauri hayo wanapaswa kuhakikisha muhanga anafichwa utambuzi wake katika maandishi ili kuzuia maumivu ya kisaikolojia anayoweza kupata huko mbeleni kama inavyosema miongozo mbalimbali.

Aidha, kupitia kikao hicho Jeshi la Magereza limepongezwa kwa kuweka vizuri anuani za wafungwa walioachiliwa kwani imekuwa rahisi kwa Mahakama kuwapata pale mashauri yao yanapokuwa yamefika katika hatua ya rufaa.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Majaji wengine wa Kanda hiyo na Wadau mbalimbali wa Mahakama wakiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Musoma, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Musoma na Mkuu wa Gereza Musoma.

Kikao cha Mahakama ya Rufani kimefanyika Musoma kuanzia 23 Mei, 2024 hadi tarehe 14 Juni, 2024 na kimeendeshwa na jopo la Majaji watatu wa Mahakama hiyo ambao ni Mhe. Augustine Gherabast Mwarija, Mhe. Abraham Makofi Mwampashi na Mhe. Zainab Goronya Muruke.

 
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Gherabast Mwarija (katikati) akiongoza kikao cha Mahakama hiyo baada ya kumaliza kusikiliza mashauri katika Kanda hiyo (post session meeting). Kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Abraham Makofi Mwampashi na kulia ni Mhe. Zainab Goronya Muruke.
Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Mhe. Monica Ndyekobora (aliyesimama mbele) akisoma taarifa kwa niaba ya Msajili wa Mahakama ya Rufani ya kikao cha Mahakama ya Rufani kilichoketi katika Kanda hiyo.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (wa pili upande wa kushoto ) na washiriki wengine wakifuatilia kikao.
Mwakilishi wa Mkuu Magereza ya Mkoa wa Musoma pamoja na wajumbe wengine  wakiwa katika kikao hicho leo tarehe 14 Juni, 2024.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe Merlyn Leonce Komba (kushoto) akifuatilia yanayojiri katika kikao. Katikati ni Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mhe. Monica Ndyekobora na kulia ni Mtunza Kumbukumbu wa Mahakama ya Rufani, Bi. Stella Mlaponi.
Sehemu ya Wadau walioshiriki wakifuatilia yanayojiri katika kikao.
Mwakilishi wa Chama cha Mawakili Kanda ya Musoma (wa pili kulia) akichangia hoja.



 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni