Jumatatu, 3 Juni 2024

MAHAKIMU 15 WAPATIWA MAFUNZO UKATILI WA KINGONO NA JINSIA


Na Magreth Kinabo na Naomi Kitonka-Mahakama

 Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia (IJC) Temeke, Mhe. Glady’s Nancy Barthy leo tarehe 03 Juni, 2024 amefungua mafunzo ya unyanyasaji wa kigono kwa mahakimu na kuwataka  kutumia elimu na ujuzi wanaoupata kuendesha mashauri ya ukatili kingono na wa kijinsia kwa kuzingatia haki na utu baina ya pande zote mbili zinazohusika.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamefunguliwa katika Kituo hicho, na yamehusisha mahakimu 15 wa ngazi mbalimbali wa mkoa wa Dar es Salaam na Pwani yenye lengo la kuwajengea uwezo mahakimu hao wa jinsi ya kuepuka kutonesha majeraha ya kisaikolojia kwa mashahidi na waathirika, hususani katika kesi za unyanyasaji wa kingono na ukatili wa kijinsia(Avoiding Re-traumatization) wanaposikiliza mashauri hayo.

Ameongeza kwamba mafunzo hayo pia yanalenga kuhakikisha wanazingatia  kanuni za kisheria na maadili  na matumizi ya teknolojia katika kushughulikia mashahidi na waathirika hao.

“Katika mafunzo haya ya siku tatu, nina matumaini kuwa tutajifunza na kuongeza uwezo wetu wa utoaji haki kwa usahihi na kujua namna ya kuwalinda na kuwahudumia waathirika hao wanapokuwepo mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi,” amesema Jaji Barthy.

Jaji Barthy amesema kuwa agenda kuu ya siku ya leo ni kuwawezesha kuwa na uelewa wa uhusiano uliopo kati ya kuwalinda waathirika wa ukatili wa kingono na kijinsia na kutimiza majukumu yao katika kusimamia haki. Hivyo mafunzo hayo yanawapa nafasi ya kubadilisha namna wanavyowahudumia na kuwalinda waathirika hao katika utaratibu wa kisheria pamoja na kuelewa nafasi waliyonayo kama Majaji na Mahakimu wanaposimamia na kutoa haki.

Mafunzo hayo yameandaliwa na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) kwa ufadhili wa Irish Rule of Law International (IRLI) na wawezeshaji ni Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu pamoja na Maafisa wa Ustawi wa Jamii wa ngazi mbalimbali.

Mafunzo hayo ni moja ya maeneo ya Makubaliano ya Mashirikiano (MoU) baina ya IJA na IRLI yaliyosainiwa Machi 2022.



Picha ya Juu na chini ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia (IJC) Temeke, Mhe. Glady’s Nancy Barthy akifungua mafunzo ya unyanyasaji wa kigono na ukatili wa kijinsia kwa mahakimu. yaliyofunguliwa leo katika kituo hecho.


Baadhi ya Mahakimu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani wakiwa katika mafunzo ya ukatili wa kingono na Kijinsia.

Mwezeshaji kutoka IJA Raymond Kaswaga 
akitoa mada juu ya ukatili huo.


Mwezeshaji kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Bw. Baraka Msike akitoa mada ya nafasi ya  Ofisa Ustawi wa Jamii juu ukatili huo.

 

Mwezeshaji  Nabwike Mbaba akitoa mada juu ya ukatili huo.


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Mhe.Ishaq Kuppa akichangia mada,

Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Mhe. Bittony Mwakisu akichangia mada.
    Picha ya juu na chini ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia (IJC) Temeke, Mhe. Glady’s Nancy Barthy (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo.





 







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni