Jumanne, 4 Juni 2024

MAHAKIMU WAFUNDWA JINSI YA KUENDESHA MASHAURI YA UKATILI WA KINGONO

Na Seth Kazimoto - Mahakama Kuu Arusha

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga amefungua mafunzo ya Wakufunzi juu ya kuzuia athari kwa waathiriwa wa unyanyasaji wa kingono na kijinsia ili kuwajengea uwezo Majaji na Mahakimu namna bora ya ushughulikiaji wa mashauri yanayohusu wahanga wa vitendo hivyo kuanzia ngazi ya familia.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo jana tarehe 03 Juni, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha, Mhe. Tiganga alisema kuwa, Washiriki watajifunza pia namna matukio hayo yanavyoripotiwa katika Vituo vya Polisi na yanavyoendeshwa mahakamani.

Alisema pia mafunzo hayo yanalenga kuwapa Majaji na Mahakimu uwezo wa kuzuia na kuepusha kurejesha majeraha yatokanayo na ukatili wa kingono na kijinsia kwa ujumla wake. Aliongeza, “ukatili wa kijinsia umekuwa suala kubwa katika jamii yetu, hivyo ipo haja ya kuhakikisha haki inatendeka pale mashauri ya jinsi hiyo yanapoletwa Mahakamani kwa kuzingatia hali walizonazo wahanga wa ukatili huo.” 

Mafunzo hayo yamekusudiwa pia kubadilisha namna ya kuwachukulia na kuwalinda wale ambao wako hatarini katika michakato ya kisheria. Hili linakwenda sambamba na usikivu wa Mahakama, kuchunguza mienendo tata ya unyanyasaji wa kijinsia na kuelewa jukumu muhimu ambalo Mahakama inatekeleza katika usimamizi wa haki. 

Aidha, mafunzo hayo yanaangazia pia namna ya kuendesha mashauri ya kimaadili, matumizi ya teknolojia katika kusaidia ushahidi na usimamizi bora wa mashauri ili kuzuia athari hasi kujirudia kwa wahanga wa unyanyasaji wa kingono lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa, kila Mshiriki anapata maarifa na ujuzi wa kuendesha mashauri ya unyanyasaji kijinsia kwa ufanisi na kuzingatia haki pamoja na kulinda utu wa wote wanaohusika katika shauri husika.

Watoa mada katika mafunzo hayo ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Nyigulile Mwaseba na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Mhe. Dkt. Patricia Kisinda. 

Mafunzo hayo ambayo yatafanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 03 hadi 05 Juni, 2024 yamehudhuriwa na Washiriki mbalimbali wakiwemo Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Mhe. Dkt. Patricia Kisinda na Mahakimu kutoka Mikoa ya Kanda ya Kaskazini. 

Mafunzo hayo yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania, Serikali ya Tanzania na Shirika la Kimataifa la Utawala wa Sheria la Ireland.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mafunzo ya Kuzuia Athari Hasi kwa Wahanga wa Ukatili wa Kingono na Kijinsia yaliyofanyika tarehe 03 Juni, 2024 'IJC' Arusha. Aliyeketi kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Mariam Mchomba na kulia ni Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Patricia Kisinda.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Nyigulila Mwaseba akitoa mada wakati wa Mafunzo ya Kuzuia Athari Hasi kwa Wahanga wa Ukatili wa Kingono na Kijinsia yaliyofanyika tarehe 03 Juni, 2024 IJC Arusha.

Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Patricia Kisinda akitoa mada wakati wa mafunzo ya Kuzuia Athari Hasi kwa Wahanga wa Ukatili wa Kingono na Kijinsia yaliyofanyika tarehe 03 Juni, 2024 IJC Arusha.

Washiriki wa Mafunzo ya Kuzuia Athari Hasi kwa Wahanga wa Ukatili wa Kingono na Kijinsia, Wahe. Harriet Mhenga (kushoto) na Julieth Mbise (kulia) wakishiriki kikamilifu katika mafunzo hayo yanayofanyika IJC Arusha.

Washiriki mbalimbali wa Mafunzo hayo wakifuatilia kwa umakini Watoa mada wakati wa Mafunzo ya Kuzuia Athari Hasi kwa Wahanga wa Ukatili wa Kingono na Kijinsia, yanayofanyika kuanzia tarehe 03 hadi 05 Juni, 2024 IJC Arusha.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni