Jumapili, 9 Juni 2024

MALALAMIKO YA WANANCHI KWA MAHAKAMA SIMIYU YAPUKUTIKA

  • Wasema wanapata huduma nzuri inayoridhisha

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Simiyu.

Malalamiko ya wananchi kwa Mahakama katika Mkoa wa Simiyu yanaendela kupungua kadri siku zinavyozidi kwenda kutokana na huduma nzuri inayotolewa na watumishi katika ngazi mbalimbali kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama ya Hakimu Mkazi.

Hayo yamebainishwa na Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Simiyu, Bw. Gasto Kanyairika alipokuwa anaongea na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg Gerald Chami alipofanya ziara mkoani hapa hivi karibuni.

Mtendaji huyo alisema kuwa katika Mkoa wake wanautaratibu wa kupokea malalamiko yanayotolewa na wananchi na kuyafanyia kazi kwa haraka na wahusika kupatiwa majibu.

"Tulikuwa na malalamiko 24 kwenye robo tatu, ambayo mengi yanahusu mashauri. Kati ya Julai na Septemba, 2023 yalikuwa 13, Septemba hadi Decemba, 2023 yalikuwa 11. Robo ya Januari hadi Machi 2024 yalikuwa matatu. Ukiangalia takwimu hizi utaona malalamiko yanaendelea kupungua," alisema.

Bw. Kanyairika alieleza kuwa kwa sasa wananchi wanaendelea kuelimishwa kutumia njia ya mtandao kwa kujaza lalamiko kwenye mfumo wa e-mrejesho kutoka kwenye tovuti ya Mahakama au kupiga simu kwenye Kituo cha Huduma kwa Mteja kupitia namba 0754500400 ambayo hupokelewa kwa masaa 24 na taarifa zao kushughulikiwa kwa haraka.

Mtendaji alieleza pia kuwa mrejesho walioupata wakati wa Wiki ya Sheria mwanzoni mwa mwaka huu 2024 umeonesha Wananchi wanaridhika na huduma zinazotolewa na Mahakama katika ngazi zote. Wananchi walisema wanapatiwa huduma vizuri na wanaridhika.

Alifafanua kuwa katika kipindi hicho walihudumia takribani wananchi 1,500 baada ya kupeleka elimu ya sheria kwenye mashule, Magereza, minada, vituo vya mabasi na katika jeshi la polisi.

Akizungumzia usikilizaji wa mashauri kwa ujumla katika Mkoa wake, Bw. Kanyairika alieleza kuwa kwa mwaka 2022, Mahakama katika ngazi zote zilivuka na jumla ya mashauri 385, zikasajili 5,787 mwaka 2023 na kuamua mashauri 5,224 na yanayoendelea ni 948.

Akifafanua mchanganuo wa usikilizaji huo, Mtendaji huyo alieleza kuwa Mahakama za Mwanzo zilivuka na mashauri 166 mwaka 2022, zikapokea mashauri 4,916 mwaka 2023 ambapo mashauri 4,348 yaliamuliwa na yanayoendelea ni 734.

Kwa upande wa Mahakama za Wilaya, Bw. Kanyairika alieleza kuwa Mahakama hizo zilivuka na mashauri 206 mwaka 2022, zikapokea mashauri 854 mwaka 2023 na kuondosha 852 na mashauri yanayoendelea ni 208.

Kuhusu Mahakama ya Hakimu Mkazi, alieleza kuwa mwaka wa 2022, Mahakama hizo zilivuka na mashauri 13, yakasajiliwa 17 mwaka 2023 na yaliyoamuliwa yalikuwa 24 na kubakiza mashauri sita pekee ambayo yanaendelea.

"Hapa kwetu kazi inaendelea na Mahakimu wanachapa kazi kweli kweli, huku tukiwahimiza watumishi wa kada nyingine kuwahudumia wananchi kwa weledi na kuendeleza nidhamu katika kazi,” Bw. Kanyairika alisema.

Wakati huo huo, Mahakama Mkoa wa Simiyu imefanikiwa kusuluhisha na kukomboa viwanja 20 vilivyokuwa vimevamiwa na wananchi katika maeneo mbalimbali licha ya kinunuliwa na Mahakama ya Tanzania.

Mtendaji wa Mahakama Mkoani hapa alieleza kuwa kwa sasa wanamkakati wa kuhakikisha viwanja vyote hivyo vinapimwa.

Kulikuwa na migogoro ya maeneo 20 ya Mahakama. Tumefanikiwa kutatua takribani yote. Iliyobaki ni Nyashimo na Kalemela. Tupo kwenye hatua ya kupeleka wapimaji kwenye maeneo mengine ili tuweze kupata hati," Bw. Kanyairika alisema.

Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Simiyu, Bw. Gasto Kanyairika akiongea na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg Gerald Chami alipofanya ziara mkoani hapa hivi karibuni. Picha chini, Mtendaji akionyesha nyaraka muhimu wakati wa mazungumzo hayo.






Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg Gerald Chami (kushoto) akimweleza jambo Matendaji wa Mahakama Simiyu, Bw. Gasto Kanyairika.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bariadi, Mhe. Caroline Kiliwa akizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg Gerald Chami (hayupo kwenye picha) alipoenda kujitambulisha kwake.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bariadi, Mhe. Caroline Kiliwa akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania, Ndg Gerald Chami (kulia). Kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Simiyu, Bw. Gasto Kanyairika.

 





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni