Ijumaa, 14 Juni 2024

MWAROBAINI WA MASHAURI YA MUDA MREFU MKOANI GEITA WAPATIKANA.

 Na CHARLES NGUSA , Geita.

Kikao cha Kusukuma Mashauri ya Jinai na kikao cha Menejimenti Mkoani Geita vimefanyika jana tarehe 13 Juni, 2023 katika ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya  Geita kwa nyakati tofauti huku ajenda kuu ikiwa ni kujadili namna bora ya umalizaji wa mashauri ya muda mrefu ili kuwawezesha washitakiwa katika mashauri hayo kujuwa hatima yao.

 

Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kusukuma mashauri, Kaimu Mwenyekiti wa kikao hicho, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita Mhe. Fredrick Lukuna amesema kuwa alisema ni lazima kila mdau katika kikao hicho awajibike ili mashauri hayo yaweze kumalizika kwa wakati.

 

 Ili kuimarisha dhana ya utoaji haki kwa wakati, ni lazima sisi kama wadau muhimu katika utoaji haki tuweze kuwajibika ipasavyo na kuhakikisha kila mmoja wetu anawajibika ipasavyo, pia  tuhakikishe mashauri yote yanamalizika kwa wakati  na kutoa fursa za wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji,”alisema Mhe. Lukuna.

 

Awali akiwasilisha taarifa ya mashauri ya Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe.Lukuna alisema kuwa katika masjala ya Mahakama Kuu Kanda ya Geita  hadi kufikia sasa jumla ya mashauri saba yaliyoiva, kati ya hayo na mashauri sita tayari yameshapangiwa vikao ambavyo vimepangwa kuanza tarehe 18 Juni, 2024.

 

Katika kikao hicho jumla ya mashauri  14 ya muda mrefu yalijadiliwa na kupatiwa ufumbuzi ambapo wajumbe walijadili kwa kina na kuonesha sababu ya mashauri haya kuchukua muda mrefu bila kumalizika. Hivyo waliazimia  kwamba ni vyema sasa mashauri hayo yakamalizika na kuzuia kuruhusu mashauri mengine kuingia kwenye mashauri mlundikano. 

 

Baada ya majadiliano ya muda mrefu , wajumbe wote walikuja na maazimio ya pamoja ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa katika kikao kingine  kijacho cha robo mwaka, mashauri yote ambayo yamejadiliwa  yawe yamemalizika ndani ya kipindi hiki cha mwezi Juni 2024, na pia  mahabusu wafikishwe kwa wakati ili kuruhusu Mahakama kuanza mapema na pia kuboresha mawasiliano kati ya Mahakama na Ofisi ya Mashitaka(NPS).

 

Kikao hicho cha Kusukuma Mashauri ya Jinai(Case flow management) kilihudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Mashitaka mkoani Geita ambaye kwa mujibu wa vikao hivi ndiye Katibu wa kikao, wahe. Mahakimu Wafawidhi wa Mkoa na Wilaya zote,Mkuu wa Upelelezi Mkoa, Magereza, Polisi , Ustawi wa Jamii na wengine wote wanaohusika.

 

Wakati huohuo  Mwenyekiti wa kikao cha Menejimenti Kanda ya Geita , Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina alifungua kikao hicho na kusisitiza  matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) katika kumaliza mashauri, hasa ya muda mrefu.

 

“Tujikite zaidi katika matumizi ya mtandao na hasa matumizi ya ‘Video Conferencing’ kwani ndiyo njia rahisi ya kuhakikisha kuwa hakuna kisingizio cha mhusika yeyote katika mashauri yetu anashindwa kufika Mahakamani kwa kigezo cha umbali hivyo tunao uwezo wa kuwasikiliza popote bila kufika Mahakamani,” alisema Mhe. Jaji Mhina.

 

Katika kikao hiki mambo mbalimbali yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na kusisitiza zaidi matumizi ya Video Conferencing na hasa katika Mahakama za Wilaya ya Nyangh’wale, Mbogwe na Bukombe ambazo ziko mbali na magereza  jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa ucheleweshaji wa mashauri kwani kuna nyakati mahabusu hushindwa kabisa kufikishwa mahakamani na pengine wakifika basi kwa kuchelewa  kutokana na umbali wa magereza wanapotoka.

 

Mathalani, katika Mahakama za Wilaya ya Mbogwe na Bukombe mahabusu wanapaswa kutoka katika gereza la Kahama umbali wa zaidi ya kilometa 100 na Nyangh’wale mahabusu wanatokea katika gereza la Geita umbali wa kilometa 120.

 

Waliohudhuria katika kikao cha menejimenti ni pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita ambaye ndiye Mwenyekiti wa kikao, Mhe.Kevin Mhina, Jaji wa Mahakama Kuu Geita Mhe. Griffin  Mwakapeje, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe.Fredrick Lukuna, 

 

Wengine ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Bi. Masalu  Kisasila ambaye ndiye Katibu wa kikao hicho, Hakimu Mfawidhi wa Mkoa, Wahe. Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya zote, Maafisa Tawala na Utumishi wa Mahakama zote katika Mkoa pamoja na Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Mwanzo zote katika Mkoa.


Kaimu Mwenyekiti wa kikao cha Kusukuma Mashauri ya Jinai(aliyekaa kulia)Naibu  Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita Mhe. Fredrick Lukuna akiwa pamoja na Katibu wa kikao hicho(aliyesimama kushoto) Bw. Godfrey Odupoy kutoka Ofisi ya Mashitaka Mkoa wa Geita  akifafanua jambo.


Wajumbe wa kikao wakiendelea kufuatilia uwasilishaji wa maada mbalimbali.



Mwenyekiti wa kikao cha Menejimenti Kanda ya Geita Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Kevin David Mhina(katikati) ,(kushoto) ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita Mhe. Griffin  Mwakapeje  na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Bi .Masalu  Kisasila (kulia) wakiwa katika meza kuu wakiendelea na kikao.

 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni