Jumatatu, 3 Juni 2024

WAZIRI CHANA AISHAURI IJA KUONGEZA KOZI ZINGINE ZA ELIMU

Na Mwandishi Wetu-Lushoto, IJA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito kwa uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kubuni kozi zingine za elimu ili kiwe na kozi nyingi zaidi ambazo zitazalisha wahitimu wengine wa kada zingine.

Mhe. Waziri Chana ametoa wito huo alipotembelea Chuoni hapa leo tarehe 31/05/2024 ambapo amesema kuwa IJA ni Chuo bora, hivyo kinahitaji kuzalisha wahitimu wengine bora wa kada zingine huku pia akibainisha kuwa kozi hizo zitakiongea Chuo mapato.

IJA kwa sasa inatoa kozi za Astashahada na Stashahada ya Sheria.

Pia Waziri amesema kuwa IJA ni maarufu na imejijengea heshima kubwa ya kutoa mafunzo kwa Majaji, watumishi wengine wa Mahakama pamoja na wadau wengine wa sekta ya sheria.

Vile vile, Mhe. Balozi Chana amekitaka Chuo kuziishi R nne za Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kusaidia kufikia dhamira ya Rais ya kuendelea kuwa na nchi yenye utulivu wa kisiasa, kijamii na kukuza uchumi. 

R nne hizo zilizoasisiwa na Rais Samia Julai 30, 2022 ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga upya.

Aidha, Waziri amesema kuwa Rais ana imani kubwa na Chuo na kuwasisitiza watumishi kufanya kazi kwa kujituma na kwa kujitoa.

Kwa upande mwingine, Mhe. Waziri Chana amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim H. Juma pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel kwa juhudi zao za kukiendeleza Chuo akitolea mfano wa ujenzi wa jengo la studio ya kisasa kwa ajili ya kufundishia mtandaoni (E-learning platform).

Awali, Kaimu Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Naibu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi, Bw. Goodluck Chuwa alimuelezea Waziri mafanikio na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa miundombinu ya kufundishia, uhaba wa vitendea kazi pamoja na changamoto ya kibajeti, masuala ambayo Mhe Waziri amesema Wizara imeyachukua na kwenda kuyafanyia kazi.

Kwa upande mwingine, Waziri alitembelea miundo mbinu mbalimbali ya chuo na kujionea ukarabati unaoendelea kwa baadhi ya majengo sambamba na kupanda mti ikiwa ni alama ya yeye kupanda mti hapa chuoni.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana akiwahutubia viongozi pamoja na baadhi ya Watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) alipofanya ziara Chuoni hapo mnamo tarehe 31/05/2024.

Kaimu Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Naibu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi Bw. Goodluck Chuwa akitoa maelezo kuhusiana na Chuo kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana (kulia) akipokea zawadi ya machapisho kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Naibu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi Bw. Goodluck Chuwa.


Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Chuo. Waliyokaa ni Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Naibu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi Bw. Goodluck Chuwa (Kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Binadamu kutoka Wizara hiyo, Bi. Nkasoru Sarakikya. 



Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana akipanda mti katika eneo la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) alipofanya ziara Chuoni hapo mnamo tarehe 31/05/2024.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana akipanda mti katika eneo la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) alipofanya ziara Chuoni hapo mnamo tarehe 31/05/2024.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni