Na. Francisca Swai-Mahakama, Musoma.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Camillus Wambura hivi karibuni alitembelea Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya.
Katika mazungumzo hayo, IGP Wambura aliipongeza Mahakama kwa ushirikiano mzuri uliopo na Jeshi la Polisi, jambo linalosaidia katika uharakishaji wa uendeshaji wa mashauri ya jinai katika kupunguza uhalifu nchini na kupunguza msongamano wa Mahabusu magerezani.
Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi pia aliupongeza uongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma kwa jitihada kubwa wanazofanya za kuhakikisha mashauri yanasikilizwa kwa wakati, jambo linalosaidia kuleta amani na utulivu katika jamii.
Aidha, IGP Wambura aliupongeza uongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma kwa utunzaji mzuri wa mazingira na kusema ni jambo zuri la kuigwa.
Akipokea pongezi hizo, Mhe. Mtulya alisema kuwa Mahakama haitaweza kutimiza wajibu wake kama inavyopaswa bila ushirikiano dhabiti kati ya Mahakama na Wadau wake, ikiwemo Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Jeshi la Magereza.
Jaji Mfawidhi alisema kuwa, kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma na wadau wake wameweza kuvuka mwaka 2023 bila kuwa na mashauri mlundikano (backlog) na kupunguza msongamano wa Mahabusu magerezani.
Alitolea mfano wa takwimu za wahalifu waliokuwepo katika Gereza la Musoma ambapo ukaguzi uliofanywa, kulikuwa na jumla ya wahalifu (wafungwa na mahabusu) 204, wakati Gereza lina uwezo wa kuhifadhi wahalifu 324.
Mazungumzo ya viongozi hao waliwahusisha pia Majaji wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Marline Komba na Mhe. Kamazima Idd, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Salome Mshasha, Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma, Bw, Leonard Maufi pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, ACP Salim Morcase.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (aliyeketi mbele) akizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Camillus Wambura (wa pili kushoto) pamoja na Viongozi wengine ikiwemo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Salome Mshasha (wa kwanza kushoto), Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma, Bw, Leonard Maufi (kulia) pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, ACP Salim Morcase (aliyekaa nyuma ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Camillus Wambura).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni