Ijumaa, 26 Julai 2024

MAHAKAMA, BENKI YA DUNIA WAMTAKA MKANDARASI MRADI WA UJENZI 'IJC' NJOMBE KUONGEZA KASI

Na Abdallah Salum, Mahakama-Njombe

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama, Mhe. Dkt, Angelo Rumisha sanjari na ujumbe kutoka Benki ya Dunia wamemtaka Mkandarasi, Bw. Lee Manchao kutoka Kampuni ya Shadong inayosimamia ujenzi wa Kituo cha Utoaji Haki (IJC) Njombe kuongeza kasi ya ujenzi wa Kituo hicho ili kukamilisha kwa wakati waliokubaliana.

Agizo hilo lilitolewa jana tarehe 25 Julai, 2024 katika kikao cha pamoja na Mkandarasi huyo kilichohusisha ujumbe kutoka Mahakama ya Tanzania na Benki ya Dunia walipofanya ziara ya ukaguzi wa Mradi wa ujenzi huo.

Kwa upande wake, Kiongozi wa msafara kutoka Benki ya Dunia (WB), Bi. Christine  Owour alisema kuwa, Mradi huo unakwenda  taratibu, hivyo, amewashauri Wahandisi waweze kujadiliana kufikia lengo ili Mradi huo uweze kumalizika kwa  wakati.

Naye, Afisa Mwandamizi kutoka Benki ya Dunia, Bw. Benjamin Mtesigwa aliwashauri Wakandarasi kuwa na mpango kazi ili kufidia muda uliopotea.

Kwa upande wake Afisa Mazingira, Bi. Edina Kashangaki alifanya tathmini ya maendeleo ya ujenzi na kutoa pongezi kwa upande wa wafanyakazi kwamba hakuna unyanyasaji wa kijinsia, lakini pia alipitia mikataba ya wafanyakazi na kuangalia  michango yao  inaingia  kwenye mfuko  wa  NSSF.

Aidha, Mkandarasi wa Mradi huo  alitoa sababu ambazo zimechelewesha kuwa ni pamoja na hali ya hewa iliyochangiwa na mvua nyingi za masika kuanzia  Januari-Aprili mwaka huu pamoja na  vifaa kucheleweshwa kufika eneo husika.   

Mradi wa Ujenzi wa IJC Njombe pamoja na Vituo vingine nane vinavyoendelea kujengwa nchini unafadhiliwa na fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia. 

 

Mhandisi ujenzi IJC Njombe, Bw.Harold Ngumuo (kushoto) akiwaonesha wajumbe kutoka Mahakama na Benki ya Dunia jinsi ramani ya Kituo hicho ilivyokaa na ujenzi unavyoendelea jana tarehe 25 Julai, 2024. Kutoka kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha anayefuata Kiongozi wa Msafara kutoka Benki ya Dunia, Bi. Christine Owour na aliyesimama kushoto kwa Mhandisi Afisa Mazingira, Bi. Edina Kashangaki pamoja na Wakandarasi wengine.

Wakandarasi pamoja na Wajumbe kutoka Mahakama na Benki ya Dunia wakiwa kwenye eneo inapojengwa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki 'IJC' Njombe wakielekea kwenye kikao cha majadiliano kuhusu ujenzi wa Kituo hicho jana tarehe 25 Julai, 2024 wakati ujumbe kutoka Mahakama na Benki ya Dunia walipofanya ziara ya ukaguzi wa Mradi huo.
 
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha (mbele) pamoja na sehemu ya Wajumbe wengine wakiwa katika kikao pamoja na Mkandarasi wa Mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Njombe wakati walipofanya ziara ya kukagua Mradi huo jana tarehe 25 Julai, 2024.
 Mtaalamu wa Manunuzi kutoka Benki ya Dunia,  Bw. Fredrick Nkya akichangia jambo wakati wa kikao kati ya Mkandarasi wa Mradi wa ujenzi wa IJC Njombe na ujumbe kutoka Mahakama ya Tanzania na Benki ya Dunia.
Wajumbe wakifuatilia kinachojiri katika kikao.
 
Wajumbe kutoka Mahakama ya Tanzania, Benki ya Dunia pamoja na Mkandarasi wa Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki 'IJC' Njombe  wakijadili juu ya maendeleo ya ujenzi wa jengo la 'IJC' Njombe.
Muonekano wa mbele wa jengo jipya la 'IJC' Njombe linaloendelea kujengwa likiwa limefikia hatua ya ghorofa ya kwanza.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni