- Kuanzisha Mahakama Inayotembea ndani ya 'SGR'
Na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam
Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi ipo mbioni kuanzisha usikilizaji wa mashauri ndani ya treni ya umeme (SGR) ili kuendelea kusogeza huduma ya utoaji wa haki karibu zaidi na wananchi.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 04 Julai, 2024 na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel katika mkutano na Waandishi wa Habari kuzungumzia historia ya Mahakama na Muundo wake uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia- Temeke jijini Dar es Salaam.
“Tumeshapeleka mapendekezo yetu Wizara ya Uchukuzi na michoro ya namna behewa hilo litakavyokuwa tayari na imeshakubalika. Kwa hiyo, ninaamini huko mbele ya safari kutakuwa na behewa maalum la Mahakama ambalo litakuwa likitoa huduma ya utoaji haki,” amesema Prof. Ole Gabriel.
Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu amesema kwamba Mkakati wa Mahakama uliopo ni kuendelea kutoa huduma bora na kumfikishia mwananchi. Amesema, kwa sasa Mahakama pia ipo mbioni kupokea Mahakama Zinazotembea mpya tatu (3) pamoja na tatu za awali ambazo tayari zimeshapokelewa na kufanya idadi yake kuwa sita (6). Idadi hii itaongeza idadi ya Mahakama hizo kuwa nane.
Akizungumzia zaidi kuhusu suala la kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi, Prof. Ole Gabriel amesema kwamba, kwa sasa Mahakama inaendelea na ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki tisa (IJCs’) katika Mikoa mbalimbali, kukamilika kwa ujenzi wa Vituo hivyo kutafanya idadi yake kuwa 15.
Kati ya Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita vilivyojengwa awali, Mtendaji amewaeleza Wanahabari kuwa mojawapo ni Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke ambacho kinatoa huduma za masuala familia ikiwemo ndoa, watoto na mirathi.
“Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kimetajwa kuwa Kituo cha kwanza barani Afrika na cha pili Duniani kwa kutoa huduma bora za masuala ya familia ikitanguliwa na Singapore ambayo nayo ina Mahakama kama hiyo,” amesema Mtendaji Mkuu.
Kadhalika, amezungumzia majengo ya Mahakama katika kipindi cha nyuma yalikuwa duni na kueleza kuwa kwa sasa yameboreshwa pamoja na kuongeza idadi ya Mahakama katika ngazi zote ambapo idadi ya Kanda za Mahakama Kuu zipo 19, Divisheni za Mahakama Kuu nne (4), Mahakama za Hakimu Mkazi 30, Mahakama za Wilaya 135 na Mahakama za Mwanzo 960.
Mtendaji Mkuu ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutii Sheria Bila shuruti, kufuata maelekezo sahihi ya upatikanaji haki kwa kutokujichukulia sheria mkononi, kutoa ushirikiano kwa Mahakama kwa kutoa Ushahidi.
Kadhalika amehimiza, mashauriano na maridhiano kuanzia ngazi ya familia na hata Taasisi kabla ya kuelekea Mahakamani (Mediation).
Mahakama ya Tanzania imeanzisha utaratibu wa kuzungumza na Waandishi wa Habari kila mwanzo wa mwezi ili kutoa taarifa ya masuala mbalimbali yanayoendelea ndani ya Mhimili huo, lengo likiwa kuwahabarisha wananchi kuhusu maendeleo ya huduma ya utoaji haki nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni