Jumanne, 2 Julai 2024

MAHAKAMA YAWEKA KAMBI SABASABA

Mwenyekiti awaita Wananchi Viwanja vya Mwalimu Nyerere

Mahakama Inayotembea yatoa huduma viwanjani

Na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam 

Mahakama ya Tanzania imeweka kambi katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ‘Sabasaba’, 2024 yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutoa huduma na elimu kwenye masuala mbalimbali ya Mahakama na sheria kwa ujumla.

Kwa mwaka huu, Viongozi na watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau mbalimbali ambao ni watalaam na wabobezi katika masuala ya kisheria wanaendelea kutoa huduma na elimu hiyo kwa muda wote wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ‘Sabasaba’ ambayo yameanza tangu tarehe 28 Juni, 2024.

Katika kipindi chote cha Maonesho hayo, Mahakama inatoa huduma mbalimbali zikiwemo za kusikiliza Mashauri kwenye Mahakama Inayotembea ‘Mobile Court Services’, kutoa Msaada wa Kisheria ‘TLS’, elimu kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mahakamani na safari ya Mahakama kuelekea Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’. 

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi na Maonesho Mahakama, Mhe. Hussein Mushi, ametoa rai kwa wananchi kutumia nafasi adhimu inayotolewa na Mahakama kwa kuwaleta pamoja watumishi wake na wadau katika kutoa elimu ya sheria bure na kuelimisha taratibu mbalimbali za kupata haki mahakamani.

“Nawaomba wananchi kutumia fursa hii ya maonesho kuja kutoa maoni, malalamiko pamoja na kupata msaada wa kisheria kutoka kwa Mawakili-TLS, Kituo cha Haki na Msaada wa Kisheria pia kujua taratibu mbalimbali za kimahakama,” amesema Mhe. Mushi.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi wote wa Dar es Salaam na Mikoa ya karibu kufika katika banda la Mahakama. 

Huduma nyingine zinazotolewa katika banda la Mahakama ni elimu kuhusu huduma na taratibu mbalimbali za ufunguaji wa mashauri, yakiwemo mashauri ya mirathi, elimu kuhusu Mahakama ya Watoto, kuelezea manufaa au faida za Mfumo ulioboreshwa wa Kusajili, Kuratibu na Kusimamia Uendeshaji wa Mashauri (Advanced Case Management System).

Nyingine ni kutoa elimu kwa wananchi kutambua umuhimu wa kutumia Kituo cha Huduma kwa Mteja ‘Call Centre’ ya Mahakama ya Tanzania kutoa malalamiko na maoni yao.

Kueleza huduma zinazotolewa na ngazi mbalimbali za Mahakama ikiwemo Divisheni za Mahakama Kuu na Kituo cha Usuluhishi.

Katika kipindi chote cha Maonesho hayo, Mahakama ya Tanzania ipo pamoja na baadhi ya Wadau wake ambao ni Tume ya Utumishi wa Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Chama Cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) pamoja na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) ambao wote watatoa elimu kuhusu maeneo yao.

Wadau wengine ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST).

Muonekano wa nje wa banda la Mahakama ya Tanzania lililopo ndani ya Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam ambapo Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa 'Sabasaba' yanaendelea kufanyika. Maonesho hayo yameanza tangu tarehe 28 Juni, 2024 na yatafikia tamati tarehe 13 Julai, 2024.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi na Maonesho Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Mushi akizungumzia kuhusu ushiriki wa Mahakama katika Maonesho ya 'Sabasaba'. Amewakaribisha wananchi kutembelea banda hilo ili kupata elimu kuhusu masuala ya sheria.
Sehemu ya wananchi waliotembelea banda la Mahakama wakipata ukaribisho na maelezo ya awali kutoka kwa watumishi wa Mahakama waliopo katika banda la Mapokezi.
Watumishi wa Mahakama katika banda la Maboresho/Usimamizi wa majengo wakiwa tayari kuhudumia wateja katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa 'Sabasaba' yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Wananchi wakipata elimu kuhusu umuhimu wa kutatua migogoro kwa njia ya Usuluhishi kutoka katika banda la Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Mashauri-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hawa Mnguruta (kushoto) akitoa maelezo kwa mwananchi aliyetembelea banda la Kurugenzi hiyo iliyopo katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa 'Sabasaba', 2024.
Wananchi wakiendelea kupata huduma katika banda la Kurugenzi ya Usimamizi wa Maadili na Ukaguzi wa Huduma za Mahakama pamoja na Kituo cha Huduma kwa Mtaje cha Mahakama (Call Centre).

Wananchi wakipata huduma katika banda la Chama cha Mawakili Tanganyika lililopo ndani ya banda la Mahakama ya Tanzania kwenye Maonesho ya 'Sabasaba'.
Wananchi wakipata huduma na elimu kuhusu masuala ya Mirathi kutoka kwa Mahakimu Wakazi wa Kituo Jumuishi cha Mahakama cha Masuala ya Familia (Ndoa, Mirathi na Watoto) Temeke.
Hakimu Mkazi Mahakama ya Watoto-Temeke, Mhe. Orupa Mtae (kushoto) akiwahudumia wananchi kuhusu elimu ya Mahakama hiyo.
Mwajiri naye yupo; Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (upande wa kulia) wakitoa maelezo kuhusu Tume hiyo kwa wananchi waliowatembelea. Tume ya Utumishi wa Mahakama nayo ipo ndani ya banda la Mahakama ya Tanzania katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa 'Sabasaba', 2024.
Mwananchi (kushoto) akipata huduma katika banda la Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) lililopo ndani ya banda kuu la Mahakama ya Tanzania.
Kituo cha
 Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nacho kipo ndani ya banda la Mahakama kwenye Maonesho ya 'Sabasaba'.
Banda la Idara ya Kumbukumbu na Huduma za Maktaba ikionesha na kuelezea kumbukumbu mbalimbali za Mahakama ya Tanzania, tulipotoka na tulipo sasa.
Mahakama Inayotembea nayo iko Viwanja vya 'Sabasaba' kuhudumia wananchi.
Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi (kulia) wakitoa maelezo kwa mwananchi kuhusu Divisheni hiyo kwa mwananchi aliyetembelea banda hilo.
Kikosi kazi kazini; sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Wadau wa Mahakama wanaotoa elimu ya Mahakama na sheria kwa ujumla wakiwa katika picha ya pamoja mbele ya banda la Mahakama lililopo katika Viwanja vya 'Sabasaba' jijini Dar es Salaam.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni