Na PAUL PASCAL –Mahakama, Moshi
Mahakama ya Wilaya Rombo mkoani Kilimanjaro imeendesha mafunzo kwa Wadau wa Mahakama na Mahakimu wa Wilaya hiyo juu ya namna ya kujiepusha kurejesha jeraha kwa wahanga wa ukatili wa kingono.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo leo tarehe 26 Julai, 2024 yanayofanyika katika Ukumbi wa wazi wa Mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Rombo, Mhe Nuruprudensia Nasari amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwapa uelewa wa pamoja katika kujiepusha kutonesha jeraha kwa wahanga wa ukatili wa kingono wakati wanapotekeleza majukumu ya utoaji haki ambalo kimsingi ndio jukumu kuu la Mhimili huo.
“Kwanza niwashukuruni nyote kwa kushirikiana na sisi katika dhamira hii yetu ya kuhakikisha tunaiihudumia jamii yetu pasi na kuwakwaza wala kusababisha malalamiko niweke wazi pamoja na mambo mengine niwaombe kutumia fursa hii ya kujifunza mambo haya kwa umakini ili sote tuweze kuzungumza lugha moja pale tunapokuwa na mazingira ya kumuhudumia mtu mwenye jeraha la uhanga wa ukatili wa kingono,” amesema Mhe. Nasari.
Naye Mkufunzi wa mafunzo hayo ambae pia ni Hakimu Mkazi Mkuu, Mhe. Ruth Mkisi aliwaelezea washiriki kwamba, chanzo na dhima ya mafunzo hayo ni kujijengea uwezo ili kujiepusha na lawama kutoka kwa jamii wanayoihudumia na hivyo kuwasihi kuwa na utulivu ili waweze kufikisha yale yote waliyoyaandaa kwa ajili ya washiriki hao.
“Mafunzo haya awali yalitolewa na wenzetu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa Ufadhili wa (Irish Rule of Law International) lakini leo hii Mahkama ya wilaya Rombo wamewaza mbali na kuona ni vema sote kwa pamoja tukapata mafunzo haya,” amesema Mhe. Mkisi.
Mafunzo hayo yamejumuisha jumla ya washiriki 16 kutoka Ofisi za Wadau wa Mahakama katika mnyororo wa utoaji haki ambao ni Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali Wilaya ya Rombo, Mawakili wa Kujitegemea kutoka Chama cha Mawakili (TLS), Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na maafisa Ustawi wa jamii wa wilayani humo.
Mafunzo hayo ni ya siku moja na mada zitakazowasilishwa kwa washiriki ni pamoja na namna bora ya kujiepusha na kurejesha jeraha kwa wahanga wa ukatili wa kingono. Mada hizo zimeandaliwa na Chuo Cha Uongozi wa Mahakama (IJA) katika mafunzo yaliyofanyika mkoani Arusha ambapo kila mkoa ulitoa washiriki.
Mahakama ya Wilaya Rombo imeandaa mafunzo hayo ili kuwawezesha wahusika wote katika mnyororo wa utoaji Haki kuwa na uelewa wa pamoja.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Rombo, Mhe. Nuruprudensia Nassari akitoa hotuba ya ukaribisho kwa washiriki wa mafunzo juu ya namna ya kujiepusha kurejesha jeraha kwa wahanga wa ukatili wa kingono leo tarehe 26 Julai, 2024 katika ukumbi wa Mahakama hiyo.
Hakimu Mkazi Mkuu na Mkufunzi katika mafunzo hayo, Mhe. Ruth Mkisi akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo ya namna ya kujiepusha kurejesha jeraha kwa wahanga wa ukatili wa kingono (hawapo katika picha).
Mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Ofisi ya Ustawi wa Jamii wilayani Rombo akichangia mada wakati mafunzo hayo yakiendelea.
Washiriki na wakufunzi wakiwa katika picha ya pamoja mbele ya jengo la Mahakama ya Wilaya ya Rombo mara baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo yaliyofanyika leo tarehe 26 Julai, 2024 katika ukumbi wa Mahakama hiyo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni