Jumatano, 3 Julai 2024

UONGOZI MAHAKAMA SACCOS WAFANYA ZIARA MAHAKAMA KANDA YA TABORA

  • Yahamasisha Watumishi kujiunga na SACCOS
  • Yataja faida lukuki za SACCOS hiyo

Na Amani Mtinangi Mahakama Kuu Tabora

Viongozi wa Bodi ya Mahakama SACCOS jana tarehe 02 Julai, 2024 walitembelea Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora na kuonana na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora wakiwemo Majaji wa Mahakama hiyo lengo likiwa ni kufanya semina na watumishi sanjari na kuhamasisha watumishi wa Kanda hiyo wasio wanachama kujiunga na SACCOS hiyo.

Akizungumza na Viongozi wa Mahakama SACCOS ofisini kwake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi aliwapongeza kwa kufika katika Kanda hiyo na kuwahimiza kuwekeza katika fursa mbalimbali za kiuchumi ili kukuza mapato ya SACCOS, kuweka mifumo rafiki ya kujiunga hasa ya kidijitali ili kuifanya iwe ya kisasa na inayoendana na mabadiliko ya kiteknolojia.

“Kwanza niwapongeze kwa kututembelea Tabora, ninawashauri mjitahidi sana kuangalia fursa za uwekezaji muwekeze huko ili kukuza mtaji wa SACCOS na muweke mifumo rafiki ya kujiunga na kwenda kidijitali ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi. Mkifanya hivyo mtaweza kuendesha Chama vizuri na kuongeza wanachama na kuwasaidia wanachama hivyo kuwa msaada kwao na Mahakama,” alisema Mhe. Dkt. Mambi.

Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Jaji Dkt. Zainab Diwa Mango aliwaeleza umuhimu wa kutumia fursa na jukwaa mbalimbali za Mahakama kuhamasisha watumishi kujiunga na chama hicho chenye fursa nyingi za kukua na kujitangaza na kuwahimiza watumishi kujiunga pamoja na kuwatafutia wanachama fursa mbalimbali za kiuchumi na kimaisha.

“Jitahidini kutumia majukwaa ya Mahakama vizuri kwa  kujitangaza maana hayo ndio yenye wanachama wenu na yatawajenga kujua maoni yao, lakini pia watafutieni wanachama wenu fursa za kiuchumi na kijamii kama viwanja ili kuwainua na kuwahamasisha kujiunga na SACCOS,” alisema Mhe. Dkt. Mango.

Naye, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Bw. Emmanuel John Munda, aliwahimiza Viongozi hao kufanya ziara na semina mikoani na kuwekeza katika mifuko ya uwekezaji ili kujipatia faida kwa ajili ya wanachama wake.

“Ninawashauri muangalie namna ya kufanya ziara za mikoani na kuwekeza katika masoko mbalimbali ya mitaji na hisa, uwekezaji huo utakuza kwa haraka mtaji na kuwanufaisha wanachama,” alisema Bw. Munda.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mwenyekiti wa Bodi ya Mahakama SACCOS, Mhe. Ferdinand Moshi Philip alisema watumishi wa Mahakama wanapaswa kujisikia fahari kujiunga SACCOS hiyo kwa sababu ina mtaji wa kutosha na huduma zinaendelea kuboreshwa ambapo kwa sasa ipo katika maandalizi ya kuingia katika uendeshaji wake kidijitali na kwamba tayari imeanza kuwekeza katika Taasisi mbalimbali.

“Ninawasihi sana watumishi wenzangu jiungeni na mjisikie fahari kuwa wanachama wa Mahakama SACCOS kwa sababu ina mtaji wa kutosha, huduma bora na ipo mbioni kufanya shughuli zake kidijitali,” alisema Mhe. Phillip.

Ziara hiyo imeleta matunda makubwa kwa watumishi kwa kuwawezesha kuijua vizuri na kupata wanachama wapya waliojiunga ikiwemo Viongozi kadhaa wa ngazi ya juu wa Taasisi ambao walielezwa kuwa Chama hicho kimepiga hatua kubwa kuingia katika zama za kidijitali hivyo kuwa msaada kwa watumishi.

Viongozi wengine wa Mahakama waliokuwa kwenye ziara hizo ni Yusuph Kaungu Mjumbe wa Bodi na Bi. Janeth Primus Mwanisawa Mjumbe wa Bodi.

Mahakama SACCOS ni Chama kilichoundwa kwa lengo la kuwa suluhisho la mtaji, kuleta watumishi wa Mahakama pamoja ili kufanikisha malengo yao.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mahakama SACCOS. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Mahakama SACCOS, Mhe. Ferdinand Moshi Philip, wa kwanza kulia ni Mjumbe wa Bodi, Bi. Aisha Yusuph Kaungu, wa pili kulia ni Mjumbe wa Bodi, Bi. Janeth Primus Mwanisawa na wa kwanza kushoto ni Mwakilishi wa SACCOS Mkoa wa Tabora, Bw. Antony Mayamba.
Viongozi wa Mahakama SACCOS wakifanya mazungumzo na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Zainab Mango (aliyeketi mbele) wakati viongozi hao walipomtembelea ofisini kwake Mahakama Kuu Tabora.
 
Mwenyekiti wa Bodi ya Mahakama SACCOS, Mhe. Ferdinand Moshi Philip akitoa semina katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, wengine katika picha, wa pili kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Bw. Emmanuel John Munda wa kwanza kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya Mahakama SACCOS, Bi. Aisha Yusuph Kaungu na wa kwanza kulia ni Mjumbe wa Bodi ya Mahakama SACCOS,  Bi. Janeth Primus Mwanisawa.

Msaidizi wa Kumbukumbu Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Bw. Hanzuruni Kalimwage akichangia jambo wakati wa semina. Wengine katika picha ni watumishi wa Mahakama hiyo wakimsikiliza.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni